Heko Rais Magufuli

Wednesday, 11 April 2018

Kijiwe chataka viongozi wa kiroho wakujipachika washughulikiwe


            Hakuna ubishi kuwa kujipachika madaraka ya kiroho imegeuka fasheni kwa baadhi ya matapeli kupiga njuluku toka kwa wachovu wajinga na waliokata tamaa. Leo kijiwe kinadurusu jinai hii na kutoa mapendekezo yake kwa lisirikali linalosifika kuwashughulikia vihiyo walioghushi japo baadhi yao wanafumbiwa jicho kama vile Bashite.
Mijjinga ndiye analianzisha “tangu aingie kwenye ulaji, rais JeiPieM amegeuka mwiba kwa mafisi, mafwisadi na vihio hata watoro makazini na walioghushi vyeti vya kitaaluma. Kwanza nimpongeze. Hata hivyo, nashauri awatumbue viongozi wa kiroho wenye uroho waliojipachika vyeo vikubwa vikubwa wakati hawana lolote zaidi ya kuwaibia wachovu.”
Mpemba anakula mic “hata mie hili nliunga nkono kwa vile nao ni watumishi wa umma sawa na wengine. Haiwezekani tushughulikie vihiyo wa sirikalini na kuwaacha wa mazabahuni. Huku wallahi mie ona kama kujipiga ntama.”
Kabla ya kuendelea Kapende anapunyua mic “usemayo Ami ni ya kweli. Nadhani hapa tutahitaji definition ya umma ili kuwapata hawa wapiga njuluku kwa kisingizo cha roho mtakatifu wakati wamejaa roho mtakakitu.”
“Hapa mmegusa kwenyewe. Kwani, huwa najiuliza: Kwanini kuwashughulikia watumishi wa sirikali kwa vile wako kwenye ofisi za umma na kuwaacha viongozi wa kujipachika wa dini wakitumikia umma ule ule? Je ni umma gani wenye kuleta maana hapa kama siyo umma wa watanzania wote bila kujali anayewatumikia ni mtumishi wa serikali, shirika binafsi au taasisi ya dini?” anahoji Msomi Mkatatamaa.
Kabla ya kuendelea, Mipawa anakamata mic “kwa vile lengo la Mkuu ni kujenga mfumo wajibifu wenye kujali na kushika maadili, namshauri apanue wigo kwa kuwahusisha viongozi wa umma wawe wa sirikali au taasisi za dini na taasisi nyingine zisizo za kiserikali. Hii ni kwa sababu wote wanawatumikia, na wengine kuutumia, umma huu wa wanyonge wanaopaswa kulindwa haki zao.”
Kanji hajivungi; anakula mic na kusema “kama iko taka maadili napasa kukama vote napachika yeye cheo kuba kuba ya roho. Vatu vote ya nchi hii iko sava. Hiwo, mimi taka sugulikia vote bila angalia nyani usoni. Iko vatu nanyonya vatu ingine nasingizia Mungu.”
Msomi anakula mic “maadili linapaswa kuwa agenda ya kaya na si ya kisirikali. Kwani, wachovu wote wanapaswa kuwa na kufaidi maadili kama jamii ya watu iliyoanza kujitambua na kuondokana na jinai ya mtu kumnyonya mwingine. Kwa sasa, tunao viongozi wengi wa kiroho tena wa kujipachika waliotokea kuwa matajiri kwa sababu tu wana mwanya wa kutumia vyeo vyao vya bandia kuwaibia watanzania wengi wajinga na waliokata tamaa kwa kuwaahidi pepo na miujiza vyote vya uongo.”
Kabla ya Msomi kuendelea Gau Ngumi Jinungaembe anasema, “kaka acha nikuchomekee.” Kabla ya kuendelea naye anakatizwa na Mbwamwitu anayesema kwa utani “unamfanya nini! haya dada mchomekee mradi msisababishe ajali kama mabasi ya City son.”
Jinungaembe anampuuzia na kuendelea “mwenzenu nashangaa namna wanavyoendekezwa waendekeze ulaji wa dezo kwa jina la roho mtakakitu. Je maadili yanapaswa kuwa ya watumishi wa sirikali tu au wanakaya wote? Je kuendelea kuwaandama watumishi wa umma walioko kwenye ofisi za sirikali na kuwaacha viongozi wa kidini wanaotumia nafasi zao kujitajirisha kinyume cha sheria na hata taratibu na kanuni za madhehebu yao siyo upendeleo wa wazi ambao ni kinyume cha sheria na tararibu za kaya ambazo zinasema wazi kuwa watanzania wote ni sawa na wanapaswa kutenda na kutendewa kwa usawa?”
“Du unauiza mashwai kama jaji au loya! Naona umigusa mashwai yangu kaibu yote. Ngoja nikuongezee shwai jingine. Je viongozi wa kiroho waiojipachika vyeo vya kiroho si sawa na wae waiojipachika sifa za kiaaluma wasizo kuwa nazo? Kwanini iwe jinai kwa mtu kujipachika uaimu, udaktai, ukaani na mengine mengi akini isiwe hivyo kwa anayejipachika cheo cha kiroho? Tinajua namna maaskofu, mashehe na wachungaji wanavyopatikana. Hivyo, hapa hakuna utata juu ya kuwatambua wote waiojipachika vyeo hivi na vinginevyo kama vile utume, unabii na vingine vingi wakati ni uongo mtupu.” Anaronga Mgoshi Machungi wa Shekiango mwana wa Mashindei.
Mzee Maneno aliyekuwa kimya anaamua kutia timu “kumekuwa na mkazo kwenye watumishi wa sirikali kutangaza mali zao. Je kwanini viongozi wa kiroho ambao nao wanashughulika na umma wanaachwa nje wakati, kwa sasa, ndiyo wanaoongoza kuwa na ukwasi usio na malezo yanayoeleweka? Je tunangoja mpaka waishambulie serikali ndiyo tuwawajibishe kama ilivyotokea kwa mmoja aliyejidai kuwa ana fedha kuliko serikali wakati fedha yenyewe ni ya kuwaibia watu mafukara na wajinga waliokata tamaa.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shangingi la kiongozi mmoja wa kiroho aliyejaa uroho na roho mtakakitu. Acha tumzomee na kutaka kumnasa na kumfanyia kitu mbaya. Leo da Sofia Lion Kanungaembe hakuudhuria. Kwani yu auguliwa na mjomba wake aliyehamishwa bondeni Jangwani.
Chanzo: Tanzania Daima Machi 11, 2018.


No comments: