BAADA ya kuuawa - sorry kufa kwa Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, msimu wa uongo na kuomba kula kwa kusingiza kura umefika.
Vyama vyote vimeishajiandaa kutwaa ulaji huu ili kufaidi ruzuku za bure. Maana siku hizi kazi ya ubunge ni sawa na uchungaji au ushehe. Hawajibiki kwa mtu isipokuwa chama chake na tumbo lake kwa walio wengi.
Baada ya wahusika kupiga kipenga kuwa ulaji tayari uko mezani, mie nilivuta subira kupima maji na kusoma kanuni za mchezo.
Mie si mkurupukaji kama yule mchungaji mbwa mwitu aliyetwisha mimawe. Kwa ufupi ni kwamba jamaa alipopolewa kwa kupigwa kipopo. Kwa vile tunalazimika kueleza sera zetu, nami nitaeleza sera zangu ambazo ni kama ifuatavyo:
Sera ya kwanza ni kuwapakazia wale ninaoona kuwa wapinzani wangu hasa waliokuwa wakishikilia kiti cha Tarime.
Nitapakaza kuwa CHADEMA, walishiriki kwenye mauaji ya Wangwe. Nimeishanunua nyundo na kuipaka damu ya kuku kuthibitisha kuwa marehemu alipigwa nyundo na wauaji wake.
Sera ya pili ni kutembeza takrima. Wale wenye njaa ya khanga, matisheti, vibandiko na upuuzi mwingine wajiwahi.
Muhimu lazima wanipe kura ili nile. Pia natoa manywaji na makulaji bure. Watu wangu ameishatapakazwa kwenye kila baa, nyumba za kulala wageni hata kwenye ofisi za Chama Chetu cha Maulaji na Masanaa (CCMM).
Tatu, natoa mshiko kwa yeyote ambaye yuko tayari kuniuzia karatasi zake za kura ili nizifanyie kazi zinifae. Kura yako ni kula. Usilaze damu. Siyo siri. Tunanunua kura ili tupate kula.
Nne lazima tuibe kura kila tupatapo nafasi. Kama mtu akilaza damu tunaingiza kura zetu zilizokwishapigwa kabla ya kufungua vituo halafu wasipotugutukia tunapeta kitsunami tsunami.
Tano, nitawachochea wahuni wangu wawapige wale wanaoonekana kuwa tishio kwangu. Ila msichanganye mambo na kupigwa kwa yule Mchungaji uchwara. Yeye alitaka kuwahadaa akina Mura Kiki ohoya akidhani hawana akili wakamtia dispilini.
Nina mpango wa kuingiza Mungiki kutoka kwa mzee Moi ili waje watembeze kichapo na kufanya maangamizi nipate nafasi ya kusomba masanduku ya kura niondoke na ushindi.
Ushindi si mchezo lazima mbinu zote zitumike halali na haramu. Na isitoshe hii ndiyo asili ya ushindi wangu.
Sita kuhakikisha kuwa lazima chama chetu kinashinda, nimemwamuru katibu mkuu wa chama chetu bwana Yusufu Makombo, aende kumwaga fitina ili tupete kama hatuna akili nzuri.
Juzi nimemtuma hata waziri wangu wa kijiwe Bill Ngelanija akaacha kupambana na kuharibika kwa kibatari akaenda kusaka kula?
Juzi wanywa kahawa waliinywa kizani baada ya taa kuharibika na Bill Ngeranija hakuhangaika kuitengeneza bali kutimkia Ushashini kusaka kula.
Saba, lazima twende maeneo ya pale Kisii tuingize wapiga kura wa kulipwa kama tulivyowahi kufanya kule Zenj kabla ya CUF na CCM kutushinda.
Kama si kuwanasa watu wetu tuliokuwa tumewa-import toka bara mbona kingeeleweka na Kalumekenge asingekuwa anatesa kwa sasa.
Kabla sijasahau, sera yangu nyingine ni kujifanya nawapenda sana wajane na vitegemezi vya marehemu Wangwe ili nionekane najali nivune kura.
Pia nitajifanya nawapenda wana-Tarime kwa sana. Nitaingia kila nyumba na kusalimiana na kula na kunywa na kila mmoja.
Nane, nitakuwa nataniana na kusalimiana kwa kukumbatiana na kila ajaye ili waone ni mwenzao. Nikishapata kura nawaacha solemba wananchi na watoto wa marehemu kama jamaa alivyowafanyia jamaa na watoto wa Mulinge kule kwa kina Ole.
Na hili litafanikiwa. Kwanza nimeishapitia Bagamoyo kujiganga ukiachia mbali kuanza kutumia runinga yangu kuonyesha mauaji ya kimbari ya Rwanda.
Unajua picha za mauaji ya Rwanda? Huwa nyakati kama hizi za uchanguzi zinasaidia kuwatisha wadanganyika wasiojua dunia inavyokwenda. Hapa najua. Katibu mkuu mchovu wa chama changu ataongeza chumvi umbea na chachandu na waliwaji wataingia mkenge mchana.
Lazima niwaambie mimi ni mtu wa amani na nchi yangu lazima iwe ya amani tena kisiwa cha amani hata kama watu wanachunwa ngozi na mazeruzeru kuuawa kila uchao.
Nitawafunga kamba tu bila kujali. Maana huwezi kuwa na amani na ukajiita kisiwa cha amani kama wewe si chizi au tapeli wakati ufisadi unapanda chati na haki inakuwa bidhaa ya kuuza na kununua.
Tisa, nitakodisha bendi ya kwaya toka Uingereza waende kuwatumbuiza wana Tarime. Kama si kiranja wa bendi ya chama changu iitwayo Tuwahadae Original of Tanzia, kukumbwa na kashfa ya kula uchache wa wapaaza sauti wake, bila shaka ndiyo ingetia timu.
Pia kuna wimbo maarufu wa mchungaji mbwa mwitu wa kuwatisha wapiga kura. Mtamuona kwenye wimbo huo huyu mchungaji njaa akiwatisha watanzania kuwa damu zitamwangika, mabomu kulipuka na kuvurugu kutokea huku watoto na kina mama wakilia bila kusahau wazee na walemavu.
Hii ikichangiwa na magazeti ya chama chetu na yale ya jamaa zetu wanaosingiziwa ufisadi lazima tushinde. Tutazidi na kuwanunua makanjanja wenye roho kama ya mbwa ili watupambe na kutupigia debe kwa sana ili wapiga kura waingie mkenge mchana kweupe.
Hapa bado hatujatumia runinga na redio za chama. Sisi lazima tushinde. Maana tuna kila nyenzo za maangamizi linapokuja suala la kusaka ushindi hata kama ni kwa bao la kisigino.
Leo sitasema mengi kwa vile nakwenda kuandaa mipango ya kuibuka na ushindi wa Kitsunami. Isitoshe sitaki niwape faida wabaya wangu wasije wakaniibia mbinu wakaondoka na ushindi wangu.
Msinione kama sina shukrani. Kwa vile wameanza wenyewe kuufanya uchaguzi wa kijimbo kimoja kuwa kama wa taifa lazima nami nitumie kila nguvu na mikakati kuhakikisha napaa na ushindi ili niende bungeni kula mshiko wa bure.
Kabla ya kusahau, kwa vile nina ugonjwa wa malale na kusahau, nikifika bungeni nalala na kupayuka kama sina akili nzuri. Nitahakikisha mwaka huu Osama bin Laden anakamatwa.
Pia nitahakikisha Tanzania inapeleka wanasayansi mwezini ili kuonyesha maisha bora yanavyowezekana kwa kila Mtanzania. Tutapandisha bendera ya taifa kule ili isimame bega kwa bega na ile ya kwa Joji Kichaka na ulimwengu utatutambua sisi ni nani.
Kila la heri tukutane Tarime. Ila nawaonya wana-Tarime. Mimi siyo yule mchungaji mbwa mwitu kidhabu wa vidhabu. Mimi ni mwanasiasa wa karne.
Chanzo:Tanzania Daima Oktoba 8, 2008.
No comments:
Post a Comment