The Chant of Savant

Thursday 30 June 2022

Mizengo Pinda sasa ni hazina itumiwe vyuoni

Katika kupitia kwenye mitandao kujipumzisha, kujielimisha na kujua kinachoendelea nyumbani, nilibahatika kupata clips za Waziri Mkuu Mstaafu Ndugu Mizengo Pinda ambaye nimetokea kumkubali hasa baada ya kustaafu na kufanya mambo tofauti na wengi. Kwa wale ambao hawajawahi kuona clips za nguli huyu wa uongozi na ujasiriamali, nawashauri wazitafute. Kwani, watafaidika sana.

       Japo nimewahi kuona clips za viongozi wengine wastaafu kama vile rafiki yangu kipenzi, Mzee Pius Msekwa (Ol Doinyo Lengai au Mlima wa Mungu au Mountain of God (MoG) ulioota kwenye kisiwa cha UK, akisoma ataelewa na kucheka) Jakaya Kikwete na Hayati Chrisant Mzindakaya, hakuna aliyenivutia na kumkubali kama mzee Pinda hasa tokana na ubunifu, utundu na utayari wake. Simjui bwana huyu binafsi kama nimjuavyo Mzee Msekwa. Hivyo, namjadili kutokana na kumsikiliza kwenye mtandao, jambo ambalo kitaaluma na kiutafiti linakubalika.  Niko namalizia tasnifu yangu juu ya Ujamaa ulivyopambana na ukabila na kuushinda Tanzania kwa kutumia njia hii ya mahojiano ya washiriki kupitia clips zao pamoja na ile nyingine iitwayo autoethnography (sina tafsiri). Haya tuyaache ni ya kitaaluma japo si vibaya kumegeana maarifa bila malipo.

       Niende moja kwa moja kwenye mada ya leo ambayo ni juu ya ndugu Pinda ambaye ustaafu wake ni kivutio cha pekee kwa wale wanaopenda kustaafu na kuendelea kuchapa kazi na kufaidi ustaafu wao kwa kuzalisha na kuwezesha wengine. Kusema ukweli uwekezaji kule Zuzu Dodoma unavutia kila mwenye akili. Si mchezo. Amewekeza kwenye kilimo kiasi cha kuanza kuwa kama taasisi ya kilimo kwa vijana wanaohangaika wakisaka ajira wasipate na kuishia kukata tamaa wakati kuna fursa ardhini zinazoweza kuwatoa. Kinachovutia kwenye uwekezaji wake ni ile hali ambayo nitaiita usetishaji au umsetoshaji yaani kuchanganya mazao mengi kwenye eneo moja. Licha ya kuwa njia ya kitaalamu ya kuongeza uzalishaji na kupambana na wadudu waharibifu, inafurahisha na kutoa fursa ya kujifunza juu ya mazao mbali mbali kwenye sehemu moja.

       Ukiachia uwekezaji katika kilimo, ndugu Pinda halimi kwa ajili ya kula tu bali hata kuuza. Je anaposambaza, licha ya kushiriki biashara, anatengeneza na kutoa ajira ngapi kwa wasambazaji wadogo wadogo kama vile mama mboga? Hapa ndipo iliposiri ya kutaka vyuo vya biashara na kilimo vimtumie katika masomo yake ya kuoanisha nadharia na vitendo. Maana, namna alivyoweka kwenye vitendo nadharia ya biashara na kilimo––––kama wahusika watamshawishi akawa anatoa mihadhara––––kunamfanya afae kuwa nguli katika maeneo haya muhimu katika uzalishaji na utengezaji fursa na ajira.

       Mbali na Ndugu Pinda kufaa kuhadhiri juu ya nadharia na vitendo katika fani ya biashara na kilimo pia uwekezaji, anafaa kuwa mshauri mzuri wa wastaafu ambao wengi wao maisha yao huwa magumu baada ya kustaafu wakati kuna fursa lukuki. Naamini wasomaji wangu ima ni wastaafu, wastaafu watarajiwa au wenye ndugu hata wazazi ambao ni wastaafu.

Je kuna nini kati miradi ya ndugu Pinda?

Kwanza, licha ya kutoa kipato, kwa wastaafu, inawapa fursa ya kujiwajibisha, kupata fursa ya kufanya mazoezi ya kiakili na kimwili kupitia kufanya kazi bila kusimamiwa na kujitegemea ukiachia mbali kuendelea kuzalisha na kutumia fursa na nguvu zao vizuri kwa ajili yao binafsi na wengine kama anavyofanya ndugu Pinda.

Pili, kuna ridhiko la moyo ukiachia mbali kujijengea kujiamini na kuachana na hofu za kustaafu. Sijawahi kustaafu japo najua hofu ya kuacha kile ambacho umekuwa ukifanya toka ujana wako na kuanza maisha mapya ambayo huna uzoefu nayo.

Tatu, unaongeza ujuzi ambao hukuwa nao na kuweza kukamilisha ndoto zako za kufanya mambo ambayo hukupata muda kuyafanya. Kwa wasataafu wanandoa, ni fursa ya kufanya kazi pamoja na kupata uzoefu mwingine unaoweza kuwasaidi wengine baadaye.

Nne ni sehemu yakufanya mazoezi ya kiakili na kimwili ukiachia mbali kujifunza ujasiriamali na uwekezaji kwa wale ambao biashara siyo fani yao. Hakuna kitu kinapambana na uzeekaji kama kuupa ubongo mazoezi. Angalia watoto wanavyojifunza hata wakiwa usingizini na wanavyoongeza nguvu na ujuzi. Hii ni faida ambaye kila mtu angependa aipate katika maisha yake.

Tukijielekeza kwa vijana ambao ima wanatafuta ajira au fursa, Ndugu Pinda ana dozi yenu. Katika mahojiano mengi amesema wazi anavyowapenda vijana ambavyo uko tayari kuwafunda na kuwasaidia. Mliokuwa mkimuona kwenye runinga, nadhani hii ni fursa mara mbili. Kumfahamu na kumtumia. Hata nasi tukirejea nyumbani, lazima tumtafute na kumtumia. Katika vita yake dhidi ya njaa, umaskini, ukosefu wa ajira na utegemezi visivyo na sababu kwa bara lililojaliwa kila kitu. Tofauti na vyuo ambavyo hutoza ada kali kutoa maarifa, Ndugu Pinda anatoa bure. Je wangapi wanalijua hili na wako tayari kulifaidi?

Mbali na kutoa msaada wa maarifa kwa vijana, uwekezaji wa Ndugu Pinda unawapa motisha makundi mawili tajwa yaani vijana na wastaafu na hata watu wote wazima wenye kutaka kuwekeza katika kilimo. Hivyo, anachofanya Ndugu Pinda siyo kwa vijana na wastaafu tu bali hata kwa viongozi walioko madarakani ambao ni wastaafu wa kesho na waliostaafu.

Leo nitafupisha makala hii nikiahidi kujipa fursa ya kumsoma zaidi gwiji huyu wa kilimo na uwekezaji lau nielezee ninavyomtafakari kitaaluma. Natamani hata kuandika kitabu juu yake na mawazo yake hasa baada ya kustaafu uongozi na utumishi wa umma. Hongera Ndugu Pinda kwa unavyofanya japo unaweza usione umuhimu na ukubwa wake kwa jamii japo wewe uliwekeza binafsi usijue matokea yake yatakuwa makubwa kuliko wewe. Nategemea uongozi wa gazeti hili utapanga ufunge safari kuja kukuhoji kwa mengine mengi kama utaamua.

Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: