Baada ya wanene kuzinduka kwenye
lepe zito la usingizi ambapo waliachia kila kitu kijiendee chini ya tawala
uchwara zilizopita zikisifika kuridhia ufisadi na wizi wa fedha na mali za umma,
kijiwe kimekaa kama kamati kupongeza hatua za makusudi zilizopelekea kupigwa
chini miziki na nyimbo chafu kayani.
Leo
Kapende ndiye anaanzisha mada. Anakunywa kahawa yake na kuzoza “jana mliona
namna wanene walivyoamua kutolea uvivu mila chafu kwa kupiga marufuku baadhi ya
nyimbo na miziki michafu? Japo wamechelewa kulienga hili, hapa kusema ukweli
wamenikuna; na nawapongeza japo sitaki walemae tokana na pongezi hizi. Pia, napendekeza
wote waniocheza na kuchezea mambo machafu kama vile kigodoro wanyongwe huku
wale wote wanioshabikia wafungwe maisha.”
Kabla
ya kuendelea Mbwamwitu anamchomekea “unasema wanene wamekukuna; wamekukuna vipi
na wapi? Hebu ongea tukuelewe na ueleweke.”
Kabla
ya kujibu, Mipawa anakula mic “tuache utani. Hali ilikuwa imefikia pabaya kiasi
cha kushindwa kutofautisha kama kaya yetu ni
ya vyangu au wanyama. Maana chini ya utaahira wa kuigiza majuu, ilifikia
mahali wachovu wakaanza kutembea uchi kama vile wale wanaovaa milegezo
wakionyesha michupi yao michafu. Natamani kila mwanakijiwe atembee na bakora
ili tuwavue hiyo milegezo na kuwanasa bakora kama siyo kuwafanyia kitu mbaya au
vipi?”
Mzee
Maneno anampoka Mipawa mic na kudema “kama ulipopiga na kugusa ndiyo penyewe
mzee mwenzangu. Ni kweli kaya yetu imejiruhusu kudhalilishwa na mataahira
wachache wanaosumbuliwa na ujinga na ulimbukeni kwa kisingizio cha usanii na
kutafuta njuluku. Mie napendekeza hawa watembea uchi nao wafungwe maisha ili
wakaozee lupango. Maana nao wanachochea ubakaji na udhalilishaji wa akina mama
hasa wale wasiotaka kujidhalilisha na kudhalilishwa.”
Mijjinga aliyekuwa akimaliza kuvuta kipisi cha
sigara kali anaamua kutia guu “napedekeza wasanii wa kigeni waliojazana kayani
wakieneza uchafu kama wale waliosamehewa kwa makosa ya ubakaji watimliwe kayani
haraka. Maana wanachafua maadili yetu huku majuha wengi wakichekelea na
kuhadaiwa kuwa hii ni burdani. Burdani gani ya kudhalilishana?”
Kabla
ya kuendelea Kanji anakula mic “veve sema jambo kuba sana. Kama hii geni nakuja
cheja ngoma itaendelea na chafu yao kaya yetu navezapoteza hishma. Kama iko
vachowu nataka burdan ya uchi kama nyama basi iende fungia kwa nyumbani yao
ifanye chafu yao. Kama nataka faidi basi iende funga kwenye bedrooms zao na
kuenjoy hii laana zao.”
Kabla
ya Kanji kuendelea, da Gau Ngumi Nungaembe anakula mic “jamani hali inatisha na
kukatisha tamaa. Sijui nani aliyeroga kaya hii? Kwanini kuwaonyesha vichanga
mambo ya kiutu uzima. Wakifyatuka na kuanza kuushobokea mnawalaumu wakati
mliruhusu nyie wenyewe kwa ujuha wenu.”
Msomi
Mkatatamaa anaamkua kutia guu “naungana na wasemaji wote waliotangulia kuwa
kuna tatizo tena la kimfumo si kuhusiana na maadili tu bali mambo yote. Tumegeuka
shamba la bibi kwa kila kitu. Tumegeuka tegemezi kiasi cha kutia kinyaa. Yaani tunaruhusu
wachafuzi wa maadili toka kaya jirani kana kwamba sisi hatuna muziki wetu kama
kaya? Nakubaliana na wanaohoji aliyeturoga. Nadhani baada ya Mzee Mchonga
kutuonya tukashinda kumeuelewa, sasa tunalipia kwa bei mbaya zaidi. Hebu tuwe
wakweli. Unaposamehe wabakaji zaidi ya kuwapa motisha wabakaji wengine ambao
hawajapatikana unafanya nini? Hivi kweli hili nalo linahitaji uwe mwanasheria
ndiyo uelewe?”
Mpemba
aliyekuwa akiteta jambo na mgoshi Machungi Shekiango anakula mic “yakhe hata
mie hili lantisha. Sijui kama hawa watoto walobakwa wangekuwa wa wanene kama
wangefikiri, achia mbali kusamehe hawa wahalifu ambao sasa wametumia fursa hii
kuwa masupastaaa. Watu wazima na akili zao watembea uchi kama wanyama huku
wengine wakitanatana nguo eti wadai hii fasheni wakati ni ulimbukeni, umajinun
na ulimpyoto. Mboni hao watasha wanioigizwa hawaigizi fasheni zetu?”
Kabla
ya kuendelea Mchunguliaji anadakia “Ami umeniacha hoi na hilo neno kutanatana
lamaanishani?”
Mpemba
anajibu “kutana huku bara mwaita kuchana sie twasema kutana. Hata njia huita
ndia wakati nyie huku mwasema njia.”
Mgoshi
anaamua kula mic “kama hawa waiosamehewa ubakaji wangekuwa Ushoto bia shaka
tingewatwanga zongo angaau waewe tisivyocheza na utu wetu. Kwa kwei inaniuma
sana kuona watoto wetu wanahaiibiwa haafu wae waiofanya hivyo wanaachiwa
kiahisi. Huu ni udhaiishaji wa akina dada na mama. This is unfair kusema ue
ukwei.”
“nyie
mnaongelea miziki michafu. Nani anaongelea lugha chafu kwenye madaladala? Nani anaongelea
lugha chafu kwenye magazeti ya uchafu? Nani anaongelea lugha chafu maofisini ambako
dada zetu wanadhalilishwa kila uchao? Nani anaongelea uchagudoa kila kona hadi
kwenye makaburi na mitaani kwetu? Sofia Lion aka Kanungaembe analalamika huku
akikatua kasha yake.
Kijiwe
kikiwa kinanoga si akapita binti mmoja alonjaza huku miguu kama chelewa akiwa
amevalia kijisuruali kilichochanwa chanwa na kubana manonihino yake utadhani
yatapasuka. Acha tumtoe mkuku tukimzomea kabla ya kukimbilia kwenye kijiduka jirani
hadi ndata walipotutawanya tusimfanyie kitu mbaya!
Chanzo: Tanzania Daima, Machi 7, 2018.
No comments:
Post a Comment