How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 17 September 2013

Katiba mpya, Kikwete mshinde shetani

HAKUNA ubishi kuwa Rais Jakaya Kikwete anakabiliwa na mtihani na kishawishi kikubwa.
Hii ni baada ya kuridhia kuandikwa kwa Katiba mpya ya Tanzania baada ya kugundua kuwa katiba viraka ya sasa hailifai taifa katika kipindi hiki cha ushindani na mwamko wa kidemokrasia.
Kwanza tumpongeze Kikwete kwa kuona mbali na kusimamia mustakabali wa taifa badala ya chama. Hata hivyo, hivi karibuni, baada ya bunge likiburuzwa na spika na naibu wake na makada na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuchakachua Katiba kielelezo, Kikwete anakabiliwa na mtihani na changamoto ya aina yake.
Ingawa wengi humuona Kikwete kama rais aliyeshindwa kuamua vema alipoanzisha mchakato wa Katiba bila hata kuomba ushauri wa chama chake, wengi walianza kubadili hisia zao juu yake.
Mambo yalikuwa yanakwenda kama ilivyopangwa hadi Bunge, kwa kusukumwa na CCM kuamua kwa makusudi kutanguliza maslahi ya chama badala ya masilahi ya taifa. Ni aibu iliyoje. Baada ya CCM kulalamika kupitia magwiji wake kama Kingunge Ngomabale -Mwiru aliyekaririwa hivi karibuni akisema kuwa hoja ya Katiba mpya si ya CCM bali CHADEMA, naibu spika aliamua kwa makusudi kuwafukuza wabunge wa upinzani tokana na kukataa kuchakachuliwa kwa katiba kielelezo.
Hapo ndipo mtihani wa Kikwete unapoanzia. Mengi yameishasemwa na kuandika hasa kumtaka Kikwete asijitumbukize yeye na taifa kwenye mtafaruko. Swali la muhimu na kuu ni: Je, Kikwete ataamua kutelekeza taifa ili kunusuru chama au ataweka mbele maslahi ya nchi hata kama ni kwa kukitelekeza chama kilichoishiwa mvuto na uhalali wa kuwa madarakani? Kwa vile Kikwete aliamuru kukusanywa maoni kwa ajili ya kuandika katiba mpya kwa hiari na uzalendo wake, wengi bado tunaamini ana uwezo na nafasi ya kuepusha kuliingiza taifa kwenye mgogoro na mtafaruku visivyo na sababu.
Kuna sababu za kuamini kuwa Kikwete atatumia busara na kuacha kusaini Katiba kielelezo iliyochakachuliwa na CCM na wabunge wao ambao waliipitisha bila kushirikisha wapinzani kana kwamba hii nchi ni mali yao peke yao.
 Pili, Kikwete hatakubali kubeba lawama kwa kuchezea kodi ya mwananchi tena maskini kwa kukusanya maoni ambayo hayakuheshimiwa na chama chake na wabunge wake.
Tatu, Kikwete atatumia busara kuepuka kuonekana kama mtu anayejipinga na asiye na msimamo. Maana kama CCM ilishindwa kumzuia kuanzisha mchakato wa kupata katiba mpya itamlazimishaje kuiua?
Nne, Kikwete hatataka kuacha mfano mbaya wa kiongozi kigeugeu asiyeheshimu mawazo ya wananchi wala utawala bora.
Tano, Kikwete anajua na kuamini kuwa katiba ni mali ya Watanzania na si mali ya wana CCM au wabunge wake. Pia Kikwete anajua fika kuwa Watanzania si wajinga wala majuha wa kufanyiwa hujuma kwenye kila jambo wasichukue hatua mujarabu. Rejea jinsi CCM ilivyoaibishwa kwenye chaguzi ndogo zilizopita huko Arusha na kwingineko.
Sita, Kikwete kama atakataa kusaini muswada wa Katiba kielelezo atakuwa ameweka historia ya kuwa kiongozi anayesikiliza umma wake badala ya kikundi cha watu wachache waliovuruga kila kitu na sasa wakataka hata kuvuruga Katiba. Hakika kwa kukataa kishawishi hiki kichafu, ataingia kwenye vitabu vya historia kama kiongozi wa kupigiwa mfano aliyeweka mbele masilahi ya taifa badala ya chama.
Saba, Kikwete anajua kuwa katiba ni mkataba baina ya watawala na watawaliwa na si nyenzo ya watawala kuwaburuza watawaliwa. Hivyo apuuze watu wenye mawazo mgando wanaomshauri upuuzi wa kulihujumu taifa.
Nane, Kikwete anafahamu kuwa mazingira ya sasa ya kisiasa nchini si sawa na yale ya chama kimoja. Kama nguli wa siasa za chama kimoja Mwalimu Julius Nyerere alifikia mahali akauona ukweli, Kikwete ni nani ajifanye kipofu, kiziwi na kichwa ngumu?
Tisa, Kikwete hana sababu yoyote inayoingia akilini ya kuibeba CCM kwenye suala nyeti kama hili.
Rejea usemi wake kuwa CCM ijiandae  kisaikolojia kuondoka madarakani kama Watanzania watachagua upinzani kwenye uchaguzi ujao. Huu ni ushahidi kuwa Kikwete hataki upuuzi na ni ahadi kuwa atahakikisha uchaguzi ujao unakuwa huru na wa haki.
Kumi, Kikwete  si kiongozi wa kujipiga mtama wala mwenye kuamini katika mawazo mgando na ya kizamani kama wale wanaomshinikiza aue katiba mpya bila kujali madhara yake.
Ushauri kwa wanaomshinikiza Kikwete aue katiba mpya. Kwanza, wafahamu kuwa hawatafanikiwa kunyamazisha sauti ya umma unaotaka katiba mpya ili kusonga mbele badala ya kuselelea kwenye kurudi nyuma.
Pili, wanapaswa kufahamu kuwa Tanzania itakuwapo baada ya wao na chama chao kuondoka. Pia wasome alama za nyakati na kubadilika.
Tatu, waonywe kuwa wanachotaka kufanya licha ya kutokubalika ni kuhujumu umma ambao ndiyo wenye nchi na sauti juu ya ni namna gani watawaliwe.
Tuhitimishe kwa kumshauri Kikwete awapuuze wanaotaka kumchafulia rekodi yake ya kuandika Katiba mpya. Tumpe mfano wa rais wa zamani wa nchi jirani ya Kenya, Mwai Kibaki ambaye aliliangusha taifa kwa kuiba uchaguzi lakini akalitoa mavumbini kwa kuandika katiba mpya kiasi cha kumpa nafasi maalumu na pekee kwenye historia ya Kenya kuliko hata waliomtangulia.
CCM wanapaswa kujua kuwa hakuna akiba zaidi ya kisiasa kama kusoma alama za nyakati na kwenda na wakati.
Kama wanadhani wanaweza kuendelea kuwalazimisha Watanzania jinsi ya kutawaliwa, waambiwe fika kuwa wanatenda kosa kubwa ambalo watalijutia siku si nyingi.
Kikwete, hakikisha unamshinda shetani kwenye mchakato wa kupata katiba mpya ili nafasi yako katika historia ya taifa iwe marejeo ya kila wanazuoni na wachambuzi wa mambo.
Chanzo: Tanzania Daima Sept., 18, 2013.



No comments: