The Chant of Savant

Wednesday 15 October 2008

Tarime na siasa za kunyonga mbwa!

NIKIWA kijijini Kuruya baada ya kutoka Komge, nilipata habari kuwa kuna mbwa aliuawa baada ya kupokea takrima ya T-Shirt kutoka kwa wabaya wangu.

Huenda hata kibandiko alipewa. Sema hakuwa na chogo la kukiweka. Hayo tuyaache.
Haraka haraka nilimpigia simu mshirika wangu Mgosi Machungi kujua kama aliyekuwa amekamatwa na kuuawa ni mbwa wangu kipenzi aitwaye Chatu Chunga Mbwa Teule au (CCMT) kama wahuni wapendavyo kumuita kwa kifupi hasa pale kijiweni.
Mgosi Machungi hakusita. Alifanya utafiti haraka haraka kwa kuwasiliana na shemeji yake mama Ndiza kuhakikisha kujua ukweli ni upi. Kumbe mbwa wangu alikuwa hai akitanua kwenye mitaa ya Tarime down town.

Ushingae kuona mbwa wangu naye yuko Tarime. Nyumba nzima tumehamia Tarime hata paka nao tumewaleta kuhakikisha tunatoka kidedea.

Kaya nzima ipo Tarime. Hata mimi mkuu mwenyewe ndiyo nimetoka zangu ziarani sehemu sehemu na kutia timu huku Ukuryani.

Bahati yao aliyeuawa si mbwa wangu vinginevyo kingeeleweka. Kwanza sikuamini kuwa watu wazima na akili zao wangemuonea mbwa badala ya kupambana na ufisadi na siasa zao nyemelezi na babaishi za kisanii au hata huyo aliyetoa takrima iliyosababisha kifo cha mbwa huyu asiye na hatia.

Kwani huyo mbwa hiyo T-Shirt aliyokuwa ametinga alimuibia mtu? Mbona mbwa ni bora kwa kuvaa kama binadamu kuliko binadamu kuuvaa mbwa na kufanya umbwa kwa kuendekeza tamaa kiasi cha kaya kuliwa tena mbichi!

Badala ya kumuua mbwa yule ilibidi wampende. Kwanza alikuwa ni mpenzi na shabiki wa chama chao. Kwani hizo nguo walitoa za nini kama siyo kutaka zivaliwe ili kujitangaza?
Je, fulana hiyo angeivaa simba au nyati naye wangemuua au kumuonea fahari? Tujalie angeivaa jogoo. Usingesita kusikia wakijisifu wao majogoo wasijue hata mbwa ni kiumbe na anaweza kuwakilisha watu fulani.

Hizi siasa za mbwa zitatufikisha pabaya. Baada ya kuinyaka hii rafiki yangu Kapende alinitwangia akisema eti nisihangaike na mbwa bali niache siasa za mbwa kwa walio wao!
Ni kweli. Hivi mbwa aliyevaa fulana ya chama na fisadi anayejivisha utukufu wakati ni mchafu nani mbaya wa kustahili kunyongwa? Imenikumbusha kisa cha marehemu Immigration kule Sumbawanga.

Kwanini tunaigeuza kaya kuwa ya mbwa hadi tunawaonea mbwa? Najiuliza kama mbwa wa Tarime angevaa fulana ya chama changu (CCMT) na si za CCM, angeuawa kweli? Hivi siku watakapojua kuwa mbwa wangu anaitwa CCMT ingawa hana uhusiano na CCM yao watamfanya nini?

Yaani tumekuwa wa hovyo na katili hivi? Acheni uvivu wa kufikiri jamani. Shughulikieni mafisadi waliotamalaki kila sehemu ikiwamo siasa.

Ingawa marehemu mbwa alivaa fulana, ameondoka bila kufanya ufisadi wowote hata kukamata kuku wa mtu. Kama kuvaa fulana ilikuwa dhambi mbona zinavaliwa na kutolewa na mafisadi kibao?

Kwa nini kupotosha watu na kuonea wanyama badala ya kushughulikia sera? Dalili za kuishiwa kiakili ni ukatili hata kwa wanyama badala ya kuwalinda.

Nao wana haki. Kitendo cha Tarime kinaonyesha tulivyo na vipaumbele vya hovyo. Tunafanya mambo ya hovyo kuwa ya maana na ya maana kuwa ya hovyo!

