The Chant of Savant

Saturday 21 November 2020

BUNGE LETU TUKUFU LISIGEUZWE KIJIWE CHA MATUSI

Akifungua bunge la 12, rais John Pombe Magufuli alisema kuwa angependa kukosolewa kwa hoja na kutoa suluhu, yaani ukosoaji chanya na wa kujenga (constructive criticism). Kwa msingi huo, safu hii itaitikia wito wa rais kwa kutoa ukosoaji chanya kuhusiana na kituko kilichoshuhudiwa bungeni hivi karibuni kwenye ufunguzi wa bunge tajwa ambacho si rahisi kuvumilia kuogopa kuweka mfano (precendent) mbaya.  Katika muda huu tajwa, mbunge mmoja mpya ambaye safu hii inamheshimu na kumhusudu sana ambaye, hata hivyo, zama za utawala wa awamu ya kwanza na pili asingeweza kufanya siasa tokana na kutochanganya dini na siasa.                Mbunge huyu aliwaacha wengi vinywa wazi. Kwani, mhusika–––pamoja na uanagezi wake–––alipewa fursa ya kuongea kwa niaba ya wabunge wakati ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuongea bungeni. Hapa nadhani ndipo kosa lilianzia. Unampaje nafasi mwanagezi kuongea wakati kuna wakongwe ambao wameyazoea mawimbi kama haya?  Mbunge huyu ambaye ni mara yake ya kwanza kuingia bungeni, bila woga wala tahadhari, alitamka matusi tena mbele ya rais huku akishangiliwa kwa mshangao wa wengi wakati mhusika akizidi kukoleza matusi yake. Katika fursa hii ya kuongea bungeni, mhusika–––bila kuzingatia kuwa kila kinachoongelewa kinatunzwa–––alimkariri waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, Sir Winston Churchill, akisema kuwa kama unakwenda mahali na njiani mbwa wakawa wanakubwekea, ukiamua kumtupia au kuwatupia mawe kila mbwa wanaobweka, hutafika. 
        Pia Churchill aliwahi kusema kuwa ni jambo jema mtu asiye msomi kusoma vitabu vya nukuu. Hapa muhimu ni kuzitumia vizuri. Je kwa kuwashambulia wahusika kwa kuwalinganisha binadamu na mbwa siyo kuanza kuwatupia mawe hao mbwa husika? Mbunge huyu mwanagezi alimaanisha wapinzani wanaolalamikia matokeo ya uchaguzi ambayo ni haki yao ilmradi madai yao yawe na mashiko.
Watanzania ni ndugu na tunaheshimiana tukishindana kwa hoja na si mapanga. Hakuna haja ya bunge letu kugeuzwa kijiwe cha uhuni na matusi. Hakuna mtanzania anayeweza kulinganishwa na mbwa hata awe hakubaliani nasi. Unapowaita wapinzani mbwa unakaribisha yafuatayo:
        Mosi, unawapa fursa wakujibu kwa kukutakana wewe na hata taasisi matusi mengi mazito bila sababu. Kwanini kulinganisha watanzania na mbwa wakati–––kama ni misemo ya busara ya kukaripia kadhia hii–––ipo tena mingi? Mfano, msemaji angesema kuwa kelele za mpangaji hazimnyimi usingizi mwenye nyumba. Tuwe na bunge la kistaarabu kama ambavyo ilikuwa kwenye kampeni; na si la matusi na visasi.
        Pili, kuwaita wapinzani mbwa maana yake ni kuwaita watanzania wote mbwa. Kwani, wapinzani nao ni watanzania sawa na watanzania wengine. Wanaweza kukosa, kukosea na mengine kama hayo. Lakini bado hakuna mwenye haki ya kuwaita au kuwalinganisha na mbwa. Hivi nao wakiamua kukuita wewe na wenzio mbwa utafurahi na kuvumilia? Usiishi kwenye nyumba ya vioo ukawatukana watupa mawe.
        Tatu, kwa kuwaita wapinzani mbwa, msemaji alipaswa ajue anamaanisha kuwa walishindana na kuwadhinda mbwa jambo ambalo haliingii akilini. Kwani, mbwa hawezi kushindana na binadamu bali mbwa wenzake. Kuna usemi maarufu kuwa jogoo aliwafundisha vifaranga kunya ndani. Hakuna haja ya watu walioshinda tena kwa kitsunami kuruhusu watu wachache wasiojua taratibu kuanza kupotezea heshima na utu kama jamii ya watu na taifa.
        Nne, kutolea matusi bungeni ni kuliondolea heshima na utukufu wake kama linavyoitwa siku zote. Bunge tukufu haliwezi kuruhusu matusi iwe kwa makusudi au bahati mbaya. Hivyo, ni vizuri wakubwa wa taasisi hii muhimu wakawaonya wanagezi wasiojua lugha za kutumia kwenye chombo muhimu kama hiki. Isitoshe, mbunge anayewawakilisha kweli wananchi, hajatumwa kutukana wenzake. Isitoshe, sijui kama kuna chama chenye sera ya matusi ya nguoni kama haya.
        Tano, watu wazima wanapotukana, tena matusi ya nguoni kama haya hadharani, wanatoa picha mbaya na somo baya kwa watoto na vijana wetu.  Watu wa namna hii wanaoshindwa kuona madhara ya maneno na matendo yao, hawalisaidii taifa wala hawawatendei haki wale wanaowawakilisha ima hawajui wajibu wao na ukubwa wa jukumu la uwakilishaji wananchi.
Je–––baada ya haya kufanyika na ushahidi kutamalaki kwenye vyombo mbali mbali vya Habari–––nini kifanyike? Tunashauri yafuatayo:
Mosi, kuna haya ya bunge kutoa waraka maalum kwa wabunge–––hasa wale wageni bungeni–––juu ya lugha na mienendo inayotakiwa bungeni.
        Pili, inapotokea mbunge kama huyu akapotoka na kuropa, basi spika au mkuu yeyote wa chombo husika amkaripia au kumpa adhabu mhusika papo hapo au baada ya kupata taarifa au malalamiko bila kujali yanatoka kwa nani. Katiba ya Tanzania iko wazi juu ya hadhi na nafasi ya binadamu kuwa wote tupo sawa mbele ya katiba na sheria.
        Hivyo, yeyote anayedhamiria kutukana, kwanza ajiulize yeye ni nani na anayemtukana ni nani? Wajibu wa kulinda heshima ya watanzania na taifa ni wa kila mtanzania.  Kwani katiba yetu iko wazi kuwa binadamu wote ni sawa na kila mtu anastahili heshima na ulinzi toka katika jamii.
        Tumalizie tulipoanzia. Si busara wala akili kuwatukana watanzania kwa kuwalinganisha na mbwa–––mnyama anayedharauliwa kuliko wote katika karibu mila zote za kiafrika. Si vizuri. Kama rais alivyosema, tupingane kwa hoja chanya na si matusi ambayo yanaweza kusababisha vurugu. Hakuna haja ya kukaribisha vituko kwenye bunge, taasisi ambayo si tukufu tu bali ni muhimu kama mmojawapo wa mhimili wa taifa. Tuonane wiki ijayo.
Chanzo: Nipashe Jumapili kesho.

No comments: