Taarifa za mauaji ya wanandoa zinazidi kuongezeka kiasi cha kukera na kutisha. Haupiti mwezi bila kusikia taarifa za mume kumuua mkewe kwa sababu mbali mbali kuu ikiwa wivu wa kimapenzi. Je mauaji haya yanasababishwa na wivu wa kimapenzi au ujinga, tamaa, uvunjifu wa maadili na mengine mengi?
Kwanza, niweke wazi. Mie ni mwanandoa ambaye nimedumu katika taasisi hii kwa miaka 25. Hivyo, licha ya uzoefu wangu kutosha, ninao uzoefu wa kutosha kuweza kuangalia ni wapi tumejikwaa kama jamii. Hii ni kutokana na sababu zifuatazo:
Mosi, tangu nifunge ndoa na mke wangu, hatujawahi kupigana wala kutukanana hata mara moja. Siyo kwamba sisi ni malaika au wakamilifu. Hapana. Ni kwa sababu tumekubali kusomana na kukubali mapungufu yetu na kuyafanyia kazi.
Pili, welewa wetu ni kwamba duniani tunaisha mara moja. Hivyo, hupenda kutumia kila fursa na kuifaidi hasa ikizingatiwa kuwa hatujui tutakufa lini. Katika kuhakikisha hatupoteze fursa hii ya kuishi, uhakikisha tunakosoana bila kutishana au kudharauliana tukijua kuwa sisi si wakamilifu na hatujui yote.
Tatu, sisi ni wapenzi wa amani. Hivyo, tangu tunakubaliana kufunga ndoa, tuliahidiana kuwa familia ya amani kitu ambacho tungependa kuwarithisha watoto wetu si kwa kuwaasa bali kuwapa fursa waangalie wenyewe kwa macho.
Nne, tunaamini kuwa hakuna binadamu mkamilifu hata mmoja. Badala yake kuna watu wenye upungufu ambao ni vizuri kukubali kuishi nao huku tukirekebishana kwa imani kuwa kuna siku tutafanikiwa kupunguza mapungufu yetu na kuyafanya kuwa fursa.
Sasa ngoja tutoke nje na kuangalia chanzo au vyanzo vya huu ukatili katika ndoa. Kwa uzoefu wangu kama mwanandoa na mwanataaluma ya mahusiano na usuluhishi wa migogoro naomba nijielekeze kwenye sababu kuu zifuatazo ambazo zaweza kuwa vyanzo vikuu vya mauaji na ukatili katika taasisi hii adhimu na muhimu iitwayo ndoa.
Mosi, wanandoa wengi huingia kwenye taasisi hii bila kujiandaa au kujipa nafasi ya kusomana na kuangalia mambo wanayoweza kukubaliana, kutokubaliana, kufanana au kukinzana kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo:
A) ujinga ambapo wahusika hufanya mambo bila kujipa nafasi ya kutafuta lau ushauri na ujuzi juu ya taasisi hii isiyoepukika katika maisha.
B) wapo wanaosukumwa na tamaa iwe ya ngono au vitu vingine kama elimu, mali na mambo mengine ukiachia mbali upofu na haraka ya kufanya mambo. Kuna makabila nchini ambapo wazazi huwaambia mabinti zao kutafuta wanaume wenye fedha au taaluma zinazoingiza fedha kama vile biashara, udaktari, uhasibu, uanasheria au zenye kuvutia rushwa bila kuangalia watu wanaoolewa nao. Unaweza kupata mume mwenye sifa hizo hapo juu mfano mfanyabiashara wa mihadarati, jambazi au hata mnyanyasaji na muuaji. Mara nyingi makabila haya ni ya watu wavivu kutafuta na wanyonyaji wanaowageuza mabinti zao vitega uchumi na ‘chuma ulete’wasijue madhara yake yanaweza kuwa makubwa hata vifo. Hawa ni wengi. Huwa hawajiamini na wanaamini katika waganga wa kienyeji na ujinga mwingine.
Mara nyingi wanawake wanaofuata ufanisi au utajiri wa mume hujikuta kwenye matatizo kama vile kutothaminiwa kama walivyotegemea hasa kwa wale wanaojua walifuata ufanisi au utajiri wao. Hawa gold diggers au wachimba dhahabu kwa kimombo, wanaishi maisha ya mbwa. Kwani, wanatenzwa kwa vitu badala ya utu kwa vile walifuata vit una hawakuwapenda wenzao kimapenzi bali kivitu. Wengine wanapozidiwa, ima huwaua waume au kuwageuka waume zao na kutaka waachane ili kugawana au kupewa mali kiasi cha kuwaacha watoto kwenye matatizo yasiyo na sababu zaidi ya tamaa.
Gold diggers mara nyingi ni wasichana wahuni waliopoteza muda wao kiasi cha kupoteza mvuto au wengine waliotumia fursa vibaya tokana na sababu mbali mbali kama vile kuchagua sana, kuringa au kuponda maisha ukiachia wale ambao wengine ni bahati mbaya tu.
Pili, wapo wanaoingia kwenye taasisi bila maandalizi ambapo wahusika hujikuta wanaingia kwenye taasisi ya kudumu kana kwamba ni ya muda. Mfano, wale wanaopeana mimba au kuzidiana akili. Kuna wasichana wengi hasa ambao wameishakata tamaa. Wakipata mtu wa kufanya nao urafiki, watafanya kila mbinu lau watoe nuksi. Mara nyingi hawa huwapata wanaume wasio na uzoefu na kuwasukumiza kwenye ndoa ambazo mara nyingi huishia kuvunjika pale wenza wao wanapokomaa na kukekengeuka kwa kujikuta wameigizwa mkenge.
Tatu, sababu nyingine ni uvunjifu wa maadili. Mfano, kutegesheana mimba au kufungishana ndoa za mkeka bila kujua udhaifu na ubora wa wanandoa kwa vile wahusika walivunja maadili na kuanza kufanya mambo yasiyokubalika kimaadili kijamii. Hili linawakumba sana wanaume wazinzi na wanaotaka kuchezea watoto wa wenzao.
Nne, ulimbukeni wa kuiga mambo nao unaweza kuwa sababu katika wakati huu wa mitandao ambapo wanandoa hukutana kwenye mitandao na kuamua kuoana bila kufanya utafiti na kujipa muda wa kutosha. Juzi juzi nchini Marekani, binti mmoja wa kikenya aliyekuwa akisomea unesi, alipotea baada ya kupata mwanaume wa kizungu kwenye mtandao ambaye anatuhumiwa kumuua na kutumia akaunti yake ya benki iliyokuwa na dola kama laki tatu hivi. Je ni wauaji wangapi wamo kwenye dating sites?
Tumalizie kwa kushauri jamii ianze kurejea kwenye maadili na kuanza kujiuliza ni wapi ilikosea. Wale wanaoendekeza kutaka wachumba matajiri waache uvivu watafute. Kwani kufanya hivyo kunawaponza watoto wao. Wale wanaokurupuka waache na kuanza kufanya utafiti, kusomana, kuhojiana na hata kutafuta ujuzi juu ya taasisi ya ndoa. Kimsingi, ndoa ni kama taaluma. Inahitaji maandalizi na muda wa kupata ujuzi na kufikia uamuzi. Kikubwa zaidi ni upendo wa kweli na uvumilivu hasa ikizingatiwa kuwa ndoa siyo urafiki wala suala la muda mfupi bali ni fursa moja isiyo na kifani.
Chanzo: Raia Mwema leo.
No comments:
Post a Comment