The Chant of Savant

Sunday 1 November 2020

KISA CHA KABWE, MEMBE NA MAMANTILIE



Wanaojua historia ya Zitto Kabwe (Kiongozi wa ACT-Wazalendo) na mgombea urais wake kisiasa na siasa za kisasa na kisasi, Bernard Membe, hata tabia zao, hawashangai maneno ya hivi karibuni ya Zitto kuwa atampigia kura mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu na kumtosa Membe. Kimsingi, Kabwe ameonyesha kile ambacho waingereza huita verisimilitude; picha ya kweli na halisi. Hii imenikumbusha kisa cha rafiki yangu. Alikwenda kwa mamantilie kupata mlo. Akiwa anangoja mlo, alisikia mantilie akimtuma msaidizi wake kwenda kumnunulia chakula hotelini. Jamaa alistuka kunani; akaamua kuondoka bila kuaga wala kungoja chakula. Maana yake nini? Mamanitilie alijua madawa machafu na sumu alivyokuwa akitumia kuvutia biashara. Katika sakata hili kadhalika, kwa wanaojua ajenda binafsi na ithibati ya wahusika yaani ulaji, hawatashangaa wala kushuku maneno na msimamo aliouchukua Zitto. Ajabu ya maajabu hata Maalim Seif Shariff Hamad (Mwenyekiti wa chama) ameamua kuukoleza kwa kukuza mgawanyiko akimuunga mkono mwenyeji wake asijue nani atafuata! Je kinachojifunua hapa ni nini, mwisho wa mwanzo wa ndoa ya Kabwe na Membe umeanza au ndo siasa? Je nani anatamchuuza mwenzake? Who’s hoodwinking whom? Waingereza huuliza. Kwa uzoefu wa uharibifu, Kabwe ana kila sababu ya kuchekelea. Hata hivyo, itategemea. Baada ya kuvurunda CCM–––asijue aishie kwa upanga hufa kwa upanga–––Membe awezavurunda hata huko ugenini na mwishowe akarejea “nyumbani.”
        Membe hatakuwa wa kwanza wala mwisho.  Sawa naye, aliponyimwa nafasi ya kugombea urais, waziri mkuu wa zamani aliyeachia ngazi baada ya kukumbwa na kashfa ya ubadhilifu, Edward Lowassa, aliamua kujitoa kwenye chama kilichomzaa na kumlea, CCM na kuhamia upinzani alikojiunga na CHADEMA kilichomteua kugombea urais akaangukia pua.  Kilichofuatia kinafahamika ingawa si vibaya kugusia ni kwanini Lowassa alihamia upinzani na kugombea urais. Hakuwa na la kupoteza bali lau ima kuukwaa urais au kulipiza kisasi kwa upinzani uliokuwa umeanzisha sakata lililomchafua na kummaliza kisiasa.
        Kimsingi, Membe, amerudufu alichokifanya hasidi wake yaani Lowassa. Hana cha kupoteza kwenye upinzani. Baada ya kunyimwa kugombea urais nyumbani, japo hakwenda moja kwa moja upinzani. Alidhani angeweza kulipiza kisasi na kufikia malengo yake akiwa ndani. Yake ilikuwa: “Tutabanana humu humu.” Haikuwezekana wala hakufanikiwa. Kwa kiasi kikubwa, Lowassa alifanikiwa kuiadhibu CCM na hata upinzani kwa kupata kura nyingi na kupata turufu ya kurejerea nyumbani. Tofauti na kipindi hiki, Membe na mwenzake Tundu Lissu wanaotaka kulipiza kisasi, hawataweza kuiadhibu wala kuiumbua CCM kwa sababu, Lowassa alipata fursa tokana na upya wa rais John Magufuli na uchakavu wa CCM ambayo kwa sasa imefufuliwa tokana na utendaji wa hali ya juu wa Magufuli. Hivyo, ni vigumu kwa Lissu na Membe kufikia malengo yao. CCM inategemea sana mafanikio ya Magufuli. Hivyo basi, wanachofanya wawili hawa, japo ni haki yao ya kidemokrasia, mipango yao itakuwa vigumu kufanikiwa. Sitaki niwahukumu japo wanahukumika kirahisi, uwezekano wa kufikia na kufanya alichofanya Lowassa ni haba.
        Kwa upande wa Zanzibar, hali itakuwa hivyo hivyo kwa maalimu Seif Sharif Hamad. Anatumia mikakati na hoja zile zile zilizomfanya ashindwe kwenye chaguzi alizowahi kushiriki. Kwanini wasikengeuke kujiuliza ni kwanini Kabwe au Freeman Mbowe wametema nafasi hii yenye ujiko na marupurupu kibao? Kwa kujua kushinda ni bahati nasibu, wenye vyama wameamua kugombea ubunge badala ya urais. Isitoshe, wanajua: wagombea wao wakishindwa hawatakuwa na uwezo wa kutishia madaraka yao kichama; kwa vile hawatakuwa na jipya la kuonyesha zaidi ya kushindwa. Kwa mfano, kwa kujua ACT-Wazalendo hakina bao visiwani, Kabwe ameamua kumwachia Seif, ambaye umri umemuacha agombee na kujifurahisha lau kutafuta sababu ya kuwa na mantiki kisiasa kwa kuanzisha malalamiko baada ya kubwagwa ili lau aendelee kuwa na ushawishi, kwa maslahi binafsi kisiasa na kimkakati.  Ukisilikiza kwa makini hotuba ya Membe ya kushukuru kuteuliwa na anavyosema, lazima Kabwe awe bungeni na siyo kwenye serikali, basi unapata jibu haraka.
        Hata ukisikiliza maneno ya Lissu kuhusiana na Zanzibar, unaona wazi kinachotegemewa. Anajua fika. Hamad anagombea kwa mara ya sita. Nini  kipya anacho au atafanya mara hii kilichomshinda mara tano zilizopita?  Ukiaongeza na ukweli kuwa king’ang’anizi mwingine Prof Ibrahim Lipumba atakuwa kwenye debe, hali inakuwa wazi kabisa. Sambamba, Lipumba naye hana jipya la kuwaambia wala kuwapa na kuwashawishi wapiga kura. Lowassa aliweza kupata kura nyingi tokana na upinzani kuungana. Je hali itakuwaje baada ya upinzani kusambaratika na kila chama kuweka mtu wake zaidi ya kutaka kulipiza visasi na ung’ang’anizi? Ama kweli, uchaguzi wa mwaka huu ni sawa na kisa cha mamantilie.  
        Kama ilivyokuwa kwa Lowassa na Sumaye, Membe atajiondoa baada ya wahusika kumtumia.
Hata Seif, akishindwa kutwaa urais Zanzibar, ima amnyang’anye Kabwe chama kama alivyomfanyia James Mapalala naye akafanyiwa na Lipumba au naye atupwe kama atakavyofanyiwa Membe sawa na Lowassa na Sumaye. Kama utabiri wetu utakamilika na wahusika kugeukana na kutumiana, ndizo siasa za kisasa na kisasi . Habari ndiyo hiyo.
Chanzo: Nipashe Jumapili leo.

No comments: