How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 16 January 2008

Kijiwe chalaani kufukuzwa Ballali peke yake

BAADA ya mkuu kuwaingiza mkenge Wadanganyika, kijiwe kimefanya kikao na kuja na azimio la ghafla kulaani kutupiwa changa la macho. Bila hofu tunatoa shinikizo BoT isafishwe pamoja na taasisi nyingine.

Mzee mzima nimewahi na kumkuta muuza kahawa peke yake akilalamikia maudhi ya mkewe. Analalamika tangu mafisadi waupeleke uchumi wetu ICU, mkewe anatishia kuondoka. Amechoka kulishwa mbwanda na bichwa la kambare.

Nikiwa nimechoka kusikiliza umbea wa muuza kahawa, mara Mgosi Machungi anatia timu akiwa anatafuna ubani.

Anaanza. "Mgosi umesikia ushanii wa Mkuu wa Kaya ya Kijiwe? Eti anamtimua Baai na kuwaacha wezi wengine, tena pae pae Benki Kuu! Mbona wae watoto wa vigogo hajagusia? Hii Kaya sina hamu Mgosi."

Wakati najiandaa kujibu naona na Mpemba anaingia akiwa anavuta tasbihi yake. Inaonekana hili la Dalaliii halimshughulishi kama Mgosi.

"Salaamaleko jamia," anasalimia Mpemba.

Tunajibu na Mgosi anaona kama wazo lake linapuuziwa. Anaamua kurejea ugani. "Ami naona unashughuika na mengine waa la Baai halikuhangaishi! Hawa makafii sijui walitilisha nini?"

Mpemba anajibu. "Weye waongelea usanii wa kutengua ulaji! Mie banki kuu nshaaitoa maana. Ile banki kuu au ya vigogo na watoto wao? Hata kule Zanzibar wevi watupu."

Wakati tukisukuti maneno ya Mgosi na Mpemba, Mbwa Mwitu anatia timu akiwa anaimba wimbo wake sijui kaunyaka wapi?

"Pokea chako kibomu,
Mkuu ninakutumia,
Hata ukinilaumu,
Siri zenu twazijua.

Kazi zao ufisadi
Jeuri ngebe na nongwa,
Baraka ya ukaidi,
Ukali ka’ embe gwagwa"
Mshenzi huyu hajali wala hasalimii anaendelea.

"Dalaliiii alijigamba
Kuwa morale i juu,
Sasa panga amelambwa,
Kakimbilia majuu"

Mara Kijiwe hakina hamu kwa umahiri wake wa kushusha mistari!

Makengeza anaamua kumkatisha kwa kumpa kipisi cha sigara ndipo anatuguna mic. "Wazee tusichukulie suala hili kijuujuu. Kwanza tujiulize kama kutengua au kufukuzwa kwa Dalaliii ndiyo jibu au ni kukwepa matatizo na kusogeza muda."


Kabla hajaendelea, Kapende anachomekea. "Huu ni ujanja hata kama wanakijiwe wameukwaa mkenge kiasi cha kumpongeza mkuu wa kijiwe ilhali naye na Dalaliii lao moja. Kwanini alichelewa na kuacha mambo yaharibike ndipo achukue hatua uchwara za kimazingaombwe?”

Akiwa anajiandaa kuendelea kutoa mapwenti, mara Mbwa Mwitu kamtimulia moshi sikioni kiasi cha kulikoroga.

"Jamani tulishasema hizi bange zitakuja kuwaweka pabaya. Inaonekana moshi wa bange zenu umeathiri wanakijiwe wote. Vinginevyo wasingekubali dhihaka na matusi haya. Ajabu wamehanikiza kama vyura kumpongeza!"

Mkurupukaji hangoji aendelee kutanua. Naye ana usongo. "Nyie mnajidanganya na hizi sanaa! Kwanza hata hao wakaguzi hawajagusa lolote zaidi ya kuja na dili ya kumtafutia Mkuu upenyo wa kujificha na kuwaficha wenzake. Hii Kaya bwana ni ya wajanja na walaji watupu kuanzia juu hadi chini."

Mzee Maneno hangoji. Anatia timu kavu kavu. "Kijana wajanja na walaji ni ndugu zako. Acheni kutukana watu mwajidai mna uchungu na kaya. Kama mnao mbona tunaishia kusema sema vijiweni bila kufanya kweli?"

Mkurupukaji hakubali kushindwa. Anaamua kumjibu mzee Maneno. "Mzee hata ukane na kuchukia, kaya yetu ni ya wajanja na walaji. Kama siyo basi sasa hivi tulianzishe uone kama hutakuwa wa kwanza kuufyata."

Mzee Maneno naye hakubali kushindwa. "Kulianzisha si tatizo hata ukitaka tuanze sasa hivi. Tatizo ni baadhi ya wenzetu kutusaliti. Chukulia mfano wazee wa virungu. Wao huamrishwa kama mbwa na kushambulia wasijue wanaowashambulia ni wenzao wanaoteseka kama wao!"

Baada ya kuona mjadala unaanza kupoteza mwelekeo, Msomi Mkatatamaa anaamua kuokoa jahazi.

Kutokana na mapwenti na kisomo chake, wahusika kuona anaanza kutia timu, wanaufyata.

Anasema. "Wazee hamna haja ya kutiana madole wala kutoana macho. Tukubaliane; wanakaya wana sehemu kubwa ya lawama kwa ukondoo wao. Hayo tuyaache."

Anakohoa na kuendelea. "Nitaongelea hili la usanii wa kijiwe chetu. Je, mbona ame-concentrate kwenye bilioni 133 ilhali zilizoporwa ni ziadi ya hizo? Mbona majina ya vigogo na makampuni yao hayatajwi badala yake tunatajiwa vikampuni vya misheni town?

“Mbona Chama Cha Namba One kilichonufaika na chumo hili la wizi hakitajwi au ni ule usanii wa wanufaika kuwatimua waliowanufaisha? Kufukuza Dalaliii siyo suluhu iwapo watoto wa vigogo wanaendelea kuiba." Anainua kombe lake la kahawa na kulipiga busu na kuendelea.

"Ukitaka kujua zimeibiwa ngapi jumlisha zote zilizotolewa kwenye takrima, zilizojenga mahekalu na zilizotoroshewa India na kwingineko ndiyo utajua Bongo inaibiwa kiasi gani.

“Zilizoibiwa ni zaidi ya upuuzi huu wa bilioni 133. Kwani siri? Ajabu wanakijiwe wanashikilia kumpongeza Mkuu bila kuangalia athari za kiuchumi na kijamii kutokana na ufisadi huu wa kitaasisi na kimfumo.

“Dokta Silaha aliturahisishia kazi kuwataja wahusika. Ametaja list of shame. Ametaja Deep Green Finance. Ametaja wahusika ambao bado wanazidi kutesa. Kwanza niwaulize. Zile kesi tulizosikia zingefunguliwa dhidi yake zimefia wapi? Je, huu siyo ushahidi kuwa wahusika ni mafisadi hata kama ni waheshimiwa?"

Akiwa anajiandaa kuendelea, Mzee Ndomo anauliza swali. "Msomi unataka kusema pesa iliyoibiwa ni kubwa kuliko tunayoambiwa, na wahusika ni zaidi ya hawa?"

Msomi anajibu. "Naam mzee wangu. Hebu jiulize takrima zilizotembezwa mwaka 2005 zilitoka wapi kama siyo huko? Je, tatizo la uchumi wetu ni Benki Kuu tu? Mbona wale wanaojulikana kusaini mikataba ya mabomu katika uwekezaji hawafanyiwi kama Dalaliii?

“Je, Dalaliii alikuwa peke yake? Mbona mwanzoni tuliambiwa wapingaji ni waongo na wasemayo ni uongo? Je, hapa muongo, tena mkubwa ni nani? Je, tutaendelea kuwaamini waongo hata kama ni wakubwa?

“Naona suluhu siyo kutengua bali kufukuza, kukamata, kutaifisha na kushitaki. Na siyo Dalaliii tu, bali wote wanaojulikana wakijijua kuwa ni mafisadi wakubwa hata kama ndiyo wanaojifanya askari wa kuwakamata mafisadi."

Mara mate yanampalia, anapiga chafya. Mara Mbwa Mwitu anachomekea kiutani. "Angalia mzee wasikukolimbe na kukumwagia tindikali. Maana kwa Bagamoyo si unawajua?"

Msomi ameishakuwa gado anaendelea. "Hapa hakuna cha Bagamoyo bali wanakijiwe kuondokana na ukondoo. Tutaendelea kuwa ngazi za mbweha na mafisi kupandia ilhali tunaumia?

“Kinachofanyika ni kudhalilishwa tena na wale tuliowapa dhamana zao. Suluhu si kukuna kipele bali kutumbua jipu. Je, Mkuu hakushiriki? Mbona nyumbani kwake wamejaa mapapa na manyangumi tu? Hata wasaidizi wake wote si safi hata kama ni marafiki zake.

“Hebu angalia Richmond, Buzwagi, AIPITIELO, mbona kila kitu hadharani? Mkuu asitutie madole machoni naye hafai ndiyo maana Babu wa Kuchonga alimkataa.

“Kwanza amrejeshe Dalaliii tumsulubu au anaogopa asitoboe siri na mzee mzima akaumbuka?"

Kijiwe kikiwa ndiyo kimenoga mara alikatiza kibaka aliyekuwa anafukuzwa na watu wenye hasira na umasikini, tukajiunga nao kumtia adabu kibaka huyooo.





Source: Tanzania Daima Jan, 16, 2008

2 comments:

Evarist Chahali said...

Nimepita hapa Mzee.Hizi kelele tunazopiga ipo siku zitazaa matunda.Ni suala la muda tu.

Anonymous said...

Thanks Evarist,
Muhimu ni kondoo wetu kuamka na kujua hili ni jukumu lao piga ua.
Mpayukaji