The Chant of Savant

Tuesday 10 November 2020

JE NI KWELI TATIZO NA SABABU YA LISSU KUKIMBIA NCHI NI TISHIO LA USALAMA AU ZAIDI?

 Kitendo cha makamu mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), aliyekuwa mgombea urais katika uchaguzi uliokwisha hivi karibuni Tundu Lissu kupanda ndege na kuelekea Ubelgiji kinazua maswali mengi kuliko majibu. Je ni kweli maisha yake yako hatarini? Kwanini iwe ni baada ya uchaguzi? Kama serikali haikumhakikisha usalama siku aliyorejea toka ughaibuni, ilikuwaje akawa salama kwenye kampeni ambazo zilikuwa zikimpeleka sehemu mbalimbali tena zisizo na usalama wa uhakika nchini? Je kweli tatizo ni tishio la usalama wake au ni zaidi? Je alikuwa ametumwa? Je alikuwa anatafuta kiki baada ya kunusurika kuuawa na kuachishwa ubunge? Je alikuwa anatafuta urais ili kulipiza kisasi au kujaribu bahati yake? Je huu si ushahidi kuwa kama angeshinda, angeweza kutumiwa kirahisi na wakoloni na maadui wa taifa? Alikaririwa na vyombo vya habari kuwa anakwenda Ubelgiji kuendesha mapambano dhidi ya maovu nchini. Du! Ya kweli haya? Je Lissu anakwenda Ulaya ili kuwapigia magoti wazungu wamtumie kudhoofisha juhudi za kuijenga Tanzania ambazo haziwapendezeshi kutokana na nchi kuachana na uombaomba na utegemezi? Ama kweli mjenga  na mbomoa nchi ni mwananchi mwenyewe.
                     Kama Lissu angeweza kujibu maswali hayo hapo juu na mengine tena bila jazba na matusi, huenda watanzania wengemwelewa. Sijui hao watanzania takriban milioni mbili waliomwamini kura zao wameshauriana naye? Je kweli hali Tanzania ni mbaya kama anavyotaka Lissu ionekane au kuna visasi vya kukosa ubunge na baadaye urais? Je aliyemshauri Lissu amemshauri vizuri? Maswali, hakika ni mengi kuliko majibu.

No comments: