The Chant of Savant

Wednesday 22 October 2008

Kumbe na mawe yanasema!

BAADA ya kubwagwa, kuambulia kapa na kupata aibu kule Ukuryani, niliamua kuikimbia zomea zomea ya Dar es salaam. Ingawa niliendelea kuchekacheka kama kawa, moyoni nilikuwa natukutua ajuaye Mungu.

Wakurya eti wanasema walistukia sera zangu za uongo, vitisho, uchonganishi na ahadi uchwara kiasi cha kusambaratisha chama changu. Ila nitawakomesha kwa kuhakikisha maendeleo hayawafikii ili wajutie kosa la kutochagua chama dume.

Nilitinga zangu Mwakaleli kwa washikaji zangu akina Mulla, Mwakabangaiza na Mwakatafunwa lau nitulize mavune, kukimbia aibu na kuwakoga waliwa wangu. Nilikwenda kule kukagua maendeleo ya mradi wa kupambana na uchunaji wa ngozi baada ya kufanikiwa kukomesha mauaji ya mazeruzeru.

Pia nilikuwa na ziara kibinafsi kwenye mgodi wa kuchimba mawe wa Kiwira unaomilikiwa na washirika zangu Tunituni na Jona. Nilitaka kukagua maendeleo yake baada ya kuunusuru kuumbuliwa kwenye kijiwe cha Idodomya. Si waheshimiwa uchwara walitaka eti watajwe wanaomiliki nyenzo hii! Bahati nzuri waziri wangu kivuli, ngosha Bill Ngeranija aliwalamba chenga na kuwatuliza hadi sasa wamesahau. Hatajwi mtu hata kama mnamjua.

Mwakaleli hakuna magazeti ya udaku ya kuongeza chumvi na kupiga chuku jinsi tulivyobwagwa Ukuryani pamoja na kuweka nguvu zetu zote. Hata hivyo, gazeti moja lilishapigwa panga tokana na kuandika uchochezi kuwa washikaji wa mkuu walikuwa na mpango wa kumnyima ulaji mwaka 200100.

Inaonekana walevi hawajui sanaa. Nani amnyime ulaji iwapo yeye aliwapa ulaji wengine wakala hata bila kunawa kiasi cha kujisababishia matatizo kama jizi Luwasha wa Ewassa wa EPA na Richmonduli.

Nilimwacha Katibu mkuu wa Chama Cha Maulaji na Mafisidunia (CCM), Yusufu Makombo (Mgosi Machungi wa Mtibwa) abebe aibu zetu. Maana ndiye alijitia kilanga kwenda kuwachonganisha watu asijue wanajua janja yetu. Inaonekana walevi wameishamchoka kwa makombo ya mawazo yake na ngonjera zake uchwara. Nasikia jamaa zangu niliowaacha kule waliamua kuondoka usiku kama wachawi baada ya kunusa habari kuwa tulipigwa bao la kisigino. Ila elewa inauma hakuna mfano. Maana ukizoea kuchinja inapofika zamu yako kuliwa we acha tu!

Nikiwa najidai kwenye misafara yangu ya kifalme bila kujali uhaba na ughali wa mafuta kama mfalme wa Saudia niliwapungia mikono na kuwachekea kinafiki walevi wajue nipo kwenye ulaji kwa ajili yao ingawa siyo. Kuna walevi walikuwa wakiuliza mantiki ya mimi kutesa hivi ilhali kaya yenyewe ombaomba. Bila hili wala lile, si mishangingi yangu niliyoazima kwa washikaji zangu yalianza kupopolewa utadhani mi kibaka!

Sikujua waliwa wameishanichoka kiasi cha kuamua kunitolea uvivu kwa kunipopoa kama jizi! Wala sikujua kuwa njiwa ingawa huwakilisha amani nao hupigana huku mawe yakisema!

Lakini ngoja nitawakomesha. Kwanza niliishawaamrisha mbwa wangu wawatafune wote waliofanya makufuru haya. Pia nitaamrisha fisi niliowafuga wafungie makaratasi yote ya umbea yatakayoniandika vibaya. Ah naota! Nitawezaje yote haya wakati sijapewa kura ili nile kama jamaa?

Ajabu hii ilitokea wakati mkuu wa chama cha wafa na vumbi la chaki, Adriyani Mikoba, aliponusurika kunyotolewa roho. Unajua mke wangu ni mwalimu wa vidudu? Ingawa ana ulaji wake na NGO yake ya Maualaji ya Wake za Wakubwa (MAWAWA) niliyomuundia kuibia kahawa na kashata za kijiwe. Huwa nawazuga wafa na chaki kuwa ni mmoja wao.

Kwanza niseme. Unajua CHADEMA waliiba kura? Inasemekana walikwenda Bagamoyo kwa kigagula akawapa dawa ya kupendwa kuliko sisi. Wasiponiambia siri ya ushindi wao nitaanza kuwapakazia kuwa wanaua zeruzeru na kutumia viungo vyao kushinda viti vya ulaji. Haiwezekani wakishinde chama changu kilichowaahidi matanuzi wanakaya.

CHADEMA kweli wanapaa japo nilidhani wanadema! Eti wanasema niliwaahidi wana kaya pepo nikawaelekeza motoni! Wapuuzi kweli. Nani anaweza kuendesha kaya bila kudanganya? Nani amewahi kuchumbia bila kuongopa ili mchumba amkubali? Lazima useme mimi ni mshirika wa Bill Gate na huwa namkopesha Warren Buffet na nina akaunti kwenye Benki ya Dunia.

Inaonekana walevi wameanza kustuka. Yaani mnapopoa msafara wa mkuu mtarajiwa kama mimi; tena kama kibaka bila aibu? Ni wapi nilikosea? Kumbe hata kondoo na kuku wanaweza kuwa hatari kwa wezi wao!

Waliwa hawana shukrani. Hawajui nilivyokuza uchumi wa kijiwe kama mkuu. Alianzisha miradi kamambe kama EPA au Elewa Pata Ahueni (kupitia benki karimu). Kuna miradi kama IPTL (Itumikie na Pambania Tanzia Leo), ANBEN (Ajutaye Nami Baadaye Ende Nonihino-Motoni),CCM (Chukua Chako Mapema) na mingine mengi ambayo ipo hapa na peponi tu.

Hivi walevi na wafa na vumbi wameingiwa na nini? Au wamesikia umbea wa wapinzani kuwa tuliwahadaa tungewapa kahawa safi badala ya shubiri ya sasa? Wako wanaoouliza wapi kahawa yenye maziwa na asali wajihisi wako Kanani.

Wapo wanaoouliza kwa nini hatuwanyongi akina Mbwa Mwitu waliowaibia kashata na kahawa. Wanadai wamechoshwa kuona wakiendelea kunywa kahawa na kujimwagia wakati wao hata tone hawapewi. Wanaosema sisi ni mafisadi na wala rushwa hawajatulia,ebo! Yaani kunywa kahawa na kula kashata kiduchu kweli ni dhambi namna hii?

Juzi niliwasikia wambea wakihoji kwa nini tunawaadhibu watoto wanapodokoa kashata moja wakati tunavumiliana sisi wakubwa tunapoiba sinia zima la kababu!

Nilisoma kwenye karatasi fulani la umbea kuwa baada ya mie kupopolewa, kuna uwezekano maswahiba zangu akina Eddie Luwasha Ewassa, Enderea Chenga, Niziro Kadamage, Nistori Nuguri, Ben Tunituni Makapu, Annae Tamaa, Yusufu Makombo, Joji Mkunjika na wengine wanaweza kuchomwa moto au kuchunwa ngozi!

Eti kuna vichaa wanapendekeza maofisi yote ya washirika na mashirika yanayodaiwa kuibia kijiwe yatiwe nari! Hivi hawa walevi wa kahawa nani amewaloga kiasi cha kuchetuka hivi? Wanataka sisi na washirika wetu tule polisi? Hawajui kuwa wajinga ndiyo waliowao?

Kwa vile mimi ni bingwa wa mikakati, lazima hawa wafa na vumbi wanyolewe na wembe uliowanyoa wenzao waliotaka kugoma. Au niwabwagie bonge la hotuba liwakune wakome; ila hili haliwezi kufanikiwa. Maana kiranja wao ameishapopolewa; hana uwezo wa kuwazuga kuwa hotuba yangu imemkuna kiasi cha kusitisha migomo kaya nzima. Ila kipindi hiki inabidi niwe makini. Maana mambo si mambo wameanza kustuka. Kumbe hata mawe wakati mwingine yanaweza kusema tena yakaeleweka? Tieni akilini wenye akili. Achana na business as usual mambo yamebadilika.

Tukutane wiki ijayo.
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 22, 2008.

No comments: