The Chant of Savant

Saturday 21 September 2013

Mlevi akataa PhD watasha vinywa wazi


Wiki iliyopita ilikuwa ya zali.  Chuo kimoja hapa Ukandani kilijipendekeza kwangu na kutaka kunipa PhD. Chuo hiki kilitumiwa na wabaya wangu waliotaka niwasukie ulaji kwenye shamba la bibi.
Hivyo, kiliamua kutumia ujanja wa kunipa PhD ili kiniingize mkenge niwauze walevi.
Baada ya kugundua janja yao niliwaambia wazi kuwa `sishobokei’ PhD. Niliwapa `laivu’ kuwa mimi si `kihiyo’, wala mpenda sifa kama yule. Inashangaza sana kuona mtu anapewa PhD wakati anafanya `madudu’ kwenye kaya ya walevi.
Kama kungekuwa na PhD ya Mismanagement of the hunk, basi ingemfaa. Mie si wa hovyo hivyo kuhongwa udohoudoho kama PhD na suti.
Huwezi kuharibu elimu halafu ukapewa PhD ikawa na maana. Kama kungekuwa na PhD za Mismanagement of Resources and Education, basi ingewafaa wale wote waliobaka elimu kiasi cha kughushi na kununua shahada kuwa the order of the day.
Kwani hawapo? Kwani hamuwajui. Leo nina hasira sana hasa wakati huu ninapovililia vitegemezi vya walevi vilivyotapeliwa kwa kujazwa ujinga badala ya elimu.
Anayebisha aende pale kwenye chuo cha Manzese ajionee mwenyewe jinsi wanaoitwa wanachuo wanavyofanya mambo ya kipuuzi. Imefikia mahali vitegemezi vyetu vimegeuka vyagudoa huku vikinunua hata majibu kama ilivyofichuliwa kule kwenye kaya ya Nyayo ya Uindependence Kinyatta.
`Watasha’ wakiwa wamejiandaa kunikaanga kwa kunizawadia makaratasi ili nifanikishe `dili’ la kuwauza walevi, walipigwa na mstuko nilipoingia na gunia la shahada za kweli, tena zilishokwishaota ukungu, nilizozipata kabla ya kuanza ulevi na uvutaji bangi.
Walishangaa kuona nina PhD in Elightenment, Management, Philosophy, Cosmology, Astrophysics, Finance, Boozing na `madude’ mengine yenye majina magumu. Walishangaa kuona mlevi nina busara kama mzee Mchonga.
Kitu kilichowaumiza vichwa ni kudai kuwa siwezi kukubali kupewa shahada bila kuangusha dissertation. Walikaribia kupata kichaa nilipowapa link ya dissertation yangu iliyovunja rekodi kwenye dissertation zangu nyingi iitwayo Decolonizing the whole, mind, soul, body and Consciousness.
Kitu kingine kilichowapagawisha ni kuonyesha tabu la dissertation yangu ya How to do away from begging and globetrotting and the whole nitty gritty of spending wisely.
Katika kitu hiki hatari na cha kisomi nilitoa hoja kuwa ili kuendelea, lazima uendelee kimaadili kwanza. Ujue hesabu rahisi kuwa huwezi kujenga uchumi wa kaya yako kwa kutegemea `kubomu’ na kuzurura ambapo unatumia `njuluku’ nyingi kuliko `unazobomu’.
Mkuu wa chuo, sitakitaja kwa sababu za kiusalama, alitoa mpya aliposema kuwa chuo chake kilitaka kunitunuku PhD kwa vile huwa naandika mambo ya kufikirisha.
Alinivunja mbavu aliposema kuwa walikuwa na mpango wa kunipa PhD nyingine kwenye jiografia kwa vile ninashika rekodi ya kuizunguka dunia kama akina Olusheiguni Oba Sanjo, Jake Zuma, Jake Kiquette na Yowe M7.
Kwa vile nilishagundua janja yake, nilimwambia kuwa kama kuzurura ni `dili’ basi hiyo PhD wawape kunguru ambao huruka toka India hadi Uswazi na kufanya unyani wao.
Niliwapa wazi kuwa mimi si Vasco da Gama wala Barthromeo Diaz, Mungo Park, Ferdnand Magellan na majambazi wengine walioleta ukoloni Afrika.
Watasha walidhani mie mshamba na limbukeni wa `kushobokea ujiko’ wa shilingi mbili. Walidhani nikiitwa Porofwesa Dk Dk Dk Dk Mlevi Orijinal nitajiona `dili’ wakati ni aibu.
Najua kuna walevi hawana raha kwa kukosa kuitwa Daktari hata kama udaktari wenyewe ni wa `kuchonga’. Kuna kipindi huwa nashangaa jinsi ambavyo mlevi anaweza hata kughushi hata kununua PhD ili naye aonekane msomi.
Kwa vile wengi hawana ndururu wala maulaji huamua kujiingiza kwenye jinai ili wapate ujiko.
Hata hivyo, kuna njia rahisi ya kupata PhD kwa wale `wanaozishobokea’.Ukitaka kupata kitu hii hakikisha unapata urais hata kama ni wa vibaka. Vyuo vikubwa vitatumia cheo chako na kukupa kitu hii ili vikamilishe `dili’ zao.
Kwa vile natokea kwenye kaya yenye madini na `dili’ kibao, vyuo viliweka mitandao yao vikitumia wapambe wangu wakaongea nami niingizwe `mkenge’ wanufaike na ulabu wa walevi.
Walikosea kudhani PhD ingenihamasisha sana kiasi cha kuanza kupanga mikakati kuhakikisha na Bi Mkubwa wangu anapata kitu hii, ili wote tuitwe madaktari.
Kwa vile wapo madaktari wa kughushi na wa kienyeji, baada ya kugundua janga hilli, napanga kupiga marufuku walevi wote kuacha kutumia udaktari wao wa mbao.
Walidhani kwa vile chuo kilichotaka kunipa PhD kinatambulika, tena cha kaya iliyoendelea, basi ningejiona `dili’ wasijue mie si mpenzi wa makuu. Kuna kipindi vyuo fulani vya uchochoroni vilitaka kuniingiza mjini kama vilivyomfanya jamaa yangu mmoja ambaye sitamtaja leo.
Niligutuka kwa vile mimi si mtu wa kupewa shahada na vyuo vya uchochoroni ambavyo huviona kama vyoo vikuu badala ya vyuo.
Mfano, inakuwaje chuo ambacho hakina hata ithibati ya kutoa shahada ya pili yaani kwa `kimakonde’ Masters, kimpe mtu PhD? Mie si juha bwana. Haya `madudu’ nayajua hata kama ni mlevi na mvuta bangi.

