Matukio ya hivi karibuni ambapo msafara wa rais Jakaya Kikwete ulishambuliwa kwa mawe kwenye kijiji cha Kanga Mkwajuni, Chunya Mbeya si jambo jema ingawa lina somo kubwa tu.
Maana yake ni kwamba wananchi wamechoka baada ya kutoyaona maisha bora kwa wote aliyoahidi rais. Tutake tusitake kumekucha.
Vyombo vya dola vyaweza kutumika kuwakandamiza kuwatesa na kuwanyamazisha wananchi, ukweli unabaki pale pale. Mtatesa miili yao lakini siyo mawazo na roho zao. Umma umechoka baada ya kuvumilia kwa muda mrefu sana.
Mlizoea kuwaonea kama kondoo na kuku msijue hata njiwa pamoja na kuwakilisha amani hupigana. Nyakati zinabadilika kwa kasi ari na nguvu mpya.
Tukio la pili ni lile la rais wa chama cha walimu Tanzania, Adrian Mkoba, kama kibaka, kunusurika kibano limetoa somo na mwamko mpya.
Somo na mwamko huu vinapaswa kupaliliwa ili visambae kwenye kada nyingine kuhakikisha ukombozi wa kweli wa wafanyakazi unafikiwa wakati huu.
Licha ya kuwa jambo la faraja ni onyo kwa wakadamizaji na wanyonyaji kuwa wanyonywaji na wakandamizwaji sasa wamejitambua na wako tayari kabisa kuchukua hatua za kujikomboa bila kujali nani anawakandamiza.
Baada ya kuanza na zomea zomea kwa mawaziri waliokwenda mikoani nchi nzima kuwahadaa kwa kisingizio cha kuelezea bajeti, sasa, taratibu, umma umeanza kuhamasika na kuchukua hatua dhabiti na za uhakika za kujikomboa.
Umma umeanza kuwachapa wasaliti badala ya kuwanyamazia na kuwavumilia.
Tukio hili la kutaka kumchapa rais wa chama cha walimu kwa kuwahujumu kwa kusitisha mgomo wao, liwe somo kwa wote wenye kuuchukulia umma kama mataahira na wavivu wa kufikiri. Ni onyo kwa wote wakubwa kwa wadogo.
Laiti mwamko huu wa kupigiwa mfano ungeingizwa na kutekelezwa na wafanyakazi wote nchi nzima. Kwani hadi sasa hakuna ajuaye hatima ya mgomo wa wafanyakazi nchi nzima uliokuwa umeandaliwa na wafanyakazi wote lakini ukavurugwa na kuhujumiwa na katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi, TUCTA, Nestory Ngulla kwa kisingizio kuwa alifurahishwa na hotuba ya rais.
Ingawa wafanyakazi hawakutaka kumbana aeleze kuvutiwa na hotuba ya rais na maslahi ya wafanyakazi vinahusianaje na amepata wapi mamlaka ya kutumia hisia zake, kuna haja ya pande zote kujifunza.
Bila kujifunza, wanasiasa na wachumia tumbo wataendelea kuwatumia wafanyakazi kama vihongwe wao. Kuna haja ya kukata mikatale hii haraka na kwa kasi ya ajabu.
Alipoingia madarakani, kwa mfano, rais Jakaya Kikwete chini ya kauli mbiu yake, kasi mpya nguvu mpya na ari mpya aliwaahidi mengi watanzania hasa maisha bora kwa kila mtanzania. Yako wapi maisha bora na safari ya Kanani? Bila vitu hivi kupatikana hapatakalika wala kutawalika. Shime tukaze uzi.
Lakini kwa kadri siku ziendavyo, hakuna la maana lililokwisha kufanyika. Hakuna hata dalili. Ufisadi na umaskini vimezidi kuongezeka kwa kasi ya ajabu huku watuhumiwa wakiendelea kutanua kana kwamba walichofanya ni cha maana kwa umma!
Maisha bora kwa watanzania yamegeuka kitendawili tata kisicho na mteguzi. Rais ameendelea kuwazungusha watanzania kwa lugha tamu tamu huku maisha yao yakizidi kuwa shubiri.
Kuna haja ya watanzania kujitambua ili kujikomboa. Wanapaswa kuasi mfumo nyemelezi uliowachelewesha na kuwanyonya kwa muda mrefu.
Leo hakuna anayeshinikiza rais atomize ahadi zake. Sasa ni miaka zaidi ya miwili na hakuna kinachoonekana kuweza kufanyika. Je tatizo hapa ni nini zaidi ya kuwa wananchi wenyewe wanaoridhika na kunyamazia jinai hii?
Hakuna ubishi kuwa walimu sawa na wafanyakazi wengine wana hali ngumu kimaisha. Maslahi na mishahara yao ni vya kijungu jiko huku wanasiasa wakizidi kujiongezea marupurupu na kupunguza huduma kwa jamii. Wanajihudumia wao na familia zao badala ya umma walioapa kuuhudumia.
Mfumo wetu umechoka na kuchaa kiasi cha kukera na kuchosha. Wanasiasa wameshindwa kazi vibaya na umma umewaacha bila kuwawajibisha. Ajabu watu hawa hawa wasiowajika wanata wenzao wawajibike!
Watu wasiowajika kuwajibishana wala kukubali ushauri wa kufanya hivyo, bila hata chembe ya aibu, wanataka umma uwajibike!
Kichapo cha Mkoba ingawa amenusurika kiwe somo kwa wale waliokosea kudhani watanzania wataendelea kuwa makondoo na kuku wa kuchinjwa na kuibiwa mayai yao wakishuhudia. Wakati wa ukuku na ukondoo unazidi kuwapa mkono. Ni muhimu wakazingatia kuwa moto uliowashwa na ujasiri wa walimu si rahisi kuuzima.
Kama kuna watu wanahitaji kubadilika kujijua na kujikomboa haraka duniani basi si wengine; ni watanzania. Maana wanapostaafu ndiyo mambo yanazidi kuwa magumu. Rejea mateso ya zaidi ya miaka 30 wanayopata waliokuwa wafanyakazi wa jumuia ya Afrika ya Mashariki na wengine wengi ambao masahibu yao hayajaripotiwa.
Hivyo basi hakuna ukombozi halisi kama kuhakikisha wafanyakazi wanapigia kuondoa unyonyaji na mfumo unaowasababishia mateso zaidi wanapostaafu.
Ni vizuri kwa wafanyakazi wa sasa ambao ni wastaafu wa kesho kuandaa mazingira mazuri ya kustaafu wakiwa wanafanya kazi sasa. Wasipofanya hivyo, watakuwa sawa na vipofu wanaotumbukia shimoni wakati wana macho. Maana haya yanayowapata wenzao leo yatawapata wao kesho iwapo mfumo na taratibu ni zile zile.
Mazingira magumu ya kazi na ukosefu wa haki na stahiki za wafanyakazi umewatumbukiza hata kwenye rushwa ambayo watawala huiadhibu kwa ukali na adhabu kubwa ilhali wakifumbia macho uhalifu wao. Sasa wamegundua kuwa kula rushwa hakutawakomboa bali kujikomboa.
Manesi, walimu, polisi, mahakimu wa mahakama za mwanzo, makarani, na maafisa wengine wadogo wamekuwa wakikamatwa mara kwa mara kwa rushwa na kufukuzwa kazi pia kufungwa. Ajabu linapokuja suala la kushughulikia rushwa na jinai kubwa vya wakubwa hakuna anayeshughulikiwa!
Rejea kuendelea kutanua mitaani kwa watuhumiwa wa uchafu kama EPA, Richmond, IPTL, TICTS, TANESCO, Kiwira, ANBEN, Tanpower, Fosnik na madudu mengine mengi.
Kwa vile wahusika walizoea kuuchukulia umma na wafanyakazi kuwa mabwege kiasi cha kuwahujumu kuwapuuuza na kuwadanganya kila uchao, basi badala ya kuwanyamazia na kunung’unika au kuzomea tuanze kuwashikisha adabu.
Ingawa si vizuri kujichukulia sheria mikononi, inapofanyika hivyo kwa lengo la kujikomboa kijamii na kitaifa, si kosa tena. Maana sauti ya umma ni sauti ya Mungu. Hata mapinduzi na ukombozi wa wafanyakazi tunavyojivunia kama vile ya Ufaransa,Poland na kwingineko, vilifikiwa kwa njia hii ya kukataa ukondoo na ukuku na kuuvaa uchui na usimba.
Chanzo: Dira ya Tanzania Oktoba 21, 2008.