

Kwa wanaojua jinsi blog hii inavyochukia nepotism, watakumbuka tumekuwa tukiandika kulalamikia aina mpya ya ufisadi ambapo wake za marais wa kiafrika nao wamegeuka marais kupitia migongo ya waume zao. Wamegeuka wafanya biashara kupitia migongo ya NGO. Wamekuwa waheshimiwa kupitia waandishi habari nyemelezi wanaojipendekeza ima kwao au waume zao. Sasa naona wameongeza kasi kiasi cha kuanza kuwa na ziara za kiserikali kama waume zao. Je jinai hii ya matumizi ya urais kifamilia itaisha lini? Je wananchi wa kawaida wanaliona hili? Eti mke wa rais yumo nchi kwa ziara ya siku sita ili kufanya nini na kwa kugharimiwa na nani? Kesho utasikia ziara ya mtoto wa rais kabla ya kufuatiwa na ya mama yake, dada yake baba yake na upuuzi mwingine. Hata kama kuna wanaopenda na kushabikia mchezo huu, bado ni mchafu unaopaswa kupigwa vita kwa nguvu zote. Maana kinachochezewa ni ofisi na pesa vya umma. Kwa utajiri gani tunaruhusu israfu hii?
No comments:
Post a Comment