Hata hivyo, kuna walevi wenye akili walionionya kuwa sina haki ya kuitwa daktari, kama udaktari wenyewe ni wa heshima. Wapo waliotaka kunigeuza juha kwa kusema eti udaktari wa heshima ni more original and real than yule wa darasani. 
Wajinga wakubwa. Eti walisema kuwa siku hizi kama akili yako inachemka huna haja ya kwenda kupoteza muda darasani kusomea PhD. Utasomeaje kitu ambacho unacho naturally?
Hivyo watasha walinipa mafuta kwa mgongo wa chupa kuwa wanafahamu kuwa mimi nina akili kuliko wale waliopoteza muda kusomea PhD zao.
Hata hivyo, wapo wanaosema kuwa ukiangalia wasomi wengi wenye PhD, `madudu’ wanayofanya unashindwa kuelewa ni kwanini watu wanakandia PhD za heshima.
Hebu tujikumbushe historia. Hivi madaktari kama Daudiii Balaliii aliyeingizwa `mkenge’ na vihiyo kama Roast Tamu la Aziz ni msomi kweli? Hivi Daktari kama Idd Iliisha Rashid aliyeiba `njuluku’ na kuzificha Uswisi sambamba na Endelea Chenga ni daktari wa kweli au vibaka waliopewa PhD baada ya kuibia mitihani darasani?
Sijui kama Daktari Mgimua anayetuletea mahesabu na takwimu za uongo kila siku anastahili kuheshimiwa kuwa ni daktari.
PhD waliyotaka kunipa ni sawa na zile za vichochoroni kama za akina mchunaji Gettie Rwakatarehe kibaka anayesifika kuiba ardhi. Hivi ubomoaji wa mjengo wake aliojenga kinyume cha sheria umeishia wapi?

Chanzo: Nipashe  Sept., 21, 2013.

4 comments:

Anonymous said...

Iwapo chuo kinaitwa "Gulp Univesity" tutegemee nini?

Usijali spelling wala walikuwa wana-"gulp" nini huko?

Dunia nzima imeamua ku-komesholaizi elimu siku hizi.

What matters is not how much is in your head, but.....

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon,
Ni kweli elimu imechakachuliwa hasa baada ya kugundua kuwa viongozi wetu waliokimbia umande wanapenda shahada za dezo. Ni bahati mbaya kuwa hata hao wanaogeuzwa mabwege hawakengeuki zaidi ya kushobokea shahada hizi za aibu. Shame on them all!

Anonymous said...

Huwa ninacheka sana unavyounga majina ya hawa "waishiwa" na matukio.

Ninakumbusha tu umesahau kumtaja dakitari mwingine aliyetakiwa kusimamia "show" ya uvunjaji au uvunjifu wa mijengo tata mjini pale.

Sgughuli tunayo

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon,
Huwa siungi majina. Huo ndiyo ukweli mtupu bila makengeza wala nguo feki. Sina jinsi ya kuelezea ninayoelezea zaidi ya jinsi ninavyoyaelezea. Hata nawe unaweza ukiamua.