Heko Rais Magufuli

Wednesday, 7 March 2018

Usafi wa kila wiki umeishiwa wapi?

See the source image
            Kwa busara zake, rais John Magufuli alipoanzisha zoezi la viongozi na watumishi wa umma kufanya usafi kwenye maeneo yao kila wiki, pindi tu alipoingia madarakani. Magufuli alidhani wasaidizi wake wangemwelewa na kulifanya endelevu nchini kote ili kuondokana na kadhia ya uchafu. Lakini wapi; hii haikuwa. Nikikumbuka watu walivyochangamka na kuhamanika rais alipoanza kufanya usafi, inakuwa vigumu kuelewa kama wanakumbuka walichofanya na athari zake kwa umma ukiachia mbali matarajio ya umma. Pamoja na ulazima na uzuri wa zoezi hili, kwa sasa ni kama limekufa au kutelekezwa. Sijui wahusika wanangoja tena rais aingie mitaani na ufagio nao ndipo watoke kwenye usingizi wao wa pono kiutendaji. Inasikitisha kuona juhudi mahsusi za rais zikifishwa kirahisi tokana na wasaidizi wa rais kukosa ubunifu na uelewa juu ya dhana nzima ya kuwa na nchi yenye mazingira safi kwa usalama na  ustawi wa watu wake.
 Usafi ni tabia. Kama wahusika wangekuwa na tabia hii, bila shaka, wasingeacha muda mfupi baada ya kumridhisha rais. Badala yake wangepanua zoezi hili hata kuongeza muda wa kujitolea kufanya usafi. Kimsingi, zoezi hili halikupaswa kuwa endelevu tu bali lilipaswa kuwahusisha watanzania wote. Kwani usafi ni kwa faida ya watanzania na si kwa faida ya rais. Inasikitisha kuona watendaji wetu wakipata muda wa kufanya mambo mengine ya hovyo huku wakilipa mgongo zoezi la usafi kitaifa. Kwa sasa, taifa la Rwanda linasifika, kuheshimika kimataifa kutokana na kuwa na zoezi endelevu la usafi kitaifa. Je hapa tatizo ni nini? Je rais ataanzisha na kusimamia mambo mangapi wakati watendaji wake wa chini wakiendelea kuhujumu adhima yake ya kufanya Tanzania kuwa taifa safi?
Viongozi wetu wengi si wabunifu.  Baada ya kuanzisha zoezi hili, wengi tulidhani kuwa watendaji wetu watastuka na kuona faida za usafi kama taifa na kama watu. Badala yake sasa, wengi wamejikita kwenye mambo ya kisiasa zaidi ya kuitendaji kama vile wakuu wa mikoa na wilaya kujiingiza kwenye kampeni za kisiasa wakati ni kinyume cha sheria kwa nafasi zao zinazowataka wawahudumie watanzania bila kujali itikadi na mafungamano yao. Nadhani hapa kinachokosekanan ni visheni na vipaumbele mahususi hasa tukizingatia umuhimu wa usafi katika maisha ya binadamu. Inashangaza na kukatisha tamaa kuona watendaji wetu wameridhika na kadhia hii kiasi cha kuifanya jambo la kawaida. Wamekosa mikakati bunifu na endelevu kukabiliana na kadhia ya uchafu nchini. Wengi wa watendaji wetu wanangoja rais aanzishe jambo ndipo wao waitikie tena wengi kwa woga na nguvu ya soda. Si katika usafi tu ambapo watendaji wetu wanapawa. Wiki chache zilizopita niliongelea namna idara zinazoshughulikia maadili zinavyomuangusha rais na watanzania kwa kufumbia macho magazeti na vyombo vya habari vinavyoeneza mambo yanayokinzana na kudhalilisha utamaduni wetu kama taifa. Hata hivyo, tabia hii haiishii hapa bali kuonyesha woga na ukosefu wa ubunifu. Kwani baada ya muda, hurejea kwenye mazoea yao kama ilivyo kwenye suala zima la maadili alilopigia kelele rais hivi karibuni ambapo waziri alikuwa amekaa tu akisuburi rais aseme ndipo achukue hatua. Kama ilivyo, ada, baada ya muda, sitashangaa kuona kauli ya rais ikipuuzwa na wahusika kuendelea kufanya ushenzi wao. Tutaendelea na uzembe huu hadi lini wakati taifa likizidi kuteketea tokana na tabia mbovu kama hizi?
Rais ana shughuli nyingi kitaifa na kimataifa. Isitoshe yeye ni binadamu.  Hawezi kufanya kila kitu kila mahali. Wasaidizi wake wanapaswa kumsaidia badala ya kungoja kila jambo litoke juu kwenda chini. Tutaanza lini kuendesha mambo yetu kwa staili ya toka chini kwenda juu au from down up?
Ukiachia mbali na rais Magufuli, ni waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina anayeonekana kuchapa kazi vilivyo akifuatiwa na waziri wa afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anayeonekana kuchakarika vilivyo kutekeleza majukumu yake. Hawa wawili na wengine ambao, kwa kiasi fulani, wameonyesha kujua wanachofanya, tunawapongeza na kuwapa heko waendelee na juhudi zao.
Ukienda kwenye miji, masoko, mahospitali hata makazi yetu mengi ni machafu tokana na kukosekana ubunifu katika kupambana na uchafu. Tunazo sheria nzuri za usafi. Je zinasimamiwa na kutumiwa vilivyo? Usafi ni nyenzo mojawapo ya kupambana na magonjwa kama vile kipindupindu ambacho kimekuwa kikihagaisha taifa letu kama ushahidi kuwa sisi ni taifa chafu. Je hili nalo litakaa limngoje rais ambaye ana majukumu mengi? Hapa hatujaongelea kadhia nyingine kama vile ufisadi, wizi wa fedha na mali za umma, uzembe na jinai nyingine zinazogharimu taifa.
Tumalizie kwa kuwataka watendaji wetu nchini waamke toka kwenye usingizi na kupambana na uchafu katika maeneo yao. Tunawaasa waupe usafi kipaumbele ili taifa letu nalo lijikwamue kutokana na kadhia hii ya uchafu.
Chanzo: Tanzania Daima, Machi 7, 2018.
 

No comments: