How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 4 September 2013

Mpayukaji kuwaanika wauza bwimbwi hadharani

BAADA ya lisirikali kukiri kuwa lina majina ya wauza bwimbwi lakini halitaki kuwataja kwa vile wengine ni wahishimwa, mzee mzima nataka niweke wazi majina ya vigogo wa dawa za kulevya.
Hivyo, wazee wamewahi kuja kusikia majina ya madingi wa bwimbwi. Mioyo inawadunda kweli kweli. Kwa vile wananiamini, wanaamini sitafanya kama yule waziri aitwaye Bill Likuvi aliyesema eti wanaogopa kutaja kwa vile wengi wa watajwa ni wahishimiwa.
Woga mtupu na kulindana. Mshindwe na kuangamia kabla hamjatuangamiza na tamaa na roho mbaya zenu. Naomba Mungu azidi kuwapa miwaya na ugonjwa wa moyo ili nanyi muangamie kama mnavyoangamiza vijana wetu. Aaamina.
Uzuri mie siogopi hili wala lile kwa vile watuhumiwa wangu si wanakijiwe bali wahishimiwa tena wakubwa sana.
Hata wangekuwa wanakijiwe mie ningepayuka tu. Hata angekuwa ni Sir God mie ningemwaga mtama. Eti liwaziri hili linasema eti wanaogopa kutaja majina kwa vile hawajakusanya ushahidi wa kutosha. Tell it to the birds.  Mgeambiwa wana mpango wa kupindua mngekuwa na cha kungoja au msalie mtume bali kukamata?
Mpemba anaamua kutupa sumbwi la kwanza baada ya kuona nimeingia na magazeti yangu nakuendelea kusoma bila kutaja. Anasema: “Yakhe mie nchukia sirikali hasa mkuu wallahi. Wasema wana majina ya wauza unga lakini wagoma kutaja? Yakhe huu ubabaishaji wa hali ya juu ati.”
Kuona kama ananisimanga, naamua kumpa live. “Ami huna haja ya kuwalaumu kwa kutotaja. Kama unayo majina si utaje wewe kwanza au unangoja kutajiwa hata watu unaowajua?
Kwani huwaoni hao unaotaka niwataje? Mbona kwenye daladala unapanda nao kila siku na humuulizi kapata wapi mibwimbwi kwani siri?”
“Mie nijuao si vigogo bali dagaa, vinginevyo wangekuwa vigogo nshataja ati.” Anajitetea.
Mijjinga anaamua kuingilia kati: “Kwani hao dagaa si wauza unga mami? Kama unawajua wewe tajaga tutajuaga kigogo na fito wasikilizaji.”
Mgosi kuona wazee wanaanza kutoana macho wenyewe kwa wenye anaamua kunivaa kinomanoma: “Wagosi hatina haja ya kuandikia mate wakati wino upo.”  Kabla ya kuendelea ananigeukia na kusema: “Mgosi Mpayukaji si ulisema kuwa leo titaambiwa majina ya wauza unga. Tafadhai basi taja walau tiende tikawatie madole kama si mangumi.”
Kabla ya kuendelea, Mbwa Mwitu anaingilia: “Unasema eti muwatie madole wauza bwimbwi? Thubutu! Si watakakuua kabisa?”
Msomi Mkatatamaa baada ya kuona Mbwa Mwitu anaendelea na utani anaamua kuweka guu, “Mzee.” Ananiangalia huku akitabasamu, “Basi tupe habari kuhusiana na wauza bwimbwi au nawe unataka ufanye kama mkuu mwenyewe ambaye amekalia orodha kwa miaka saba?”
Naamua kujitetea: “Mie si kama huyo ila msinighasi kana kwamba mnanidai ati.”
Mipawa kachukia kaamua kutia buti. “Nkwinga usitake kutuchanganyaga. Kama huwajui huna haja ya kutuwekaga roho juu. Au wamekukatia kitu kidogo na kikubwa ukaamua kuwa kama wale wanaowatetea na kuficha orodha zao?”
