Mie kama rahis mpendeka na msikivu wa Mafyatu nina bonge la soo ambalo nawamegea kidogo tokana ufyatu wa Mafyatu wanaotaka kujifanya kunifyatua wasijue nitawafyatua kiroho mbaya na kifyatufyatu. Kama rahis aliyeko juu ya kila kitu, nimepewa mamlaka na katiba kuteua na kutengua nimtakaye bila kutoa maelezo kwa yeyote hasa pale nimapomfyatua. Hivyo, tangu niangukie urahis wa Mafyatu, nimekuwa nikifanya kazi kuu tatu, yaani kuteua, kutengua, na kufyatua. Napenda sana hii kitu kwa sababu inafanya kila Fyatu aniogope na kunishobokea akitegemea nimpe uteuzi ili aweze kuwafyatua Mafyatu bila mimi kumfyatua wala yeye kunifyatua.
Pamoja na mamlaka niliyopewa na Mafyatu waliofanya kosa kufanya hivyo, wapo Mafyatu ambao wameanza kunichora na kunisengenya kuwa siko makini katika kitu hii. Hii ni kutokana na ukweli kuwa huwa nafanya uteuzi, utenguzi, ufyatuaji, na ufyatuzi kila mara tena bila kueleza vigezo nitumiavyo kufanya hivyo. Ebo! Mafyatu kweli fyatu. Nitoe maelezo na vigezo vya nini wakati mimi ni kigezo na anayejua yote ya wazi na sirini kama rahis wao?
Kutokana na kadhia hii inayowakasilisha Mafyatu, nilikuwa nimeuchuna na kuwaacha wabweka. Kwani, kelele za chura hazimzuii tembo au nguruwe kunywa au kuchafua maji kisimani. Ila, kadiri siku zinavyokwenda, naanza kujikera hata mimi mwenyewe. Hii ni kutokana na ukweli kuwa, wakati mwingine, nasahau niliowateua mbali na kutowachuja wala kujua kama wanafaa au hawafai. Hata hivyo, kwanini nijali wakati wasiofaa hawaathiri ulaji wangu wa dezo? Nijali nini wakati nina mamlaka ya kufanya nitakavyo na wakati na kwa namna nitakavyo? Mwenye wivu si ajinyongelee mbali!
Mafyatu wasiojua ugumu na unyeti wa urahis wanadhani ni rahisi. Hakuna kazi ngumu duniani kama urahis tena wa Mafyatu wasioridhika. Juzi, si nilimteua shosti wa Bi Mkubwa wangu mwenye kukabiliwa na kashfa kila aina za ufisi na ufisadi! We! Wacha Mafyatu wafyatuke na kuhanikiza! Kwa vile mie huwa sijali, nilikula pini na shosti sasa anatesa. Nilidhani Mafyatu walisahau. Kumbe, walikuwa nao wamekula pini wakinichora hadi sasa najisikia kuchoka na kuchoshwa na ulalamishi wao. Hivi, nikimteua shosti wa Bi Mkubwa hata kitegemezi changu au sweetheart wake wao inawahusu nini? Sijui kwanini Mafyatu hawakati kukubali kuwa kutesa, kuhomola, na kuhobdomola ni kwa zamu! Kwanini kuingilia mamlaka na zamu vyangu vya kujinoma mimi, familia, mashosti, marafiki, washirika, na hata mabambataa wangu wanaonifanya nijisikie raha na kuwa salama? Mkomeni na kukomaa kabla sijawakomesha vizabizabi nyie mlioshindwa kushika adabu na adabu ikawashika.
Sasa natangaza moja kwa moja. Yeyote anayeudhiwa au kulalamikia uteuzi na utenguaji wangi siyo ajinyonge tu. Ajue. Mie sichezewi na wala sitaacha kufyatua na kufanya nionavyo na nitakavyo watake wasitake. Kwani, mamlaka waliyonipa Mafyatu ni ya kazi gani kama siyo kufyatua kwa raha zangu japo kwao karaha? Kwanini hawataki kujua kuwa hawakunichagua bali nilichaguliwa na Sir God kupitia kura zao ambazo nazo nilizichakachua na kuwafyatua! Nani nyinyi mpingao kazi ya Sir God wanahizaya watupu niliowafyatua? Sasa mjue. Hata nikimteua kuku tetea wangu au jogoo wake au kumtengua malaika, hiyo si kazi yenu bali yangu. Nimeapa kufanya haya nifanyayo hata kama hayawaridhishi kwa vile hamtaki kuridhika na mkiridhika hamirdhishwi. Mamlaka ni kujiridhisha na si kuwaridhisha wengine. Loo! Sasa nini hii kuanza kufyatuka na kujifyatua mwenyewe na kutaka kuwapa Mafyatu zana za mafyatuzi wanifyatue! Hili bange nalo!
Hakuna kitu kinaniudhi kama Mafyatu kujifanya wanajua utadhani Nshomile Bwana. Mwenzenu nimesoma hadi maandishi yakabanduka mbali na maprofesa kuniomba niwafundishe. Najua visivyojulikana kwa Fyatu yeyote isipokuwa mimi. Sikosei. Na hivyo, nisikosolewe. Hakumuambiwa kuwa sisi marahis tumeumbwa kwa mfano na kupewa mamlaka ya Sir God mwenyewe? Sasa kosa langu ni nini nikitenda kama Sir God? Kwanini Mafyatu hawataki kukubali kuwa mimi ni kiumbe pekee aliyebora aliyeumbwa na Sir God baada ya kupita wale waliopita wa kwenye ngano za kale? Mie si mbabaishaji na msanii kama hao wawahubirio hao kwa mazwazwa wawaaminio wakati ni changa la mato.
Wote wanaonikosoa na kunikosea adabu wajue. Mimi sikosi, kukosea wala kukosolewa. Mjue. Nikikosa au kukosea sikosei. Kazi zangu kama vile uteuzi na utenguzi hazina makosa. Makosa ni pale wakosoaji wanapokosoa makosa wasijue kuwa kukosoa ni makosa na kukosea. Mliona wapi rahis msomi mwenye magunia ya shahada tena za juu na mwenye busara kama Abunwas akakosea? Hata kama nakosa na kukosea, nyinyi inawahusu nini?
Hapa, natoa ushauri. Kama nikikuteua, hakikisha unafanya ufanyavyo ila usinikosea. Kosea kaya lakini siyo mimi. Fanya yanipendezayo na siyo yatakiwayo. Kwani, ukifanya hivyo, sitakutengua. Huwa sipendi wajuaji wanaofanya mambo na kupingana na matakwa na matarajio yangu kama rahis wa Mafyatu aliye juu ya sheria na taratibu zote za Fyatuland ambayo, kwa sasa, ni mali yangu binafsi. Si mlinikabidhi wenyewe?
Du! Kumbe nimegundulika kuwa na ugonjwa wa kusahau!
Chanzo: Mwananchi Jtano leo.
No comments:
Post a Comment