The Chant of Savant

Friday 5 August 2011

Nimeanzisha kampuni ya biashara ya MKUYATI

BAADA ya kuona mafanikio ya kampuni yangu ya Trust Fund yangu ya MTF na kugundua kuwa ufisadi na jinai vinalipa kwenye kaya yetu, nimeanzisha kampuni ya Mpayukaji Kampani of Ufisadi Yote And Tanzia Inc (MKUYATI).

Hii kampuni itakuwa tishio kwa makampuni mengine ambayo yamekuwa yakihomola kiasi cha kuwalazimisha wezi fulani kuvuana magamba. Mie si gamba. Mie ni ngozi tena nzito kama ya tembo. Hivyo washitiri wangu walioko Ikuu wasihofie chochote. Hakutakuwa na kuvua gamba wala nguo bali kuvua minoti.

Wabaya wangu msihangaike kwenda BRELA haipo kule. Sikuisajili kule kuhofia wanoko kuifuatilia na kuanika ulaji wangu kama walivyowafanyia akina Kagoda. Nimesajili kampuni yangu kwenye visiwa vya Jersey baada ya kuwasiliana na mtaalamu wa kuficha minoti kule aitwaye Loya Endelea Chenga na Daktari Iddiliisha Rashidun. Mpo washirika hapa?

Bila kuwakawiza ngoja niwamegee kidogo shughuli zetu ambazo zitakuwa kama ifuatavyo:
Kwanza, tutaghushi cheki kwenye mabenki hasa BoT ambayo siku za karibuni imegeuka shamba la bibi ambapo kila jambawazi anaweza kwenda na kuhomola atakavyo na sheria isimfanye kitu. Nani atamgusa iwapo ni ushirika wa wanono. Wazungu huita fraternity in crimes. Kama nimechapia mvumilie na kuelewa mie ni prof wa ung’eng’e. Hata kwa mama wananiogopa kwa kuutema ung’eng’e.

Pili, tutaingiza bwimbwi nchini kupitia Mwl Julias Kabarega Nyenyere bila kushtukiwa kutokana na kuweka vijana wangu kupitia idara ya uhamishaji. Upo hapo? Ukitaka kujua siri ya hili nenda uone vijana walioajiriwa jana wanavyoporomosha mihekalu kama hawana akili nzuri. You know why? It is simply because we nourish them for nourishing our biz. Kaa mkiambudia mibaka na wahalifu sisi tunapeta kama hatuna akili nzuri.

Tatu, tutashughulikia tenda kanyabwoya za kusambaza vitu mashuleni, majeshini, magerezani na kusimamia tenda za ununuzi wa vifaa kama rada, Meli, silaha, ndege, bajaj na mashangingi ya serikali.

Ujambazi usiulize tutapata wapi silaha na vigofu vya kusindikiza mizigo yetu. Waulize ndata wanajua siri hii.

Nne, tunasafirisha nje twiga, chui, viboko, nyoka, kobe na wanyama adimu duniani. Hata ile dili iliyofichuka kule KIA kulikuwa na mkono wangu. Na ndiyo maana mambo hayakwenda popote zaidi ya kuandikwa na kusahaulika.

Hapa huwa nashirikiana na mshirika wangu Brigedia Ally wa Falme za Kimanga aliyeingizwa nchini na mzee mwenyewe wa Ruxa zama zile za kina Muhdeen Ndongala wakibaka Loliondo. Mara hii mmesahau dili hizi kuwa ndicho chanzo cha ufisi na ufisadi wa sasa!

Pia tutawekeza kwenye nishati na madini na kufaidi msamaha wa kodi kwa miaka mia huku tukitafuna na wakubwa.

Mbinu, kupata vimemo toka kwa wazito vimeo wenye maulaji. Tulipata teknolojia hii toka kwa Richmonduli.

Kuanzisha makampuni ya uwakili ya kimalegesi legesi na kimajaarmajaar kusaini mikataba yetu.

Baada ya kuchuma nitagombea ubunge kupitia Chama Cha Mafisadi (CCM siyo Chama Cha Mapinduzi kumbuka).

Ili kupitisha bwimbwi bila mbango tutaanzisha makampuni ya ki-TICKS TICKS.

Pia tuna mikakati lukuki. Tumeishwasiliana na yule mwandishi nyemelezi yaani Shangingi la Kinshomile aitwaye Silvia Rweyependekeza atutafutie waandishi wa kutuandika vizuri ili umma utuamini na kutukubali.

Tutakuwa tukitoa michango kwa mamilioni kusaidia chama na watu wenye shida mbalimbali. Kadhalika, tutakuwa tukikaribisha wanono kuja kufungua miradi yetu. Mbinu hii tumeinyaka toka kwa wale jamaa waliowahi kumtumia na kumtapeli mzee Ruxa aliyekuwa rais wa China wakati wa uzinduzi wa kampuni ya OKO. Tumia OKO. Mara hii mmeisahau OKO! Sijui nayo ilifia wapi Yarabi?

Ili kupata dili za kimataifa, tuna mpango wa kuwa tunaadamana na mkuu kila aendapo ughaibuni kutanua ili kukutana na matapeli sorry wafanya biashara wenzetu wa kimataifa. Tutatoa misaada hata makanisani na misikitini ili waombee biashara yetu ipanuke na kujaa dunia. Yale makanisa shindani ya biashara yetu ya bwimbwi hatutayapa misaada. Tutaanzisha mitandao kwenye CCM ili kulinda maslahi yetu.

Nikishafanikiksha biashara yangu haramu na aibu mtaniona nikianza kuheshimika na kuachana na ulevi wa kangara na mataputapu. Nitaanza kunywa Mutzing bia toka uropa. Nitaanza kupokea vicheko na tabasamu hata kutoka kwa wale waliozoea kuninunia.

Nitaanza kuongea na waheshimiwa kiasi cha kuwa mheshimiwa. Unacheza na pesa nini? Siku hizi walevi hawaangalii umepataje. Ndiyo maana kuna mafala, majambazi na vyangudoa kibao wanaheshimika wakati utajiri wao unatokana na aibu yao. Ni wangapi wanaliwa hata kutembea na mbwa au kaka zao wana pesa na wanaheshimika wakati wanapaswa kulaanika, kuzomewa hata kunyongwa?

Ni machoko na wauza unga wangapi wanaitwa wafanyabiashara maarufu? Je ni majambazi wangapi wanaonekana majukwaani na wakubwa wakati wanapaswa kuwa Ukonga au Segerea? Haya shauri yenu msipotia akilini mtabakia kulalamika na kulialia huku mkiendelea kuliwa mnajiona.

Zipapa lamkani kutzacha! Tafsiri leo sitoi maana imekuwa too much watu wanakaa wanataka kila kitu uwatafunie wao wameze. Bwana Mdogo Yesu aliongea kwa mafumbo ili wenye akili watie akili na waso nazo wabaki kuuchapa. Zipapa lamkani kutzacha au tuseme kuchile! Nani mara hii kasahau maneno
Alisema si wote wasemao Bwana Bwana watauona ufalme wa Mungu. Vihivyo nasema mwenye akili atie akilini na mwenye masikio asikie. Si wote wajiitao waheshimiwa wanaistahili.

Wengine ni vibaka na mibaka iliyochakachua uchaguzi ipate kura ya kula iwale walevi. Hata waitwe wabunge wengi wala ubuge ubuge sirini kama alivyodai Kafulia kuwa waliomba rushwa kwenye wilaya yake ya Uswekeni kule.

Wako wapi waliosema amewakashifu? Kama wamekashifiwa si waende mahakamani. Au ni yale yale ya wale wa Mwembe Yanga? Hata mkulu mzima alinywea na kuendelea kuwahadaa walevi kuwa si fisadi wakati ananuka ufisadi.

Mitaa ya Congo bwana upuuzi mtupu. Naona yule kibaka anatolea mimacho kisimu changu.

Kumbe niko mitaa ya Congo siyo! Kwaheri!
Chanzo: Tanzania Daima, Agosti 3, 2011.

No comments: