The Curse of Salvation

The Curse of Salvation

Sunday, 11 October 2026

Namna ya kuimarisha mahaba hata baada ya kupata watoto

Kuna kisa tulisoma kuhusu wanandoa wawili. Baba hakutaka mkewe kujifungua kwa njia ya kawaida kwa kuchelea via vya uzazi vingepanuka na kuathiri maisha ya wawili hawa kingono. Hivyo, kila mama alipopata ujauzito, alijifungua kwa kufanyiwa upasuaji si kwa sababu alikuwa hawezi kujifungua kwa njia ya kawaida bali kwa matakwa na shinikizo la mumewe.
Kwanza, huu ni ujinga wa kiwango cha laami. Mama, hata ajifunge watoto mia, hakuna kinachobadilika na uwezo na utendaji wake kingono unabakia kuwa kawaida. Hivyo, wanaofanya au kuamini hivi ni matokeo ya ujinga na kukataa kujielimsha.       
            Mbali na hali hii ya kimaumbile, lipo suala kisaikolojia.Mama anapojifungua anaweza kukumbwa na kile kiitwacho postpartum depression au msongo wa mawazo baada ya kujifungua japo si wote au wengine hupata wasijue hali hii tokana na uwezo wao wa kuelewa. Hali hii mama huwa na msongo wa mawazo kiasi cha kukosa furaha, kupoteza hamu ya kula, kuchukia na kujichukia, huzuni, kujiona hana thamani na mengine mengi. Hiki huwa kipindi kigumu kwa wale wanaokumbwa na hali hii. Ni kipindi ambacho uhitaji uelewa wa hali ya juu kwa wenza wao ili waweze kuwasaidia badala ya kuwahukumu na hata kuwa sababu nyingine ya maumivu.
            Tukirejea kwenye mpito wa kujifungua, kisa kifuatacho kinaweza kutoa jibu. Wanandoa wawili waliochukua muda mrefu kupata mtoto hatimaye, walibahatika kupata mtoto wao kifungua mimba. Siku hiyo walifurahi sana na kumshukuru Mungu kwa hili.  Kila mmoja alijiona kukamilika sasa wasijue ndo ulikuwa mwanzo wa changamoto za uzazi. Haukupita muda, mama akawa bize na mtoto kiasi cha mume kujihisi kama hakuwa hakupendwa tena. Mume alianza kulalamikia hali hiii. Bila kuficha, alimwambia mkewe kuwa alikuwa akiona kama mapenzi kwake, ima yalikuwa yameisha au yalikuwa yamehamia kwa kichanga. Maskini, si mama wala baba aliyejua hali hii.
            Katika kutafuta suluhu, baba alimwendea mama yake na kumueleza kila kitu. Badala ya kumuonea huruma na kumpa jibu alilotafuta mwanae, mama aliangua kicheko kiasi cha kumsababishia maudhi na kukata tamaa mkazamwana wake. Katika busara na uzoefu wake, mama alimwambia mwanae kuwa si kweli kuwa mkazamwanae alikuwa akimchukia mwanae. Hivyo, alimshauri naye kuanza kumpenda mtoto kama ambavyo mkewe alikuwa akimpenda na hata kumjali.
            Baba alirudi nyumbani na kuanza kuonyesha mapenzi kwa mtoto kiasi cha mkewe naye kuona kama alivyoona yeye na kuanza kulalamika. Hali iliendelea hivyo kwa muda hadi wawili walipokwenda kwa mama mzazi wa mume. Kama awali, mama aliangua kicheko kwa furaha kiasi cha kuwachanganya wahusika wasijue ni kwanini.
             Kufupisha hadithi ndefu, mama wa baba aliwashauri wanandoa hawa wasimpende mtoto tu bali nao wajipende na kupendana. Waliporudi nyumbani walianza kumhudumia mtoto bila kujisahau kama mwanzo na huo ulikuwa ndiyo mwisho wa tatizo lao ambalo kimsingi, lilitokana na ukosefu wa welewa na uzoefu.  Watoto hutumia muda mwingi wa wazazi kuliko wao wautumiavyo wao kwa wazazi. Hivyo, ni vizuri wazazi wapime na kutumia muda wao katika masuala ya malezi bila kusahau kuwa nao wanahitaji kujaliwa na upendo sawa na watoto.
            Kinachotakiwa kipindi hiki ni uelewa na kujaliana ili muweze kuwalea na kuwafurahia watoto wenu. Kupata watoto ni hitajio la ndoa lenye majukumu mengi mapya ambalo linawapasa wahusika kupima mambo. Watoto na changamoto zao haviepukiki katika ndoa. Kwani, baada ya kipindi cha uchanga wakafikia balehe au kuvunja uongo, pia huwa na changamoto zake.
            Hapa kuna kisa pia. Baada ya wazazi kuzaa, kulea, na kukuza binti, alianza shule na kupewa mimba. Baba alianza kumlaumu mama kwa malezi mabaya kana kwamba ima yeye hakuwa na jukumu hili au mama alikuwa ima anamtunzia binti siri au akienda na binti huko alikopatia mimba. Wazazi mnapopata chagamoto kama hii, siri ya kwanza ni kuungana na kuikabili mkiwa kitu kimoja kwa sababu kama ni aibu au hasara inawakumba wote kwa usawa.
            Tuhitimishe. Changamoto za malezi haziepukiki na ni mambo ya kawaida. Hivyo, wazazi msifarakane kwa mambo ya mpito kwa vile hata hao watoto wanayo maisha yao.
Chanzo: Mwananchi J'pili leo.

No comments: