Baada
ya mamlaka kuwaijia juu waharibifu wa maadili yetu, kama Kijiwe tumekaa
kuzipongezana kuwaonya hata kuwalaani wale wanaojiona wao ni masupastaa japo ni
masupastaa uchwara waliolewa sifa kiasi cha kuanza kujiona wao wako juu ya
sheria.
Mgoshi Machungi mwana wa Mashindei
analianzisha ‘hivi jamani juzi muimsikia msanii fuani akidai eti wazii
amemhujumu kwa kupiga maufuku upuuzi wao unaokiuka maadii ya kaya?’
Kabla ya kuendelea, Mbwamwitu anamkwanyua mic
“unaongelea hawa malimbukeni wetu ambao wamelewa sifa zitokanazo na usupastaa
uchwara siyo? Nafurahi kuwa mamlaka
zimeanza kula nao sahani moja kuhakikisha wanafuata maadili ya kaya. Maana,
chini ya tawala za kilimbukeni zilizopituka, kaya ilikuwa imegeuka dampo la
kila aina ya uchafu wa kiutamaduni wa kigeni.”
Mijjinga aliyekuwa anamalizia kikombe chake
cha kwanza cha kahawa anaamua kutia guu “ni kweli, kaya yetu iligeuzwa dodoki
la kunasa kila uchafu wa kigeni kiasi cha kuanza kuonekana kama ni jamii ya
mataahira au wendawazimu wasiojitambua. Hivyo, kama wanakijiwe, nashauri
tuwalaani wajalaana hawa huku tukiziimiza mamlaka kuwapa kibano hadi wakome na
kukomaa. Haiwezekani tukaendelea kuendekeza njaa huku tukichekwa na kaya za
jirani kwa ujuha na upuuzi huu utokanao na ujinga na ulimbukeni.”
Msomi Mkatatamaa anaamua kula mic “japo mada
hii inaweza kuonekana si muhimu, tukiangalia tulipo, tulipotoka na
tunakokwenda, kuna haja ya kutafakari kwa kina. Juzi nilimsikia Denjamani
Makapi akilalamikia ilmu kuwa imeendelea kudorora wakati naye alichangia kuiua.
Siku hizi usanii uliojaa ulimbukeni na ukosefu wa maadili umegeuka chanzo
kimojawapo cha matokeo ya kifo cha ilmu yetu kama kaya. Vijana siku hizi
hawataki kusoma. Badala yake wanatumia muda mwingi kuimba upuuzi ili wapate
njuluku na kuukata kirahisi. Zamani haikuwa hivi. Je tutageuka kaya ya wasanii?
Nni wataendesha kaya huko tuendako iwapo hatutakuwa na wataalamu wa kutosha
tena wanaojitambua? Hii ukiiangalia inatisha sana. Hata hivyo, nashukuru kuwa
dingi ameliona hili na kuamua kulishikia bango japo sijui kama wasaidizi wake
wataendelea na msimamo huu. Maana wengi wanafanya kazi kwa mazoea na kutafuta
kiki ili wasitumbuliwe au kutimliwa.”
Kabla ya kuendelea, Kapende anamchomekea
“unaongelea njomba Makapi siyo? Japo anachosema kina mashiko, amekumbuka
blanketi asubuhi hasa ikizingatiwa kuwa naye ni sehemu ya tatizo. Waliua ilmu
kwa kuendekeza ulaji kiasi cha sasa kuanza kulalamika. Mlikuwa wapi wajalaana
nyie ambao mlipeleka vitegemezi vyenu kwenye skuli za binafsi na ughaibuni huku
mkiua elimu na mfumo mwetu? “
Kanji naye anaamua kula mic “hii leo iko
naongelea ilm. Kesho tasikia nalalamikia afia. Yeye nasomesha toto yake
ghaibuni natibiwa Bombey kama naugua. Kwani kama taua ilm au afia takosa nini
vakati vanalipiwa vitu yote ugaibuni?”
Kapende aliyekuwa ametoka kuongea na mshirika
wake wa bedroom anaamua kula mic “kimsingi, kumekuwa na kuendekezana chini ya
usupastaa uchwara. Hamsikia limbukeni mmoja akimlalamikia waziri kuwa amemtilia
mtima nyongo kwa kupiga marufuku nyimbo zake za kipashkuna akidai kuwa kufanya
hivyo kunafanya vitegemezi vyake vikose riziki kana kwamba lazima riziki
itokane na sanaa chafu? Hata hivyo, ana bahati vinginevyo ilibidi afungiwe
maisha ili akauze maandazi. Si aliwahi kujiweka kwenye mtandao akijifanya kuongea
slang ya kiJoji Bush kuwa ana njuluku kama hana akili nzuri. Basi, kama anazo
aendeke akatumie hizo asituletee wendawazimu na ulimbukeni hapa.”
Da Sofia Lion aka Kanungaembe anamkonyeza
shoga yake Gau Ngumi Linungaembe na kula mic “mwenzenu hakuna kinachoniudhi
kama kuwadhalilisha akina mama kwenye miziki yao ya mitusi. Kwanini wanawavua nguo
na kuonyesha laana zao utadhani kuna anayezitaka? Akina mama nasi tumezidi. Tunapewe
vijisenti kumi halafu tunauza na kudhalilisha utu wetu na wanawake wote tokana
na ujinga, umaskini na ushankupe.”
Mpemba aliyekuwa akisikiliza kwa makini
anaamua kuchumpa na kula mic “wallahi japo akina mama mpaswa kulaumiwa, mie
nadhani wa kulaumiwa zaidi ni jamii yetu iliyojirahisi na kuwa ya kidaku na
kitwahuti bila sababu. Kwanini ntu acheze nziki uchi halafu ategemee kuungwa
nkono? Yakhe hii yauma na kuumiza haswa jamii nzima inapogeuzwa dodoki la
kubeba kila uchafu na upuuzi eti nayo waita sanaa. Sanaa gani hii zaidi ya
laana?”
Mzee Maneno kama kawaida yake anaamua kuingia
kivinginevyo. Anaramba mic “wenzenu wanajihadaa kuwa huu ndio usasa wakati ni
ushamba na ulimbukeni wa kutupwa. Wengine wanasema huu ndiyo ujana. Kwani nani
hakuwa kijana? Mbona hatukufanya upuuzi kama huu? Nashauri uwepo mkakati wa
kulazimisha vijana wasome kwanza ndiyo wavamie hiyo sanaa baadaye.”
Msomi anamchomekea “mzee Maneno umetoa pwenti
ya msingi. Kama vijana wetu waliogeuzwa watumwa kimaadili kwa kutaka kuukata
wakati unawakata wangekuwa na elimu safi na ya kutosha, wala wasingekubali
kugeuzwa watumwa wa kimaadili. Wangeweza kuwa na nyenzo ya kupima kila jambo na
kufanya mambo ya maana. Kimsingi, sanaa siyo mbaya bali wasanii uchwara
wanaozuzuliwa na ulimbukeni wakisukumwa na njaa na ujinga. Finish.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si kakapita
kanungaembe kakiwa uchi wa mnyama! Gues what. tuliamua kukatia bakora
kakawaambie wapuuzi wenzake.
Chanzo: Tanzania Daima Leo Machi 28, 2018.
No comments:
Post a Comment