The Chant of Savant

Wednesday 29 October 2008

Sikuadhimisha miaka tisa ya Nyerere

INGAWA wenzangu wengi walimfanyia kitu mbaya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuadhimisha miaka tisa ya kufariki kwake, mie roho ilinisuta.

Kusema ule ukweli mimi na mke wangu, hatukuadhimisha siku hiyo. Roho zilituuma kwa vile tulivyo mafisadi. Kuna kipindi nilitaka nijitoe kimasomaso nimtume Bi. Mkubwa aende kumfariji mama Maria.

Lakini roho ilinizuia baada ya kugundua kuwa Maria hakuwa na NGO ya ulaji ya Wake wa Wakubwa na Matanuzi (WAWAMA). Wala mumewe hakuwa tapeli, jizi na fisadi kama mimi. Hivyo niliachana na unafiki huo.

Kitu kingine kilichonisibu nisifanye hivyo ni kuona kuwa chama changu kilipigiwa teke huko huko Musoma kutokana na sumu aliyoacha Mwalimu.

Kitu kingine kilichonizuia kuadhimisha siku ya kufariki kwa Mwalimu ni ukweli kuwa nilikuwa nikitafuta jinsi ya kuepusha uso wangu kwenye kashfa ya Elewa Paka Anadokoa (EPA) ambamo washikaji zangu kibao wanashutumiwa tena kwa ushahidi wa wazi, kuibia kijiwe kahawa na kashata.

Ingawa nami niliwatumia akina Mbwa Mwitu na mgosi Machungi kuiba na kufaidi kashata na kahawa za kijiwe hasa nilizowahonga wanakijiwe wanichague, sijatajwa moja kwa moja ingawa mazingira yanaonyesha nilivyoshiriki.

Nyuma ya pazia siku hiyo nilikuwa bize nikitafuta bangusilo au mbuzi wa shughuli wa kusaidia kuficha aibu zetu. Lazima niwatoe watu kafara ili walevi wajue kuwa sasa nafanya kweli wakati ni mahepe matupu!

Ili kuhakikisha walevi hawazinduki usingizini lazima niwaite waandishi wa habari na kukitangazia kijiwe kuwa msione watu hawaonekani mitaani, wako Lupango wakisota baada ya tume yangu kuwakamata na kuwasulubu.

Tutawafungulia mashitaka vidokozi uchwara huku mapapa tukitesa. Hapa washikaji zangu hasa akina Kanji, Jitu na Chande watarejeshwa kwao Ugabacholini ili walevi waamini wako Lupango. Kumbe hola!

Kwa wale washirika zangu wa karibu nitaendelea kula pini hata kama wambea watashika bango vipi. Mimi sijibu. Najifanya kama sisikii wala sipo.

Pia lazima niandae vitu vya kuwapoteza maboya kama kutangaza mikakati kamambe na kuzidi kujichimbia ughaibuni ili muda uishe niwaache solemba. Haya tuyaache. Watayaona walevi wenyewe wakati wake ukifika.

Kitu kingine kilichonifanya nisipoteze muda wangu kumkumbuka Nyerere ni ukweli kuwa Mwalimu alinizuia kugombea ulaji kwenye anga za juu za Kijiwe alipogundua kuwa nilikuwa na kampani na vibaka walioibia nchi mafweza kibao na kujilimbikizia utajiri wa kutisha wakati ni watoto wa makapuku. Alijua akili zangu hazinitoshi.

Nisingejielewa wala kueleweka kuadhimisha siku ya mtu niliyemchukia na kumuangusha vibaya. Yeye alipenda nchi. Mimi nakichukia kijiwe. Nakipenda kukitumia kama shamba langu na washikaji wangu tunaoshirikiana nao kuwaliza walevi.

Kitu kingine kilichonikera nusu nipasuke ni ukweli kuwa siku chache baada ya walevi kuadhimisha kumbukumbu ya Mwalimu walilewa sumu yake kiasi cha kutishia kunitoa roho nilipokuwa nikijivinjari na washirika zangu mitaa ya Chunya pale Ilala.

Si washenzi walirushia mawe msafara wangu wa baiskeli wakati tukisherehekea matanuzi na makamuzi baada ya kutokuwapo Mwalimu.

Unajua paka akiondoka mipanya hujitawala. Baada ya Mwalimu kuondoka tumepata nafasi ya kujinafasi bila woga wala hakuna mtu wa kutuwekea kauzibe.

Kitu kingine kilichofanya nisipoteze muda adhimu kumkumbuka mtu ambaye alinizuia ulaji ni ile hali kuwa nilikuwa nikitafakari wapi pa kwenda kutanua kwenye ziara ughaibuni. Bi Mkubwa alikuwa ametishia kunivisha gauni kama nisingetengeneza ziara ya haraka haraka ili akakague akaunti zake huko.

