Baada ya kuona kila masadukayo wanakuja na nyaraka
kwa wachovu kila wakijisikia na wakidhani mambo yanakwenda ndivyo sivyo, nami
profesa emeritus mtumishi wa Mungu aliye juu ya miungu yote ya kigeni nakuja na
waraka wangu kwa masadukayo. Kama ilivyo haki kwa masadukayo kuja na nyaraka
zao kwa umma, naona ni haki kwangu pia kufanya hivyo. Tofauti na nyaraka za
masadukayo, huu waraka ni tofauti na nyaraka nyingine ambazo wachovu wamezoea.
Kwani, waraka huyu si wangu bali ni maneno ya mwenye dunia mwenyewe ambaye
wengi humtumia kujipatia ulaji na ujiko kirahisi tofauti na mimi ambaye ndiye
kinywa chake pekee kilichobakia. Hivyo, wewe unayeusoma, ujue unaongea na Mungu
moja kwa moja. Hii ni bahati yako na utapata baraka tele kwa kusoma na
kutafakari waraka huu mtakatifu usio na uroho mtakakitu bali roho mtakatifu na
mtukufu. Kama utaupuuzia waraka huu, laana zake mwenyewe mwenye kutisha
zitakuandama hadi utakapokuja kwangu kutubu kabla mengine mengi na zahama
havijakukuta. Mimi si askopo wala mtume wa kujipachika. Wala si mchunaji wala
mchungaji bali msemahovyo lakini kweli tupu unabii niliorithi toka kwa mzee
Waambie mwana wa Wapasha bila woga wala kutafuna maneno.
Kwanza, nitamke wazi wazi. Kaya hii si mali
ya mja yoyote isipokuwa wachovu wote kwa umoja wao. Hivyo, hakuna mwenye
stahiki ya kumburuza wala kumTunduLissu mwenzake.
Kabla ya kumwaga ujumbe wa mwenyewe, naanza
kwa maswali: Je wao wanafanya yale wanayotaka lisirikali lifanye kama vile kuwa
na demokrasia kwa kondoo wao wanaoburuza na kuwachuna kila uchao huku wao
wakiishi maisha ya kutanua wakati wanayedai kumhuribiri alikuwa kapuku wa
kunuka hadi akashindwa hata ndururu ya kumpa Kaisari hadi samaki alipompa taafu?
Je wako tayari lisirikali kuingilia anga zao na
kuwataka wafanye kama lionavyo? Je muda wote walikuwa wapi hasa wakati ule kaya
yetu ilipogeuzwa shamba la bibi na akina Mzee Ruxa, Njaa Kaya na Denjamani
Makapi?
Aliyejuu anaonya kuwa, ukimuelekezea mwenzako
kidole jua vitatu vinakuelekea wewe. Kwa kulijua hili, nachelea kuhukumu wala
kushinikiza ili nisijegeuziwa kibao siku moja.
Kwanini inakuwa rahisi kuona maovu ya wenzao wakati yao wakiyalimbika
kana kwamba wachovu hawaoni wala kujua wanavyotanua kwa zaka na mapato ya
makapuku? Je kwanini leo si zama zile za
utwahuti wa wazi kimfumo na kitaasisi hadi kaya inapata jembe la kuikomboa hata
kama ni kwa kuminya baadhi ya haki jambo ambalo halikubaliki? Wakati wachovu
wakiuzwa na kubinafsishwa kishenzi mbona hawakutoa waraka? Je ni kwanini
hawakutoa waraka baada ya kuibuka tuhuma dhidi ya wenzao wanaotuhumiwa kubaka
na kulawiti ukiachia mbali waliojipatia ukwasi kwa kuwahadaa na kuwaibia
wajinga wetu maskini kwa kuwaahidi miuya wakati miuya yenyewe ni kuwaibia? Nangoja
majibu si majipu tena yanayoingia kichwani.
Tokana na wengi kukwazwa na kuudhiwa na mambo
ambavyo yanakwenda ndiyo siyo, nawashauri, ili waeleke wako upande gani, basi
waanzishe chama cha siasa lau tuwajue kuwa ni wanasiasa. Usawa huu ni wa uwazi
wa kweli na ukweli wa ukweli unaomtaka kila mmoja wetu asimame hadharani na
kuonyesha upande anaolalia. Kwani, haiwezekani kutumikia mabwana wawili yaani
aliyeko juu na hawa walioko chini. Lazima mhusika aamue kufanya maamuzi magumu.
Kwani si vizuri kutumia majukwaa ya kiroho kufanya mambo ya kisiasa wala
kutumia majukwaa ya kisiasa kufanya mambo ya kiroho. Huu ni uroho tena
uliopindukia. Kwani Bwana mkubwa mwana wa Maria alisema kuwa kabla hujatoa
boriti jichoni mwangu, ni vizuri kutoa kibanzi kilichoko jichoni mwako au siyo?
Nilimsikia mmoja akisema kuwa wao kufanya
siasa kumekuwapo tangu yapata miaka 2,000. Je siasa hazikuwapo pia? Kama anataka
kujua ni namna gani zilikuwepo siasa kabla ya hata roho mtakakitu, ajiulize
akina Farao kule Masri walikuwa wakifanya nini? Si walikuwapo kabla ya hao
wanaojifanya wana kila sababu ya kupiga kelele?
Nikigeuka upande wa pili, jamani, tufike
mahali tuache kuburuzana, kutishana wala kunyotoana roho ukiachia mbali
kusakiziana kesi feki. Huku nako ni
kughshi haki sawa na wale wanaoghushi sifa za kitaaluma na kiroho kama
masadukayo wa kujipachika hadi wengine wanapayuka kuwa wana mchele kuliko
lisirikali. Anayedhani amesimama achunge asianguke. Mamlaka na ulaji ni kama
maua kwenye shamba. Huwa na msimu wake na ukiisha hunyauka. Nani mara hii
kamsahau Tunituni Makapi aliyefanya kila makufuru na kuwaita wachovu kuwa wana
uvivu wa kufikiri wakati yeye alikuwa ndiye mwalimu na kiongozi wao katika
uvivu huu uliogeuza kaya shamba la bibi huku bibi mkubwa akimtumia bwana mkubwa
kupiga njuluku. Wako wapi kwa sasa zaidi ya kutegemea hisani tena ya vijana
wadogo?
Ndugu zanguni, nimalizie kwa kuwaasa muwe na
busara katika mapito yenu. Kwani kila lenye mwanzo huwa na mwisho. Na wote
tuliopo chini ya jua si chochote wala lolote bali wasafiri waendako
wasikokujua. Mamlaka, nguvu na utajiri vina thamani gani iwapo tufapo kila mtu
huondoka na shuka moja? Mwenye akili na azingatie unabii huu kwa wote.
Chanzo: Tanzania Daima leo Jumatano, April4, 2018.
No comments:
Post a Comment