How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 24 April 2018

Kijiwe kutembelea Brazil na Korea ya Kusini

O dia que marca a derrocada de 3 ex-líderes mundiais: Lula ...

            Leo hii kijiwe kinakuja na mada ambayo ni mama au baba wa mada. Kwani, kinazama kwa kina na kuangalia namna ya kuleta uwajibikaji kayani hasa kwa madingi wa zamani waliopunyua njuluku za kaya wao, washirika zao wa bedroom ukiachia mbali vitegemezi na maswahiba na waramba viatu wao. Tumeamua kufanya mapinduzi ili kuepuka kuendelea kusota wakati wao wakitanua na kutucheka kana kwamba hawakutuibia ukiachia mbali kuwa ukwasi wanaotanulia ni jasho letu.
Msomi Mkatatamaa ndiye analianzisha ‘jamani mmesoma habari za madingi wa Brazilini na Kuria ya Kusini kupigwa mvua lupango?”
Kabla ya kuendelea Mgoshi Machungi mwana wa Mashindei anajibu “mimi na bi mkubwa tiizisoma tikiwa tinatokea Mashindei kumjulia hali bwana mdogo Shemtwashua wa Shemkaa na kufurahi tikitamani na hii ingefanyika hapa kayani.”
Msomi Mkatatamaa anaendelea “ukiangalia kaya zote zilizoamua kufanya kweli, zimeendelea au zinaendelea tofauti ya yetu inayoendelea katika kutoendelea tokana na kuendekezana na kulindana kama inavyoendelea. Inakera kuona wanene wanakwiba na kulindana huku wakituimiza tuchape kazi waibe na kuneemeka wakati sisi tukiteseka. Inatupasa kufanya mapinduzi ya kifikra kuhakikisha haki kwa wezi wawe wakubwa inatendeka badala ya kuwaabudia mibaka huku tukiwachoma moto mibaka.”
Mpemba anaamua kula mic “mie wallahi naona tufanya npango twende kwenye hizi kaya kujifunza lau tuje tulianzishe au siyo? Maana, kulindana kunzidi hapa kayani tunikoambwa tusiwaguse wateule wasioguswa wakati sie twaumizwa madhambi walotenda. Natamani kunfanyia kitu mbaya audhillahi minaashaitwan rajiim yule wezi wakuu. Wallahi ingekuwa uchaguzi wangu ningewatumia popobawa lau awapopoe kidogow lau waonje uchungu wa dhulma.”
Mipawa anampoka mic Mpemba na kuronga, “lazima kwenda kujifunza namna wanavyowazawadia madingi wao waliojizawadia maulaji kwa kuyatumia vibaya wasijue yangewatokea puani kama ilivyotokea kwa brother Lula na da Park wakati tukingojea ya Jake Zuma kule Sauzi.”
“Nakubaliana nawe asilimia elfu moja. Lazima twende wote hata kama ni kwa kuuza mashamba yetu hata washirika zetu au vipi?” Kabla ya kuendelea Mgoshi anadakia “Unashemaje? Eti tiuze washiika wetu wa bedium? Kauze wewe mie nimnunue tena kwa kasha sasa hivi,” anajibu Mijjinga huku akimpa kipisi cha sigara kali mzee Maneno ambaye anakupua mioshi kama sita hivi na kula mic “hakuna haja ya kuuza mashamba wala washirika zetu kama jamaa zetu wa kaya jirani wanaowaazima washirika zao kwa watalii ili kupata njuluku ya aibu.  Tuombe njuluku toka kwa lisirikali linalosema linapambana na ufisadi kama kweli siyo longolongo hakuna shaka litatukatia chochote kitu ili kulitea ujuzi tutakaotumia hapa kayani kuwasulubu akina Tunituni, Njaa Kaya na wengine ambao tunao maya.”
Kanji anakula mic ‘mie iko unga kono na guu vazo ya juluku toka kwa salkarini. Kwani, kila siku iko sikia kuwa iko na juluku tosa sana. Kama nayo napambana na fisadi tatupa sisi juluku twende tembea kwa kaya zile haraka sana dugu yangu. Mimi iko penda kwenda Kuria na kupitia Bombey kuona bibi yangu na toto.”
Gau Ngumi aka Jinungaembea anakula mic “yote pangeni. Lazima niwemo kwenye huu msafara lau nami nikatanua kama wao walivyokuwa wakitanua wengine wakishindana na Vasco da Gama. Hapa lazima nikapige shopping kali kama mshirika wa bedroom wa Jongwe kule Zimba za Mabwe aliyetesa hadi akaitwa Gucci.”
Kabla ya kuendelea Mbwamwitu anamchomekea “da Gau huwezi kwenda kwa sasa. Maana sisi tutakaokwenda bila washirika zetu wa bedroom tunaweza kuambiwa tukapime DNA baadaye kuonyesha kama tulionja tundi au la.”
Kabla ya kuendelea Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua naye kuchomekea “sasa umeanza. Kama ukila tunda kosa liko wapi ilmradi isiote mbegu?  Unaogopa kupima DNA au bi mkubwa kukuvisha gagulo?  Mie nakwenda kule kuchapa mzigo wa uchunguzi wa kisayansi wa kuondokana na ujambazimbuzi wa wanene wetu hasa wa zama zile waliojigeuza miungu wakaishia kulindwa kama vichanga. Tumeelewana kaka yangu; wala huna haja ya kuogopa kuandamana nasi.”
Wakati akitaka kuendelea, Kapende anakula mic na kusema “da Sofi acha nkuchomekee kidogo. Mie sina ugomvi na kwenda na yeyote ilmradi katika nsafara huu mie napanga kuwa kwenye ule kwa kwenda Kuria Kusini japo niende kule nikafaidi hisani na ukarimu wa wakuria hawa weupe. Nasikia vimwana vyao vinawazimikia sana waswahili kwa vile hawana makuu wala kuendekeza vitu kama warume wao.”
Mzee Maneno anaamua naye kutia guu “jamani, badala ya kushughulikia mikakati ya namna tutakavyokwenda kupata darasa la uwajibishaji mhangaishwa na mambo ya bedroom. Hayo sisi hayatuhusu. Hata lisirikali halipaswi kujihangaisha nayo kwa vile ni mambo nyeti sana yanayotaka umakini kama alivyosema profesa fulani. Hivyo, nashauri, tugawane sehemu za kwenda. Inabidi tujue watakaokwenda Brazil na watakaokwenda Kuria ya Kusini na mapema au siyo?”
Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shumbwengu la dingi wa zamani akitokea kwenye matanuzi yake. Acha tumzomee kwa uvivu wake wa kuthink hadi akajipa maulaji na kutuibia hadi kuishi kwa kulindwa kama kichanga.
Chanzo: Tanzania Daima, Aprili 24, 2018.

No comments: