Japo mie si msemaji wa Ikulu, Rais wala Tanzania, leo nataka niongelee jambo ambalo wengi hawajalielewa vizuri ima tokana na kutoelimishwa au wahusika kutolifanyia kazi ipasavyo japo si wote. Rais Samia Suluhu Hassan ameanzisha kitu kipya baada ya kurithi utawala tokana na kifo cha bosi wake Rais John Pombe Magufuli (Mungu Ailaze Roho Yake Peponi). Alipoingia madarakani, kwanza, wengi hawakuamini angefaa na kufanya mambo ambayo ameyafanya ukiachia mbali kuendeleza yale aliyorithi toka kwa mtangulizi wake. Hata hivyo, Mama kajitutumua na kufanya mambo–––taka usitake.
Pamoja na mengi ambayo ameishafanya kwa muda mfupi, Rais amejitahidi kuja na ubunifu kwa kiwango ambacho–––hadi sasa kinaridhisha, kama mambo hayatabadilika––––kwa kuja na mambo mapya na tofauti na mtangulizi wake. Leo siyo siku ya kumpa kadi ya repoti ya utendaji wake. Kwa upekee, naomba nigusie kile kinachoitwa Royal Tour au Safari ya Kifalme–––ya kuitangaza Tanzania na vivutio vyake ambayo Mheshimwa Rais alifanya hivi karibuni nchini Marekani. Japo imetangazwa sana bila kutoa elimu juu ya umuhimu wake hasa kwa wananchi wetu ambao ni wadau, kwa kiwango kikubwa, inaweza kunufaisha taifa letu.
Je kwanini leo naongelea kitu ambacho kidogo kimepita? Kuna rafiki yangu aishie Marekani ambaye, sawa na wengine wengi, anaonekana kutopata kilichofanyika na madhumuni yake. Alinitumia ujumbe wa barua pepe akilalamika kuwa kwanini Rais alipoteza muda wake kutangaza utalii na kutumia mamilioni ya shilingi ‘kutanua’ wakati mabalozi hata Mawaziri wa Mambo ya nchi za nje na wa utalii wangeweza kufanya hivyo. Rafiki yangu alilalamika na kulaumu sana bila kujua au kuhoji upande wa pili.
Je Royal Tour ni nini? Kwa tafsiri rahisi, Royal Tour ni safari ya kifalme ambayo mara nyingi hufanywa na wafalme au wana wa wafalme nje au ndani ya ufalme wao. Hata hivyo, kwa hii ya Tanzania, imepewa jina hili tokana na nafasi ya Mheshimiwa Rais hata kama siyo mfalme au malkia lau kuvutia wengi. Japo sijui mantiki ya kuiita hivyo, nao ni mojawapo ya ubunifu wa kuvutia wawekezaji na wale wote ambao wangeshawishiwa nayo.
Je faida zake ni zipi? Nadhani zipo nyingi. Hapa nitataja baadhi japo kwa uchache kama ifuatavyo:
Mosi, kwa mujibu wa msemaji wa Ikulu Zuhura Yunus, Royal Tour imeiwezesha Tanzania kusaini mikataba saba ya jumla ya shilingi trilioni11.7 zenye uwezo wa kutengeneza ajira zaid ya laki tatu kama zitakamilika. Kwa taifa maskini kama letu, hii siyo chenji ya mboga wala fedha kidogo. Pia kiwango cha ajira zitakazotengezwa si haba hata kwa viwango vya nchi tajiri kama Marekani. Kazi zitakazotengezwa na matokeo haya ya Royal Tour visibezwe vinginevyo wanaofanya hivyo watupe takwimu zao.
Pili, Mheshimwa Rais alipata fursa ya kujitangaza binafsi kama Rais mpya wa Tanzania. Si rahisi kwa viongozi wa kiafrika kukutana ima na Rais wa Marekani au Makamu wake. Lakini katika ziara hii, Mheshimiwa Rais aliweza kukutana na Kamala Harris, Makamu wa Rais wa Marekani jambo ambalo ni nadra kwa viongozi wa kiafrika tokana na mfumo wa kikoloni na mataifa makubwa kuyadharau. Hapa tumpongeze Rais kwa ubunifu ulioweza kupenya ukiritimba wa mataifa haya koloni hasa wakati huu ambapo nguvu zao nyingi zimeelekezwa Ukraine.
Tatu, Mheshimiwa Rais pia aliweza kwenda Uganda kukazia ujenzi wa bomba la mafuta ambalo nalo litaingizia taifa mabilioni ya shilingi na ajira si haba. Ikumbukwe kuwa Uganda iliingia makubaliano na Kenya kupitisha bomba hili kabla ya Hayati Magufuli kuingilia kati na kuleta mradi huu Tanzania. Hili si jambo dogo hasa kwenye wakati huu wa ushindani. Kama Mheshimiwa Rais asingekazia, nani ajuaye kipi kingeendelea kwenye mradi huu baada ya kufariki Magufuli?
Nne, Royal Tour imetangaza na kuimarisha utalii nchini. Ni bahati nzuri kuwa mmojawap wa walioshiriki ziara hii ni Sirili Akko, Katibu Mkuu wa Tanzania Association of Tour Operators (TATO) ambaye alikuwa kwenye msafara husika. Nilikuwa nikiwasiliana naye kila mara tangia New York hadi Los Angeles. Kimsingi, Akko alionekana kuvutiwa sana na Royal Tour kwa kuwaunganisha waendeshaji shughuli za utalii nchini na wale wa Marekani. Hili nalo si jambo dogo hata kidogo.
Kabla ya kumaliza, sasa ngoja tuone kile kinachoonekana kama utata wa Royal Tour na kumshirikisha kiogozi wan chi. Kwanza, ifahamike kuwa Mheshimiwa Rais ni kila kitu namba moja nchini. Ni kiongozi namba moja. Ni raia namba moja. Ni mfanyabiashara namba moja. Ni muongoza utalii namba moja. Ni balozi namba moja. Hivyo, anapoamua kufanya shughuli yoyote kisheria ni jukumu lake. Wengine wanaofanya shughuli kama vile idara na wizara wanamwakilisha yeye. Hivyo, wale wanaoona kuna’utata’ kwa Mheshimiwa Rais kuongoza Royal Tour kutangaza vivutio vya Tanzania wajue kuwa yeye ndiye mtangazaji wa vivutio vya taifa namba moja pia naye akiwa kivutio kinachovutia wengi kila anapokuwa.
Kwa wale wanaojua umaarufu wa Rais wa Marekani na dege lake la Airforce One, watakubaliana nasi kuwa kuna mbinu nyingi kwa mataifa kujitangaza na vivutio vyake mojawapo ikiwamo Royal Tour. Hivyo, Mheshimwa Rais kuongoza Royal Tour alifanya kazi yake bila kuvunja sheria yoyote. Wapo wale wanaohoji inakuwaje Rais anasafiri mara kwa mara wakati mtangulizi wake hakufanya hivyo. Jibu ni rahisi kuwa Magufuli alipenda kukaa nchini na kumwachia Makamu wake ambaye ndiye Rais wa sasa kufanya kazi za kusafiri akimwakilisha. Hivyo, kwa Mheshimiwa Rais kusafari badala ya kumtuma Makamu wake ni haki ya kisheria ilmaradi safari zake zina maslahi kwa taifa na hazikumbwi na utata kama ule wa nyakati za akina Vasco da Gama ambao walipenda matanuzi nje.
Naomba niitimishe kwa kuwambo wasaidizi wa Rais kuuelimisha umma juu ya maana, madhumuni na mafanikio ya Royal Tour. Kwani wanalipwa kwa kazi hiyo. Itangaze Royal Tour ndani ya nchi sawa na hata zaidi ya mlivyoitangaza nje ili wananchi ambao, kimsingi, ndiyo wadau watakaowapokea watalii na wewekezaji wawe sehemu ya Royal Tour. Kuwaelimisha wananchi, licha ya kuwafanya sehemu ya mkakati mzima, kutaepusha lawama na upingaji visivyo na msingi. Kama hamtawaelimisha, ni haki yao kulalamika juu ya Royal Tour na kuiona kama tata kama ilivyokuwa kwa rafiki yangu aliyenilalamikia.
Chanzo: Raia Mwema, June 29, 2022.
No comments:
Post a Comment