The Chant of Savant

Thursday 23 June 2022

Dini ni janga jipya kwa Afrika (I)

 


Japo tunaaminishwa kuwa lengo la kuwapo dini ni kuwakomboa wanadamu tokana na dhambi ambazo hata hivyo hazieleweki barabara, zimeanza kuwa chanzo kikubwa cha maangamizi kama ilivyokuwa wakati zikianzishwa ambapo karibia dini zote kubwa zilishiriki maangamizi ya wale wote waliozipinga wakati zikianzishwa. Ukristo wa Kiroma ambao ndiye baba na mama ya ukristo wote unasifika kwa kushiriki kwenye kile kilichoitwa inquisition au patilizi ambapo wapinga dini walichoma moto, kuzamishwa hata kunyongwa kwa vile hawakukubaliana na mambo ambayo waliona hayawaiingii akilini.
    Uislam kadhalika uliwasulubu wale wote walioupinga zama zile za vita ya jihad ukiachia kupitisha sheria kali za kuchinja au kuua kati masuala mengi ambayo hayakuhitaji.  Hata hivyo, wasiojua siri ya kutumia adhabu ya kifo sana kuwa ni kutokana na kutokuwa na magereza ya kuwawekea hao wabaya wao.
        Sasa hebu tuangalie namna historia ya uovu wa dini za kimapokeo inavyoanza kujirudia. Hivi karibuni huko Nigeria, waumini wa kikristo zaidi ya 20 waliuawa wakiwa wanasali kwa kupigwa risasi na kurushiwa mabomu. Kisa, eti kundi la kigaida la Boko Haram lilikuwa linatafuta namna ya kuihangaisha serikali! Tulishuhudia makundi mengine kama vile al Shabaab, al Qaida na ISIL na mengine mengi yalivyotaka kutumia dini kupata madaraka ya serikali bila mafanikio. Hata hivyo, yameumiza watu wengi wasio na hatia ima kwa kuwaua au kuwaingiza kwenye jinai ya kipumbavu kwa ahadi uchwara na upuuzi mwingine mwingi. Kwani, hayakuwambia wapumbavu wengi yanaotumia kuwa yanachotafuta ni madaraka kama ilivyo kwa Taliban huko Afghanistan bali si dini pepo wala nini.
        Mbali na ugaidi, waafrika wengi wajinga wameingizwa upumbavu wa kuamini miujiza badala ya kufanya kazi na uhalisia. Hili limejenga misingi ya ushirikina na uvivu kiasi cha mtu kuamini kuwa akimuua mwenzake na kumtoa kafara anaweza kupata utajiri na asiamini kuwa akifanya kazi wa bidii na maarifa anaweza kuukata. Wapo waliowatoa watoto wao kafara ukiachia waliojitoa kafara wenyewe na kudhalilishwa na waganga. Watu wanahubiriwa miujiza isiyokuwapo wanaaamini na kuibiwa kidogo walicho nacho bila msaada. Ajabu hata serikali zetu zimeendelea kufumbia macho jinai hii ya halaiki kwa vile inaweza kuitumia na kufanya mambo yake bila upinzani wala kusumbuliwa.
    Hakuna dhambi kama vile kuchukiana na kutenganishwa kwa waafrika kwa faida ya wakoloni. Waislam wanawaita wasio waislam makafiri. Wakristo wanawaita wasio wakristo waliopotea utadhani wao hawajapotea kwenye ukoloni wa kimila! Nani ambaye hajapotea wakati anaona fahari kuitwa majina ya kigeni huku akionea yake aibu au hata kuyatukana pamoja na mila zake? Watu wanachukiana na kushindanisha miungu yao huku wakiitukana yetu kana kwamba kuna anayejua ikoje. Miungu yote ina siri na fanani moja. Yote haionekani, haisemi, haifanyi chochote isipokuwa watu.
        Dini zimefanya baadhi ya watu wetu walio wajinga kuukana ukweli kuwa wao walikuwa na dini zao zenye kuwafaa kwa maelfu ya miaka kabla ya kuingizwa kwenye dini za kigeni na kinyonyaji. Tokana na ujinga na ulimbukeni wao––––chini ya kisingizio cha uhuru wa kuamini–––wameukana ukweli. Wamejipa haki ya kuhukumu wenzao wasioamini kwenye mambo yao bila kukubali kuwa nao wana uwezo na sababu za kuwahukumu. Wamejipa utukufu na ukuu na kuwadhalilisha wengine wasijue nao ni ukoloni unaowafanya nao wawe wakoloni. Heri ya wakoloni. Hawakuwa ndugu wa damu wa wale waliowatesa na kuwatawala sawa na waswahili wanaotawalana na kuchukiana kwa sababu ya tofauti za kidini. Tena wengi wanajiita wasomi wakati wamekaririshwa ukoloni wa kimila na wakoloni. Wanabaguliwa na kujibagua na kubaguana. Lakini hawajitambui kwa vile hawajitambui.
        Hivi tukisema kuwa dini zimesababisha waafrika kupoteza utambulisho tutaambiwa tunakufuru? Mmakonde anaitwa John Johson siyo Kachere wa Nkapa. Msukuma anaitwa Ahmed Mohamed kana kwamba ni mwarabu. Kamwambie mwarabu au mzungu aitwe majina ya Kiafrika. Atashauri upimwe akili kama siyo kukutemea mate.  Mwambie mwarabu kuwa Mungu anajua kimakonde. Atashauri upigwe mawe hadi ufe. Kwanini? Kwa sababu anajua udhaifu wako wa kujichukia na kujikana. Pia, atakwambia umekufuru nawe utaogopa na kutetemeka wakati hakuna kitu kama hicho. Tumeuziwa mbuzi kwenye gunia nasi tukanunua. Angalia kashfa za ulawiti na uzinzi kwenye kanisa tena kubwa kuliko yote au tuhuma mballi mbali za wanaitwa walimu wa dini au na wengine kujihusisha na jinai ya zinaa. Ukihoji, unaambiwa dini nao ni tofauti. Ni maji gani safi yafua nguo inabiki chafu? Ni manukato gani yanamfanya mtu anukie vibaya yakabaki manukato?  Ni utajiri gani unamfanya mwenye nao alale njaa na kuomba ubaki utajiri?  Hivi nani alituroga kushobokea vya wenzetu huku tukiviponda vyetu?
        Mwisho, ukisikiliza sababu, kwa mfano kwa waarabu kushushiwa mitume na dini eti ni kwa vile walikuwa wametenda madhambi ya kutisha kama vile yale ya Sodoma na Gomora. Hapa Afrika tunaingia vipi? Wachina na wajapan waliambiwa hadithi kama hizi wakawambia wahausika kuwa wao sio wachafu kama wao na hivyo, hawahitaji suluhu ya matatizo yasiyohusika. Waafrika, kwa ujinga, walipwakia. Watoto wenu wakibakwa na kulawitiwa mnaanza kulalamika wakati mliishaambiwa msielewe. Historia ina tabia ya kujirudia ukiachia mbali dini kuficha mambo mengi kama vile kusaidia ukoloni kuingia Afrika mbali na unyonyaji usioisha kwa visingizio mbali mbali. Sasa tazama watu wetu wameharibiwa kiasi cha kuamini kila upuuzi wakaacha kuchapa kazi. Tumeanza kuana sisi kwa sisi. Hapa ndipo dini zinapogeuka janga jingine na aina nyingine ya ukoloni Afrika.
Chanzo: Raia Mwema.

No comments: