Hakuna shaka wala ubishi hata chembe. Maneno mazito na ya kizalendo ya Mheshimiwa Mbunge wa Gairo (CCM) Ahmed Shabiby ambaye alisema kuwa wachina wanaingia Tanzania kama shamba la bibi wakati watanzania wakizuia kuingia China kwa kisingizio cha Ukovi yanahuzunisha na kuamsha hasira kiasi cha kuhoji uwezo wetu wa kufikiri. Shabiby alitoa duku duku hili akichangia kwenye kikao cha Bunge kinchoendelea. Mchango wa Shabiby na wengine ulinifanya kujiuliza swali moja kuu. Je China mkoloni mpya tena wa kiuchumi? Je ni wangapi wanaliona hili na wanafanya nini kulidurusu na kulipatia jawabu mujarabu? Je hali ikoje? Je nani alaumiwe hapa kati yetu na wachina waliotugeuza kichwa cha mwendawazimu kinyozi kujifunzia kunyoa? Je nani anafaidika na nani anaumia na kwanini? Haya ndiyo maswali leo nitajaribu kuyadurusu na kuyapatia majibu.
Mbali na Mhe. Shabiby, mwingine aliyegusia suala la wachina kutuhujumu ni Mhe. Joseph Kasheku Msukuma (Geita, CCM) aliyeonyesha uzalendo wa aina yake akichangia hoja ya uraia pacha. Mhe. Msukuma bila woga, aligusia suala la wachina kutamalaki nchini na mashine za kuchezesha kamari. Je tumeshindwa kununua hizi mashine na watu wetu wakazitumia na kupiga fedha kama wanavyofanya wachina au hawa wageni kuna vigogo nyuma yao ambao hawataki kuona ukweli? Je ni mchezo ule ule kama tuliowahi kufanyiwa wakati wa sakata la jambazi Chavda aliyekuwa akitumiwa na baadhi ya wakubwa wasiowaaminifu kuhujumu taifa letu? Hivi kweli hatuna watu wenye uwezo wa kununua na kusimamia mashine za kamari hadi waje wachina? Je hatuna watu wenye uwezo wa kufanya umachinga wanaofanya wachina kweli ama tunahujumiana?
Niseme wazi. Kwanza, huu ni ubaguzi tena wa kujibagua na kuwapa nafasi wengine watuumize hata kutubagua kama wachina walivyoonyesha wakati wa kuzuka kwa Ukovi ambao unasemekana ulianzia kwao kwenye mji wa Wuhan. Pamoja na ukweli huu, wale wale walitubagua waafrika na kusingizia kuwa gonjwa hili lilotokea Afrika wakati lilitokea Wuhan. Pia, kama wenzao toka Asia, wanajulikana kwa ubaguzi wao japo si wote.
Je kwanini nasema tunajibagua na kuwapa wabaguzi fursa ya kutubagua na kutunyonya kirejareja? Tumewaruhusu wachina kufanya umachinga kwetu ambapo hatuwezi kufanya hivyo kwao. Mhe. Shabiby alishangaa kuona wachina wakiuza plastiki Kariakoo kana kwamba watanzania hawa uwezo wa kufanya hivyo. Alitahadharisha kwa uchungu kuwa tusipoangalia, tutabakia kufanya umachinga wa mazao yetu huku bidhaa nyingine wakichuuza na kuuza wageni.
Mbali na kufanya umachinga nchini wakati sisi haturuhusiwi kufanya hivyo japo, hata hivyo, hatuna machinga wa kwenda China, tumewaruhusu wachina kuingia nchini watakavyo wakati sisi haturuhusiwi hata kwenda kwao. Je hapa tutawalaumu wachina kwa kuingia nchini watakavyo wakati wakiwazuia watu wetu kwa sisi kushindwa kuwapiga marufuku? Rejea mchango wa Mbunge Shabiby bungeni akilalamikia utitiri wa wachina mitaani wakifanya umachinga. Nani anaweza kuuza mahindi nchini China au kuuza mitishamba kama wafanyavyo wachina kwetu? Je hatunao waganga wengi wa kienyeji wakichina hata kikorea na wengine wasiojua Kiswahili wala kiingereza wanaouza mitishamba ya kichina na kikorea kana kwamba sisi hatunayo? Je huyu mtu asiyejua Kiswahili anawasilianaje na wateja wake? Je mitishamba yake ni salama au hatarishi? Nani anagahaika kuipima na kujiridhisha na viwango vyake? Je kuendelea kuruhusu upuuzi huu siyo kuweka afya za watu wetu rehani?
Mbali na madawa ya kienyeji, wachina wanasifika kwa kutuletea eti madadawa ya kuongeza makalio wakati wachina wenyewe hawana hayo makalio. Nani anahitaji makalio hadi yapanuliwe? Je huku siyo kutumia ujinga na ulimbukeni wetu kutuumiza? Nani anajiuliza wapi pa kuwapata hawa waleta madawa ya makalio kama yataleta madhara kwa wapumbavu wetu wanaoyapwakia? Wanawajaza watu wetu kansa na upumbuvu huku nasi tukichekelea kana kwamba hayatuhusu. Tumekuwa wa hovyo kiasi cha kufanyiwa majaribio na kuruhusu watu watufanya shamba la bibi kirahisi hivi! Je hapa nani amlaumu nani kati yetu na wachina na wengine waliotugeuza shamba la bibi?
Sitashagaa kukuta wachina wakianza kuuza mahindi hata ugoro kwa vile sisi tumelala na kuzubaa. Sitashangaa kutukuta kile kinachowakuta wakenya kwa sasa ambapo wanaagiza samaki waliolishwa madawa wakati wachina wale wale wakisafirisha samaki safi toka Kenya kwenda kwao. Sitashangaa kuona wachina wakigeuka madalali wa majumba tena yetu kwa vile sisi tumelala fofo na kuzubaa. Sitashangaa kukuta wachina wakijazana kwenye migodi yetu mbali na mbuga za wanyama wakiwinda na kuongoza watalii wakati watu wetu hawana ajira wala namna ya kufaidika na raslima za taifa lao walizopewa na Mungu.
Nimalizie kwa kusema wazi kuwa sina chuki wala ugomvi na wachina na wageni wengine kama watafuata sheria na taratibu na kufanya shughuli wanazopaswa kuzifanya chini ya sera ya uwekezaji lakini siyo umachinga. Pia nichukue fursa hii kuisihi na kuishauri serikali iangalie kwa makini kadhia hii ya wachina na wageni wengine ambao wanafanya shughuli ambazo kisheria zinapaswa kufanywa na watu wetu. Pia, ufanyike uchunguzi kuhusu namna wachina na wengine wanavyoruhusiwa kuingia nchini na kuvunja sheria kwa kufanya umachinga. Kama tumechoka sana hivi, basi wekeni masharti lau ya kuwalazimisha wageni kumilki hizi biashara kwa ubia wa nusu kwa nusu na wananchi wetu lau taifa lifaidike na fursa hizi tunazovuja kwa mauti ya taifa na watu wake. Kila siku Mhe. Rais anahubiri diplomasia ya uchumi ilhali nyumbani anahujumiwa na mazabe na uzembe kama huu.
Chanzo: Raia Mwema.
No comments:
Post a Comment