Wameona fitina hazitoshi sasa wanaanza hata kuua wanyama mahuluku wasiojua hata kinachoendelea! Ni kuishiwa kiasi gani?

Mbona hatushughuliki kuelezea tunavyoshindwa kusimamia rasilimali zetu? Mbona hatushughulikii na ufisadi na ujambazi mwingine na jinsi ya kujikomboa na uwekezaji nyemelezi na wa kijambazi?

Mbona hatuelezi jinsi ya kuwashughulikia watawala kutuibia na kujilimbikizia mali za wizi? Mbona hatuwanyongi Richmond, EPA, TICT, IPTL na uoza mwingine uliosababishwa na watawala wetu?

Mbona hatunyongi walionyonga miiko ya uongozi aliyoiacha Mwalimu kikundi cha wahuni fulani kikaisambaratisha? Mbona hatuwanyongi aliowatuhumu Nape Nauye wala mitandao uchwara iliyozagaa kwenye chama kinachojiita mkombozi wakati ni muuaji wa uchumi na maendeleo yetu?

Je, hawa wanaojulikana kwa ujambazi na ulafi wao na maskini mbwa, nani mbaya kwa taifa?
Mbona hatuwanyongi wanaowakadamimza vijana akina mama na watoto wala mauaji ya mazeruzeru na vikongwe bila kusahau mauaji ya uchumi wetu?

Tushughulikie kutokuwapo usalama kwenye mipaka yetu kiasi cha kuruhusu magenge ya wahuni na wezi kuivuka na kuja kutuibia hata kwenye uchaguzi.

Tushughulikie ombwe la uongozi na uwajibikaji bila kusahau visheni na misheni ya kwenda karne ya 21.

Tushughulike na kumtafuta ambaye yuko tayari kuwaondoa Watanzania kwenye dimbwi la umaskini walimowekwa na matapeli wa kisiasa.

Tushughulike na kuwekeza katika uchumi badala ya ghilba usanii na siasa za mbwa. Kwa nini badala ya kuwekeza kwenye siasa za uchonganishi, ugomvi na uonevu tusitumie muda huu kujifunza kufikiria na angalau kutimiza ahadi na majukumu yetu?

Kwa nini kitendo cha mbwa kuvaa fulana kisitusaidie kuondokana na takrima za kugawa vitu vya hovyo kama fulana, vibandiko, khanga na ubwabwa?

Je, sisi siyo walevi kiasi cha kujisahau? Kwangu kifo cha mbwa huyu asiye na hatia kina mafunzo mengi.

Ni ishara za kuwa na jamii onevu na ya hovyo. Ni dalili za udikteta. Kwani tunawazuia watu wetu kufikiri na kuonyesha hisia zao.

Kama tunaweza kumuonea mbwa asiye na akili, je, hawa wenye akili watakapotaka kutuwajibisha tutawafanya nini?

Au ni yale yale ya kina Horace Kolimbwa na Daudi Ballalii?

Tulimkolimba Kolimba hatukutosheka. Tulimu-EPA Ballali hatukutosheka. Sasa tunaanza hata kuwanyonga viumbe wasio na hatia. Ni ukatili kiasi gani?

Tuna ubavu wa kuwaua mbwa na kuwanyenyekea wenye silka za mbwa kama wale walioliingiza taifa kwenye nakama. Kiburi chote hiki cha nini kwenye dhamana za umma?
Je, kwa mbwa kuwa habari tena ya juu siyo dalili kuwa siasa zetu zinaanza kutawaliwa na mbwa? Ndiyo. Amezitawala kweli kweli.

Watetezi wa haki za wanyama mko wapi? Watapatikana wapi watetezi wa haki iwapo wamekosekana wa kuwatetea mazeruzeru na vikongwe?
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 15, 2008.

1 comment:

Anonymous said...

I LIKE YOUR BLOG VERY EDUCATIVE AND UTTERLY AWESOME, LAKINI WATANZANIA BLOG KAMA HII HAWA-VISIT WANATAKA BLOG ZA PICHA TU,KWELI TUTAFIKA? THIS IS A BLOG TO READ, KEEP IT UP ONE DAY YES.

Yours: EDWARD ALEX MKWELELE
edwardmkwelele@yahoo.co.uk