Kitu kingine kilichonifanya nisiadhimishe kifo cha Mwalimu ni ukweli kuwa wanoko wangeniuliza ni jinsi gani namuenzi iwapo hata kusimamia kahawa na kashata za kijiwe nimeshindwa. Sijui ningekuwa naongoza nchi kama yeye ingekuwaje Yarabi?

Wakati walevi wakiadhimisha kifo cha Mwalimu nilikuwa natafakari jinsi ya kupanua ulaji wangu ambao unaonekana kuanza kuingia mchanga baada ya wambea kunishupalia kuwa mimi ni fisadi.
Huwa nawashangaa hawa wambea. Kama mimi fisadi kwa nini mnataka nipambane na mafisadi? Nani alimuona panya akikimbiza mkia wake ili autafune?


Huwa nawashangaa walevi. Iwapo mimi ni fisadi nanyi sio kwa nini mnanivumilia? Msingekuwa mafisadi msingekunywa kahawa na kula kashata nilizowahonga wakati nikigombea ukuu wa Kijiwe. Ambaye hakula kashata wala kunywa kahawa ajitokeze nimuone. Senzi nyie.

Mie ni mjanja Bwana! Nahonga walevi hata mbwa wao. Nahonga hata miti maziwa na bahari. Vyote vinaimba utukufu wangu ingawa wachache wameanza kunistukia kiasi cha kunivurumishia mimawe kama kibaka.

Walevi ni watu wenye akili zilizolewa na zisizoelewa. Eti wapo wanaodai kuna siku nitauza hata deli la kupikia kahawa! Niliuze mara ngapi iwapo na Kijiwe niliishamuuzia Kanji?

Mbona wanachekesha. Walitaka niwe kama Mwalimu ambaye alikalia madini akaacha kuyaendeleza kama yanavyoendelezwa kwa sasa kupitia uwekezaji wa ‘tajiri kapagawa anagawa bure’?

Hivi walitaka niwe kama Mwalimu aliyekuwa tayari kufa maskini wakati alimilki nchi yenye utajiri lukuki? Lazima ninywe kahawa na kulewa huku nikila kashata na kuvimbiwa.
Jambo moja tunakubaliana kuwa Mwalimu alikuwa kidume, nami kidume. Unadhani ni mchezo kuwaweka sawa walevi ukiwapa maji yaliyochanganywa na mabaki ya kahawa huku mwenyewe nikinywa kahawa yenye maziwa?


Mwalimu alikuwa na siasa za ujamaa. Mimi zangu ni za uhujumaa na ufisudaa. Wenye husda wajinyonge. Kwanza ngoja nitoe tafsiri ya siasa zangu za uhujumaa.
Uhujumaa ni mfumo wa maisha ambapo kila mtu anaishi peponi kwa imani siyo matendo. Pia Uhujumaa ni mfumo wa kupambana na ujamaa.


Si kwamba mfumo huu unashindwa kufanya vitu hivi vionekane hapa duniani. Kwa vile mtu anapokufa anaishi maisha marefu kuliko akiwa hai, mfumo huu huwandaa watu kuishi maisha ya raha baada ya kufariki. Huchukua miaka kama kumi hivi watu kuelewa somo.
Katika mfumo wa Uhujumaa watu huishi kama familia wakiongozwa na kiongozi aliyechaguliwa na Mungu. Kiongozi ambaye hakosei wala kuchukia.


Ni mfumo bora wa maisha kuliko mifumo yote iliyowahi na itakayokuwapo dunia. Mfumo huu husisitiza amani hata kama kuna mateso na hujuma. Hivi hutumika kuwapima na kuwaandaa kwa ajili ya maisha ya raha hapo baadaye.

Mwalimu alisomesha watu bure. Sisi hatuwapi watu kahawa bure. Lazima wateseke hapa duniani ili wakifika huko wastarehe. Kweli mimi nilisoma bure hadi nikawa na ujanja wa kufika hapa kwenye ukuu.

Lakini walevi hawahitaji elimu zaidi ya ahadi. Hivyo katika mfumo wetu ahadi ni bora kuliko mali na elimu. Ndiyo maana tunahimiza zifunguliwe Glosari nyingi kuliko mashule na mahospitali.
Hebu kwanza tuachane na kumbukumbu za Mwalimu. Mna habari kuwa siku chache zijazo nitaishangaza dunia kwa kutangaza vita hasa ya kuwakamata mafisadi wote wa kahawa na kashata Kayani?


Waliokuwa wakisema mimi ni lame duck wataibika wenyewe. Hakuna haja ya kutoana roho. Ngojeni mjionee wenyewe mambo na siyo mazingaombwe na sanaa kama wabaya na wachonganishi walivyozoea kusema.

Tukutane Kanani kwenye nchi ya maziwa na asali kwa ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya. Mambo ndiyo yanaanza. Tia akilini. Mwalimu wangu usinibaini. Wajinga ndiyo waliowao nikipata kumi tano zako. Amina.
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 29, 2008.

No comments: