The Chant of Savant

Saturday 14 November 2020

Kila Mmoja Sasa ni Ndugu Yake Kamala Harris Makamu wa Rais Mteule Marekani!

Wataalamu wengi wa masuala ya kisaikolojia na kijamii wanakubaliana kuwa binadamu wana hulka ya kutaka kujinasibisha na kile kilicho bora; na si vinginevyo. Jiulize ni watu wangapi wenye ndugu zao majambazi, dhulumat, wezi nakadhalika wanaotaka kunasibishwa nao. Hakuna. Hivi karibuni, wanaojua mahusiano ya wahindi na waswahili, watakuwa walishangaa kuona picha mbali mbali toka India ambako waswahili huitwa kalu au nyani wakisherehekea ushindi wa binti wa kimarekeni mwenye asili ya Jamaica, Kamala Harris alipoibuka kuwa mwanamke wa kwanza mmarekani na mwafrika kuteuliwa makamu wa rais wa taifa kubwa la Marekani baada ya rais Mteule Joe Biden kumbwaga rais mbaguzi anayeondoka Donald Trump. Siyo India tu bali bara zima la Asia wakiwamo wachina ambao juzi juzi waliwabagua waswahili eti wana Covid-19 wakati ilianzia huko Wuhan China. Rejea waswahili waitwao Jarawa kwenye kisiwa cha Andaman wanavyotumika kama kivutio cha utalii ambapo wahindi huenda kuwatazama kama waswahili wafanyavyo kwa manyani ya mbuga ya Gombe kule Kigoma.  Ajabu wachina walivyoshukiwa kuwa na Covid-19 hapa Amerika ya Kaskazini walilalamika sana wakati wakiwafanyia vibaya zaidi waswahili huko kwao.
            Kwa waswahili wa Dar Es Salaam na Afrika Mashariki watakuwa wameshangaa ubora wa ghafla wa Kamala. Mama huyu mwenye umri wa miaka 56 ni mtoto wa Daktari Donald Jasper Harris Mjamaica na mama wa kihindi marehemu Daktari Shaymala Gopalan. Kwa vile urathi wa mtoto hufuata kiumeni, Harris ni mswahili. Pamoja na kuwa na asili ya kihindi, ni vigumu kumnasibisha na India kiasi cha kuamsha hamasa na mapenzi makubwa kwa watu wanaoishi kwenye na kushikilia mfumo wa kibaguzi (caste) ambapo kuoa au kuolewa na mswahili au mtu wa tabaka jingine ni kitu kisichokubalika wala kuwezekana na nuksi kwa familia ya mhusika na jamii kwa ujumla. Sina haja ya kuleta hisia za kibaguzi bali kusema ukweli japo–––kama jamii na watu–––tujifunze kuwa wakweli kwa nafsi zetu.
            Kama Kamala, mswahili mwenye asili ya Jamaica angegombea hata ujumbe wa nyumba kumi nchini India hata katika baadhiya nchi za kiAfrika, angeambulia patupu. Pamoja na ubabe wao, hapa wamarekani wanatufundisha somo la usawa ambalo limezishinda nchi nyingi hasa za Afrika na Asia. Sijui kama kuna mswahili au mtu yeyote mwenye asili ya Afrika mwenye cheo chochote katika bara la Asia hata kiwe kidogo namna gani.
            Niliwahi kusema kuwa kama rais wa zamani wa Marekani mwafrika Barack Obama mswahili mKenya, angekulia Afrika, asingekuwa rais hata wa nchi ndogo yoyote tokana na ubaguzi wa kisheria utakao mgombeaji wadhifa huu awe amezaliwa na wazazi raia waliozaliwa katika nchi husika. Sambamba, sidhani kama Kamala angeweza kuchaguliwa kuwa rais wa Jamaica au–––kama nilivyodokeza hapo juu–––taifa lolote la Afrika au Asia. Hii inaonyesha namna tulivyo wabaguzi kuliko hata hawa wamerekani tunaowatuhumu ubaguzi na ukandamizaji japo hii haiondoi kadhia hii kwao na kwetu. Jiulize kwa mfano, mataifa mengi ya Afrika yanakataa uraia pacha wakati mataifa tajiri ya Magharibi hayana pingamizi hili tena kwa watu maskini toka Afrika na Asia. Pingamizi hili linatupa taabu waswahili tuliko huku. Kwani, hushindwa kufaidi  baadhi ya fursa kama masomo na nyingine kwa kuogopa kukana uraia wetu kitu ambacho ni kikwazo nyumbani na hapa ughaibuni. Mfano, mswahili ambaye hana uraia wa Kanada ukijiunga na chuo chochote unalipia mara tatu. Kuepuka hili, inakupasa ukae Kanada kwa miaka ili upate ukazi wa kudumu angalau uweze kupunguza makali ya huduma kama hizi ambazo ni nafuu kwa wananchi na kidogo kwa wakazi.
            Ukiangalia ni kwanini taifa la Marekani limeendelea, utagundua kuwa tabia yake ya kumkubali mtu kama alivyo, hasa inapokuja kwenye mchango wake kwa taifa, ndiyo imekuwa chachu yake kubwa ya maendeleo ambayo hivi karibuni ilikuwa imedumazwa na Trump ambaye alikuwa na mtazamo wa kuangalia ndani na nyuma bila kuangalia mbele (backward and inward looking). Tokana na udhaifu huu, wamarekani, hasa chama cha Democrat, kiliamua kuutumia na kumuangusha.
            Kwa sasa Afrika na Jamaica zinajivuna kuwa na binti yao kwenye Jumba Jeupe (White House) akiwa ameweka historia katika taifa hili ndani ya muda mfupi baada ya mwingine kukaa pale akiwa ndiye bosi. Asia nayo, inataka kipande cha keki cha ufanisi huu wa kinadharia ambao kivitendo, hauna lolote la kuisadia Afrika wala Asia ikizingatiwa kuwa sera za Marekani huendeshwa kitaasisi na si kwa kutegemea ni nani aliyeko ikulu japo mwenye kuwepo anaweza kuvuruga mambo kwa kiasi kikubwa kama ilivyotokea kwa Trump.
        Tumalizie tuliopanzia. Umefika wakati wa Afrika kujifunza kutoka kwa waliotutawala linapokuja suala la uwezo wa mtu binafsi. Tuwapokee wote wenye asili yetu kama wanavyopokelewa ughaibuni ili waweze kuchangia kwa bara letu pendwa. Laiti mgombea yoyote wa urais wa Afrika au Asia angeambiwa amteue mgombea mwenza kama Kamala Harris, licha ya kuchekwa na kuzuiliwa, angeonekana kama hamnazo; kwa vile sheria na mazoea ya huko hayaruhusu. Ama kweli jiwe la pembeni walilokataa waashi limekuwa bora! Ndiyo maana bara lenye kusifika kwa kubagua waswahili kama Asia sasa linajivunia binti wa kiAfrika kuwa makamu wa rais wa Marekani. Tuonane wiki ijayo.
Chanzo: Nipashe Jumapili kesho.

No comments: