Wiki iliyopita ilikuwa ni siku ya akina mama
duniani. Hivyo, kijiwe hakikubaki nyuma. Kwani, nani hana bibi, dada, mama au
shangazi ndipo asiwajali wala kuwasaidia akina mama popote walipo? Hata mitume
walikuwa na.? Kwa kuzingatia hili, wanakijiwe–wa vile ni magwiji wa haki za
binadamu na usawa–hawakubaki nyuma. Baada ya kuamkuana tulikubaliana; kila
mmoja aelezee alivyosherekea siku hii adhimu.
Tukiwa
hatuna hili wala lile, Mgoshi Machungi wa Shekiango ndiye anaanzisha mada.
Anakunywa kahawa yake na kuronga huku akitabasamu kwa mbwembwe na bashasha
“mwenzenu kwenye siku ya akina mama niimsaidia bi mkubwa kupeeka kitegemezi
zahanati kue Mashindei Ushoto. Niipofika kue niipigiwa vigeegee kwa sana na
akina mama waiokuwa wamepeeka vitegemezi vyao kucheki afya zao.”
Mijjinga alipoka mic na kuchekesha kijiwe.
Alisema “mimi tokana na mapenzi makubwa kwa bi mkubwa wangu, siku hiyo,
niliamua kwenda kisimani kuchota maji. Acha maji yanimwagikie ukiachia mbali
kushindwa kubalance ndoo ya maji kichwani.”
Mbwamwitu anamchomekea “usemayo kweli au
unataka kuchekesha kijiwe? Haya mahaba yameanza lini; hebu tujuze tukuelewe.”
Mijjinga alijibu “nidanganye nini wakati
hicho ndicho nilichofanya? Unanishangaa mimi kubeba ndoo ya maji kichwani?
Mbona humshangai yule waziri mdogo wa maji aliyetundika ndoo kichwani tena si
kwa ajili ya bi mkubwa wake bali kwa ajili ya kuzindua kijimradi kidogo cha
maji kule Mji Kasoro Bahari?”
Kabla ya kuendelea Mbwamwitu anachomekea
“nasikia kule UG M7 alisherehekea sikukuu ya akina mama kwa kumwacha bi mkubwa
wake atawale tokea bedroom.”
Kijiwe kinacheka na kuvunja mbavu juu ya
usanii huu wa kisiasa. “Nani anataka waziri anayebeba ndoo? Tunataka waziri
anayeleta maji kwenye mabomba siyo visima” anachomekea Kapende.
Mpemba naye hakutaka kuachwa nyuma. Anakwapua
mic na kuronga ‘wallahi mie hiyo siku nlimpikia bi Nkubwa pilau ya kukata na
wembe. Hata hivyo nilipatikana hasa ikizingatiwa twatumia jiko la nkaa. Huo
moshi ulivoniumiza matoni wala sina nfano.”
Da Sofia Lion aka Kanungaembe anamkonyeza Gau
Ngumi aka Linungaembe. Leo Sofia kaupara kama hana akili nzuri! Baada ya
kumaliza kukonyezana na mwenzio da Sofia anasarandia mic na kunena “kijiwe cha
leo cha kihistoria. Kwani, inapendeza kwa baba kumsaidia mama hata kama ni mara
moja kwa mwaka. Mie ningeshauri huu moto wa mahaba mliowasha wala msiuzime.
Endeleeni kuwasaidia wake zenu japo mjifunze na kujua masahibu yao. Au vipi
kaka zangu?’
Kanji kuona hivyo naye anaamua kuonyesha
mapenzi ya kigabachori. Anakula mic “mini kosaidieni mama kwenda dukani ya maua
nanunulia yeye maua.”
“Halo halo! Veve Kanji hiyo kazi nafanya iko
dogo sana. Mimi ile siku iko nabeba toto na kubembeleze yenyeve hadi bi kuba
nafurahi sana kwa moyo, mwili na roho. Kwani hiyo bibi yako iko zungu au mbuzi
hadi naleta majani kwa yeye?” anachomekea Mchunguliaji.
Bwana mdogo Mchunguliaji kama ni mashindano
naona hunifikii mimi. Kwani, nilitandika kitanda na kumbeba bi Mkubwa hadi
nikamlaza salama salimini kwa furaha na maraha.”
Msomi Mkatatamaa aliyekuwa kimya anaamua
kutia guu “mwenzenu mie sikumsaidia mke wangu. Huwa sipendi lugha hii tamu ya
kusaidia. Nilichofanya ni kuwajibika kwangu kwake. Hata hivyo, siku hii adhimu
nilikuwa na kibarua cha kumfanyia homework yake. Mwenzenu shemeji yenu anasomea
shahada yake ha upili kwenye Uongozi na Utawala Bora. Japo huwa nawajibika kwa
kufanya mambo mengi ambayo wengi wanaonekana wameyafanya. Sidhani kama tutakuwa
wa kweli kuwasaidia wenzetu siku moja kwa mwaka ni jambo la kujivunia.”
Kabla ya kumalizia tunaangaliana kwa aibu na
mstuko namna Msomi anavyotusuta.
Kabla ya aibu ya kusutwa kuzama si Mipawa
akaja na mpya ambaye ilitusahaulisha yote! Bila kuonyesha chembe ya woga wala
shaka anasema “kama kuwasaidia washirika zetu wa bedroom ni kukvunja rekodi
basi mie ndiyo nimeweka rekodi mpya. Kwani, pamoja na kumfanyia mambo yote
mengi ambayo sina haja kutaja, cha mno nilimsukaga nywele akapendeza hadi
nikahisi wivu usipime. Alipowaambia mashoga zake kuwa mie ndiye niliyekuwa
nimemsuka walishangaa sana hadi wakamshauri tufungue saluni nikagoma.”
Wakati tukiwa tunakenua si Mzee Maneno akatoa
mpya. Alisema “mwenzenu mie nilideki nyumba na kuhakikisha kuwa najazia maji
kwenye mboga.”
Kabla ya kuendelea, Mbwamwitu anamchokoza
“ulivaa na gagulo siyo?” kabla ya kuendelea sim zee Maneno akaamka na kutaka
kumtia mikono! Huku akiwa amechukia aliuliza “je baba yako huwa analivaa hilo
gagulo unaloona la maana sana siyo? Koma na ukomae na ushike adabu ikushike
kabla sijakushikisha adabu. Wewe ni wa kuniambia kuwa nilivaa gagulo? Mimi siyo
saizi yako. Kama utani mali basi naweza kutaniana na baba yako au mama yako.”
Huku tukiwa hatukutegemea, mzee Maneno
anaamka kutaka kumshikisha adabu kweli Mbwamwitu ambaye bila kukawia anaamka na
kutoka mkuku huku tukibaki tukiwa tumeghubikwa na taharuki tusijue la kufanya!
Kapende anahanikiza na kusema “siku ya akina
mama hoyee!”
Je wewe umesherehekeaje?
Chanzo: Tanzania Daima leo Machi 14, 2018.
No comments:
Post a Comment