“Mipawa tuheshimiane. Kwanza niombe msamaha kwa kunilinganisha na mafisi na mafisadi wasio na huruma wala akili zaidi ya kutumia masaburi.”
Nafoka huku nikimtazama Mipawa kwa hasira.
Kanji kapata pa kushika: “Sasa kama veve jua hao uza unga kwanini hapana taja? Sasa ona vatu naanza chukia na kosea veve heshima.”
Kuona maji yanazidi unga naamua kujitetea zaidi, “Mbona mna haraka hivyo? Mnaweza kuniharakisha nikaamua kuwataja nyinyi. Eti Kanji nianze nawe siyo?”
Kanji kusikia hivyo anachachawa na kuogopa na kusema: “Sasa Payukaji veve tani baya sana. Badala taja gogo ya dawa anza onea vatu dogo kama mimi?”
Mgosi Machungi naye anaamua akamue: “Waswahii waisema haaka haaka haina baaka na ngoja ngoja huumiza matumbo. Hebu timpe muda Mpayukaji atitajie hawa wahaifu haafu tuwatokee na tiwachome moto kama vibaka au mnasemaje?”
Kaswahili, huyu na Mijjinga ni wanakijiwe wapya waliokuja kutembea, anakamua mic: “Mzee tunakuaminia. Hutafanya kama wale ambao baada ya maunga yao kunaswa Sauzi waliamua kuepusha balaa kwa kuja na sinema ya Shehena Pondwa. Huoni wachovu walivyosahau kila kitu?”
Mijjinga anamuunga mkono Ntayomba, “Tena umenikumbusha. Hivi lile suala la unga uliokamatwa Sauzi zaidi ya Mwakiembe kuwatimua vidagaa limeishia wapi?”
“Unauliza jibu ndugu yangu? Hili shamba la chizi. Nani anakumbuka zaidi ya wahusika kujikita kwenye sinema nyingine kama kutimuana uanachama na upuuzi mwingine?”
Nikidhani kuwa yameisha si Msomi alining’ang’ania. Alisema, “Mzee hebu sasa mwaga mtama basi.”
Mgosi naye alipigilia msumari wa mwisho, “Mpayukaji, kama nilivyosema. Hebu titajie tiende tiwafundishe adabu sasa hivi bila kujai kama ni wakubwa au wadogo. Nina hasia mie tate nane.”
Bila kujivunga nilianza kutaja, “Wauza unga nambari wani wapo pale airpot. wa pili mnawajua. Mliwapigia kura kwenye uchakachuaji uliopita.”
Hata kabla ya kuendelea kila mmoja alipigwa na bumbuwazi asiamini niliyokuwa nimesema.
Mie kuona hivyo niliendelea: “Muuza unga namba moja aaanh tusameheane. Muuza unga namba mbili ni wale wahubiri wanaoibuka wakawa matajiri wa kutupa ndani ya muda mfupi.
Wanajifanya kuhubiri neno la Bwana wakati wanafanya biashara ya maunga. Kwani hamuwajui? Muuza unga namba tatu ni aaaanh mkuuuu lo! Tuyaache. Kigogo wanne ni wale wanaowakingia kifua wakiogopa kuwataja.”
Eti walitaka nitaje wakati kila mtu anawajua. Nendeni muwakamate mateja wawambie wanakopata hiyo kitu au nenda uwanja wa ndege mkaulize wale wanaowaruhusu kila uchao.  Mbona wanawabomu mia mbili wakapate?
We mkatie tau moja uone kama hakupeleki kwa wauza. Mkishindwa si muende ikulu muombe rais awape orodha ambayo amekalia miaka saba.
Kijiwe kikiwa kinanoga si alipita manzi nikamkata jicho na kusahau kila kitu kiasi cha Wanakijiwe kunizomea. Niliamua nijikate kwa maudhi.
Chanzo: Tanzania Daima Sept., 4, 2013.

No comments: