The Chant of Savant

Wednesday 1 October 2008

Siku Mpayukaji aliposhuhudia kuanguka kwa Mbeki

KUTOKANA na jitihada zangu za kutaka kum-recall jamaa huko tuendako, genge la mapinduzi la chama tawala cha Afrika Kusini, African National Congress (ANC), lilinialika kwenye kigwena cha kumtimua shujaa Thabo Mvuyelwa Govan Mbeki.

Kwanza, hawakujua kuwa Mbeki ni rafiki yangu damu damu kwa vile wote tuna misimamo inayofanana ya kutojikomba kwenye vijiwe wala kuvitumia kubakia kwenye ulaji hata kama hatufai. Sisi ni kanga si kuku. Sisi ni waasi wa kuzaliwa.

Ingawa sikuunga mkono mpango mzima kutokana na uchafu wake, sikuwa na jinsi. Nilihudhuria ili kujifunza mbinu za kum-recall jamaa.

Siku cheka cheka bali kuwa makini. Ingawa uliofanyika ni uhuni kutokana na kufanywa mtu asiyefaa, nilitamani uhuni huu ungefanyika kayani.

Sikumpenda Jacob Zuma, kutokana na kupenda vimwana na kujilimbikizia mimali ya wizi. Ningempendaje mtu Chitalila na Kihiyo, achia mbali fisadi!

Kilichonifanya nimsikitikie Komrade Mbeki ni ukweli kuwa alifukuzwa kwa fitina na tamaa ya madaraka. Alifukuzwa na watu wachafu, tena vibaka waliopaswa kuozea lupango.

Hakuwa fisadi wala hakuwalinda wala kuwakopesha mafisadi. Alifufua uchumi wa Bondeni. Ameacha waswahili kibao wenye jeuri ya pesa tena halali. Ila binadamu hana shukrani.

Nilihudhuria kwa moyo mzito nikijua historia itaweka sawa mambo. Kwani nafahamu Zuma hana lolote kama jamaa yetu. Yake ni kiu na uchoyo wa madaraka. Laiti Mchonga angekuwa hai angeonya. Ogopa watu wanaokimbilia ikulu. Wanakimbilia nini iwapo hakuna biashara huko? Tuliishawaona waliokimbilia huko wakapageuza pango la wevi wa kigabacholi kuimaliza kaya.

Ingawa kilichojiri ni machukizo, kuna somo kwa wapambanaji kama mimi. Nimejifunza kuwa taifa siku zote lazima lije kwanza na chama baadaye.

Maana kuendekeza vyama kumesababisha magenge ya majambazi na mafisadi wajiitao chama kuziteka nyara kaya zetu. Kwa Mbeki hii ilitimia. Ila kwa Zuma na genge lake ilikuwa ni Zuma kwanza taifa mwisho.

Kweli wahenga walisema, kwenye miti hakuna wajenzi na kwenye wajenzi hakuna miti. Kilichotokea Bondeni hakikupaswa kutokea huko bali kayani. Wakati mtu akihangaika kuokoa maisha yake hospitalini hadi kuuawa na vichaa pale Mwihimbili, wapo watu wanajinyonga!

Kaya inahitaji kuwa-recall vibaka wetu waliojificha nyuma ya ushindi wa kitsunami uliogeuka kiama chetu.

Komrade Mbeki hajawahi kutajwa kwenye aina yoyote ya ufisadi. Haijui wala kuikingia kifua EPA, Richmonduli, Ticks, IPTL wala dawa za kulevya.

Hakufanya hivyo kwa vile si tick au kupe wala mlevi wa madaraka. Hata alipolazimishwa kukitoa hakupinga, bali kuachia akiwaachia mtego Wabondeni wajionee walivyoingizwa mkenge kama Kayani.

Hakuwa na waziri hata mmoja wala aliyewahi kuwa waziri mwenye kitegemezi kilichoghushi vyeti kuajiriwa kwenye benki kuu ya ulaji.

Hakuwa na mbunge hata mmoja aliyewahi kughushi vyeti na kuwadanganya wapiga kura kama jamaa yangu Chitaahira wa Kihiyo. Hata mkewe shemeji Zenele hakuwa na NGO za ujambazi kama nohino na Salama wake au Dungong Tunituni wa Makapi na Annae Tamaa wake.

Mbeki na mke wake walijua kuwa madaraka ni ya watu. Maana ilisemwa; Cheo ni dhamana, ingawa wenzetu wanakifanya kuwa cha maana wakati wao hawana maana wala muamana.

Wala hakukiongoza chama wala nchi kujichotea mabilioni ya Rand. Wala maskini Mbeki hakuchaguliwa kutokana na nguvu ya takrima. Hakuwa mbabaishaji ukiachia mbali kupenda kufanya ziara nje.

Hata hivyo alifanya hivyo kwa sababu za msingi si za kuokoteza kama za jamaa na kimwana wake waendao kujirusha na kushangaa shangaa ukiachia mbali kuejoi mipigo ya akina Boyz II Men.

Mbeki, alikataa utumwa wa chama. Alikataa kukumbatia mafisadi na wezi ili aendelee kuwa madarakani. Yeye ni mbwa mwitu, si mbwa. Ni kanga si kuku kama jamaa zetu.

Pamoja na machungu yaliyompata Komrade Mbeki alinipa wosia niwaletee. Msikubali chama kiwaburuze kwenda kuzimu. Wala msikubali wanaojificha kwenye chama wawapeleke kuzimu. Wapelekeni wao kabla hawajawapeleka. Heri nusu shari kuliko shari kamili.

Mbeki, anaacha nyuma kundi la kati la Waafrika wenye uchumi mzuri. Kwa kitaalamu huitwa “Middle class”. Hajaacha kundi la magabacholi na wawekezaji uchwara wanaoendesha nchi yake wakati ni mamluki wa kiuchumi.

Hakuacha nyuma serikali inayotegemea misaada ya makombo ya wezi wa kigeni wajiitao wawekezaji wakati ni wachukuaji. Haachi nyuma mbweha na fisi wakaao nyuma ya wanaojiita wakubwa na waheshimiwa wakati ni wenye ubongo mdogo na wanaostahili kudharauliwa hata na mbwa wetu.

Ingawa ANC itagawanyika kutokana na kondoo kujitofautisha na mbwa, ina kila sababu ya kuacha somo. Somo lenyewe ni kuwa hakuna haja ya kung’ang’ania genge la wezi. Maana kama alivyosema mzee Musa, genge si wazazi wako.

Mbeki anatuachia somo kuwa ipo haja ya kujiamini na kutenda mema badala ya kutegemea mitandao na upuuzi mwingine unaowaumiza wananchi.

Kinachofurahisha kwa Komrade Mbeki ni ukweli kuwa alishiriki kwenye mapambano ya kuikomboa Bondeni. Yeye si mdandizi wala nyemelezi wala kupe aliyeibuka kutokana na umaarufu uchwara kama Zuma.

Yeye ni msomi kuliko huyo Joyce wowowo mpenda sifa asiye na sera wala nyimbo, bali sanaa na wizi wa mchana. Kwa ufupi naachia hapa. Nina machungu na hasira Mungu anajua. Acha niende pembeni kuombolezea taifa la Bondeni kama ambavyo nimekuwa nikiimboleza Danganyika.

Habari njema, yule mbwa mwitu ajiitaye mchungaji Kris Mtukula alibondwa juzi kutokana na uzabizabina na umbea wake. Hakujua kuwa wadanganyika wanaanza kujitambua na kuamka. Ndiyo. Wanaanza kuchenjiana kama alivyowahi kusema Arawa. God bless Africa and God bless Danganyika.

Habari nyingine njema ni kwamba yule changu wa maadili na kanjanja Deomatusi Balila, amepigwa teke na mafisadi. Tulimuonya kujikomba na kutumia ni vibaya, akatuona wabaya. Hakujua maskini kuwa mafisadi hawana tofauti na fisi.

Huyo si wa kulilia bali kumuombea azidi kudhalilika na uchafu wake kufunuka. Ya Yusufa Mahanji kuwa kichocheo cha uchumi wetu wakati ni jizi, mmeyasikia.

Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 1, 2008.

No comments: