The Chant of Savant

Thursday 25 August 2011

Rais avunje na kusuka baraza la mawaziri

Hakuna ubishi. Baraza letu la mawaziri linamweka rais majaribuni na kwenye lawama bila sababu. Maana kila uchao zinafumka kashfa zinazoonyesha kuwa baadhi ya mawaziri hawafai au tuseme hawafanyi au hawajui kazi zao.

Waandishi wa habari watakuwa bado wanakumbuka kashfa ya Loliondo ambapo mwandishi mwenzao Stan Katabaro aliuawa kwa kuifichua na kuishupalia. Hii ilitokea wakati wa awamu ya pili ambapo mwarabu aitwaye Brigedia Ali alishirikiana na watendaji waroho na wapuuzi wa serikali kuliibia taifa.

Wakati ule, wanyama walikuwa wakiuawa hovyo huku wahusika wakishuhudia na kunyamaza kutokana na sababu walizojua. Ilifikia mahali mbuga zetu zikawa kama mali ya watu binafsi. Nani mara hii kasahau ilivyokuja kubainika kuwa baadhi ya mawaziri wa wakati na familia za baadhi ya vigogo walikuwa na maslahi ya moja kwa moja kwenye makampuni ya uwindaji? Kwa sasa sijui hali ikoje ila hali ilivyo itakuwa mbaya zaidi ya awamu ya pili na tatu. Ninachojua ni kwamba mchezo huu wa Brigedia Ali unazidi kunoga. Maana, hata kwenye sakata la mitambo ya Dowans Ali huyu huyu aliletwa na Rostam Aziz akidai ndiye mwenye kampuni wakati siyo.

Japo serikali imekuwa ikisema haina ubia, ukiangalia tangu awamu ya ruksa ya Ali Hassan Mwinyi, ulijengeka ufisadi wa ajabu ambapo wezi na matapeli wa kimataifa hutumia vimemo au mamlaka za wakubwa kuhujumu nchi bila kushughulikiwa. Hii ndiyo siri ya wezi wa EPA kutopatikana wala kushughulikiwa. Wangepatikana na kushughulikiwa vipi wakati watuhumiwa ndiyo hao hao waliopaswa kujikamata?

Hata ukienda kwenye kashfa ya ununuzi wa rada, ndege ya rais na ukarabati wa ikulu wakati wa awamu ya tatu mambo ni yale yale. Tapeli anakuja nchini kwa kutumia mgongo wa mkubwa mkewe au mwanae na kufanya kila uhalifu bila kuguswa.

Ripoti kuwa wanyama 116 na ndege 16 walitoroshwa kupitia uwanja wa kimataifa wa Kilimanjaro kwenda kusikojulikana ni upuuzi. Haiwezekani wanyama wengi kiasi hicho watoroshwe kusikojulikana. Je walikopelekwa hakujulikani? Bila shaka kunajulikana. Kama wahusika hawajui nani wa kumuuliza walipopelekwa hawa wanyama basi waende mamlaka ya anga. Maana hakuna ndege inayoweza kuingia na kutoka nchini bila kujulikana wala kupewa kibali cha kufanya hivyo. Watuhumiwa wa pili ni mamlaka za mbuga za wanyama zilizokabidhiwa jukumu la kulinda wanyama. Hivyo tusidanganywe kuwa wanyama waliotoroshwa hawajulikani walikotoroshewa wala aliyewatorosha. Hapa tutake tusitake lazima kuna mkono wa mtu au watu wazito. Maana itakuwa nchi ya ajabu ambapo madege yanaweza kuingia na kuchukua mali zetu sisi bila kujua. Achia mbali kuingia na kutua nchini. Hata ndege ikikatiza kwenye anga zetu lazima mamlaka husika ziwe na taarifa. Je ni ndege ngapi zimeishaingia mara ngapi na kwa muda gani nchini mwetu na kuondoka na madini, nyala hata dola? Kama ndege zinaweza kuingia na kutua bila kujulikana zinatoka wapi, kwenda wapi na kubeba nini, nini mantiki ya kuwa na mamlaka husika? Je hili haliweki usalama wa taifa letu hatarini hasa kipindi hiki ambapo uhalifu wa kimataifa kama vile kusafirisha mihadarati, silaha na ugaidi vimeongezeka?

Kwa kuangalia uzembe na uhujumu huu wa kutorosha wanyama, tupaswa kumshauri rais avunje baraza la mawaziri na kuwatimua mawaziri husika.

Kwanini tumeruhusu nchi yetu kuwa shamba la bibi tena linalosimamiwa na mataahira?
Siyo siri, kwa sasa kuna mawaziri ambao hawapaswi kuwa ofisini. Hawa ni waziri anayeshughulikia mbuga za wanyama na naibu wake, Ezekiel Maige, waziri wa Nishati, William Ngeleja na naibu wake Adam Malima ambao wameshindwa kutatua tatizo la umeme na uhaba wa mafuta, waziri wa mambo ya ndani, Shamsi Vuai Nahodha na naibu wake Sued Kagasheki ambao jeshi lao la polisi linasifika kwa kuua, na waziri wa ulinzi, Hussein Mwinyi na naibu wake ambao mabomu yao hivi karibuni yaliua watu wasio na hatia kule Mbagala na Gongo la Mboto.

Pia wapo mawaziri waliotuhumiwa kughushi shahada zao za kitaaluma ambao ni Mary Nagu, Makongoro Mahanga, William Lukuvi, na Emanuel Nchimbi.


Pia wapo mawaziri wanaopwaya kwenye nafasi zao kama vile Hawa Ghasia, Celina Kombani,Jumanne Maghembe, Shukuru Kawambwa, Sofia Simba aliyejipatia umaarufu kwa kuwatetea mafisadi.

Kwa wanaofuatilia utendaji wa mawaziri tajwa, watakubaliana nami kuwa wanapwaya kiasi cha kumfanya rais achukiwe kutokana na uzembe au makosa yao. Sina sababu ya kumtetea rais bila sababu. Hii si kazi yangu. Ila kama mwananchi wa kawaida, najua mbivu na mbichi kama ambavyo wengine wanaweza kuona. Bahati mbaya hatuna utamaduni wa kutafuta maoni ya watu wetu kuhusiana na watawala wao. Ungekuwapo utaratibu huu na ukawa ukitumika kuwatimua au kuwabikiza watu maofisini, bila shaka hali ingebadilika tena haraka. Hata hawa niliowaorodhesha kama watapigiwa kura ya maoni, wataonekana kuwa tatizo kwa serikali. Haiwezekani kwa mfano nchi ikae kizani zaidi ya mwaka mzima waziri husika apendewe au aonekane anafaa. Itakuwa ni ajabu ya aina yake. Haiwezekani wanyama waibiwe tena kwenda “kusikojulikana” mawaziri husika waonekane wanatimiza wajibu wao. Haiwezekani watu wapigwe risasi hovyo na kuuawa au kulipukiwa na mabomu mawaziri husika waonekane wanafaa. Haiwezekani kabisa.

Haiwezekani, kwa mfano, waziri anayehusika na utawala bora awalinde mafisadi wazi wazi na bado aonekane anafaa. Haiwezekani waziri wa sheria apinge mchakato wa kuandikwa katiba mpya aonekane anafaa. Haiwezekani. Hata kama wananchi wetu hawana nafasi na hawasemi, wanaona kuwa mambo yanavyokwenda siyo. Wanaishia kulalamika tu kwa vile hawana pa kwenda kushitaki wala wa kuwasikiliza. Badala yake wanatutegemea sisi wachambuzi tuwafikishie kilio chao. Na hii ndiyo maana, badala ya kumtwisha lawama rais moja kwa moja kabla ya kumweleza ukweli, nimeamua kuandika makala hii nikiamini atapata salamu zangu.

Tuhitimishe kwa kumtaka na kumshauri rais kuvunja baraza la mawaziri na kuondoa mawaziri wanaoonekana kuwa mzigo kwake bila sababu. Rais hana sababu ya kulaumiwa kutokana na uzembe wa watu wachache aliowaamini wakashindwa kuaminika. Kuna haja ya kusafisha safu yake ili wote wenye madoa waondolewe na kwenda kujisafisha wakiwa nje ya ofisi za umma.

Kichekesho ni pale eti waziri wa wanyamapori kumsimamisha mkurugenzi wa mamlaka hiyo wakati na waziri ni mtuhumiwa! Tangu lini mtuhumiwa akawahukumu watuhumiwa wenzake?
Chanzo: Dira Agosti, 2011.

1 comment:

Jaribu said...

Shida ni kwamba suruali ya madaraka imempwaya rais mwenyewe na hawezi akaivaa ikamtosha. Si rahisi kwa Kikwete kubaini au kutaka kubaini mapungufu ya wateule wake kwa kuwa anaogopa kuonekana kuwa hakuwa na umakini wa kuwachunguza kabla hajawapa nafasi hizo. Vile vile ana kiburi kama cha George Bush kuwa hawezi kurejea uamuzi wake, hata kama ikija kugundulika kuwa siyo sahihi.

Kwa hiyo Kikwete atakumbatiana na mawaziri wake, kama kuanguka wataanguka pamoja.