Hivi karibuni jamaa moja aitwaye Bashiti au mtoto wa Dingi alichafua hewa kijiweni. Si baada ya kutaka eti baadhi ya wanakijiwe waende kwake kupima DNA kujua kama walivunja amri ya sita na kupanda mbegu kwenye mashamba yasiyokuwa yao?
Mchunguliaji anaingia akiwa amenuna utadhani atapasuka tokana na maudhi aliyo nayo. Baada ya kuamkua hata hachukui gazeti kama kawaida yake. Kwa mara ya kwanza anaanzisha mada “wazee mnasemaje kuhusiana na hizi siasa za kusaka sifa ambako Bashit anaonekana amedhamiria kuumiza familia zetu?”
Kabla ya kuendelea Mgoshi Machungi wa Mashindei anampokonya mic na kuuliza ‘mgoshi unamaanisha nini? Eeza vizui tikueewe ii tikusaidie.”
“Mgoshi unaishia dunia gani ambaye hujui wala kuhangaishwa na sekeseke na sheshe la akina mama kwenda kwa mkuu wa koa kudai warume waliotelekeza vitegemezi vyao washikishwe adabu ili wakome ukware? Eti tunaambiwa tukapime DNA. Je yeye amepima DNA kujua kama vyeti vyake ni feki au halali?” Mchunguliaji anajibu swali kwa swali.
Kabla ya kuendelea, Kanji anakula mic ‘iko ongelea hii balaa ya kuu ya Koa kutaka vatu vote natelekeza tegemezi yao kwenda chukua yote kwake? Sasa iko jua mbovu na mbichi dugu yangu. Kama veve napanda begu kwenye samba ya venyeve sasa nakujikana.”
“Nitamwambia nini mshirika wangu wa bedroom ambaye ameishatikunivisha gauni kama nami nitabainika kuwa nililima kwenye mashamba ya wenyewe au yasiyo na wenyewe lakini yasiyo yangu. Maana siku zote huwa namwambia kuwa nampenda kuliko hata uhai wangu. Kabla ya kuendelea, Mijjinga anauliza. “Hizi kusema ukweli ni si siasa bali mbinu ya jamaa kusaka sifa na kupata kiki. Kwani yeye mambo ya vitegemezi vyetu na washirika zetu wa bedroom wa kando yanamhusu nini? Kwani, yeye ni ustawi wa jamii au kiranga tu?”
Msomi Mkatatamaa anaamua kutia guu na mapema “huyu jamaa, japo anachofanya kina mashiko, anafanya hivyo kwa nguvu ipi kisheria? Je huku siyo kuingilia faragha za watu ukiachia mbali kuvunja sheria na kuingilia kazi na uhuru wa mahakama? Kwanini asiwaachie wahusika wamalize mambo yao hasa ikizingatiwa kuwa kuna taasisi zenye ujuzi na mamlaka kisheria kufanya hivyo ukiachia mbali kuwa wahusika hawakumhushisha walipoamua kula tunda na kuvunja amri ya sita. Kwanini hataki kusoma historia na kujifunza toka kwa Agus Lyatongolwa aliyejiingiza kwenye kashfa na kadhia hii wakati ule akikusanya mtaji wa kugombea urahisi akaishia kushushuka na kukutwa kumbe naye alikuwa mshirika? Nadhani kuna haja ya kuacha kuingilia mamlaka ya taasisi nyingine hata kama wahusika wanakingiwa kifua na dingi.”
“Msomi umenikumbusha na kunifikirisha. Je huyu dogo ana ujuzi gani wa mambo ya ndoa ukiachia mbali yeye kukalia kashfa ya kughushi? Hawa walighushi upendo wao sawa naye alivyoghushi vyeti. Au siyo?” anazoza Mipawa huku akibwia kahawa yake.
“Jamani kaka zangu acheni utani. Mngejua sisi tuliojizalia tu tunavyohangaika hasa kuishi bila matunzo wala msingepinga hatua hii ya ukombozi. Mungu azidi kumsimamia huyu kijana hata kama ana madhambi yake.’ Anachomekea Gau Ngumi aka Jinungembe huku akimwangalia da Sofia Lion aka Kanungaembe. Wanaangua kicheko kuonyesha kuridhika na hatua anazochukua Bashit.
Kapende anaamua kutia guu akionyesha wazi kuchukia “kuingilia ndoa za watu, mambo ya vitandani mwetu hayalihusu lisirikali. Huyu anatafuta kiki tu.Je ameishamaliza tatizo zilizoko chini ya mamlaka yake kisheria. Je anajua mipaka ya mamlaka na kazi yake. Je ameisoma historia ya kadhia kama hii na uingiliaji wa maafisa wa lisirikali? Kama alivyosema Msomi, kwanini jamaa amekuwa mvivu wa kufikiri kiasi cha kusahau yaliyompata Lyatongolwa pale wenye kujua walimwambia wazi kuwa hawana sababu ya kumwamini kwa wake zao.”
Mpemba anakula mic na kusema “Mie siungi nkono wala kulaumu kadhia hii. Hata hiyo tujiulize. Untegemeani iwapo matokeo ya vipimo vya kinasaba DNA yaoneesha kuwa vitegemezi vingi vinavozaliwa kwenye ndoa ni vya baba wa nje tokana na nchepuko? Unategemea nini kaya iniporuhusu mambo ya kipuuzi kama short guest houses ambazo zinajulikana wazi kuwa kazi zake ni kuharibu maadili na kupromoti umalaya?”
“Duh! Ami unaongea utadhani wewe ni mwanasheria!” anachomekea Mbwamwitu.
Mpemba anajibu “wadhani hiyo sharia kuisomea siwezi? Basi mwenzio mie nimesoma fiqh nje na ndani. Hivo, nisemayo si matokeo ya hasira wala husda bali uhalisia wa mambo ati. Je untegema nini kaya inaporuhusu waganga wa kienyeji kutangaza wanavotibu matatizo ya ndoa wakati lengo lao ni kutembea na kuwaibia wateja wao ambao wengi wao ni akina mama? Nadhani kama huyu dogo anataka kueleweka, basi aachane na mambo ya kulazimisha watu wazima wakapime DNA badala yake apambana na chanzo cha janga hili ambalo ni kukosekana uaminifu, uvunjifu wa maadili na utapeli wa kawaida hasa rushwa. Kwani wapo wengi walopewa mimba kwa njia ya kutoa ana kupokea rushua ati.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si likaja kundi la akina mama wakiwa na vitegemezi vilivyotelekezwa na madingi wao! Acha tutoke mkuku kuogopa kuumbuliwa!
No comments:
Post a Comment