How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Sunday, 17 August 2014

Mlevi atikisa kwa Obama

       Baada ya mlevi kutoa tishio la kutaka kubomoa ghorofa uaji la uhindini si wahusika wameamka na kuogopa hadi wakapiga nyundo mahekalu ya mchunaji Rwakatarehe. Hayo tuyaache humu si mwake.
Najua wengi wataona natania wasijue mwenzao si mwenzao bali ni Future World leader. Basi washirika, si nilipata zali la mentali kuhudhuria kongamano la Young African Leaders kule kwa mzee Brack Obama kama ambavyo bi mkubwa wake Michele wa Mpunga hupenda kumuita. Tuliteuliwa vijana wanaochemka kwenda kumpa jamaa tafu kuhusiana na jinsi ya kuitawala dunia ambayo imegeuka gunia kutokana na wajuaji na wajinga wengi kuiyumbisha kuanzia ugaidi wa akina Bin Aladin hadi wa ule wa akina Ben Niitenyau pale Gaza na kwingineko,
          Kwa vile mimi ni kipanga katika kufikiri na kuchemsha akili, nilikaribishwa pamoja na bi mkuwa wangu yaani Mama Domo Kubwa Kulakula binti Kutanua kwenye kongamano hili la Young African Leaders ili lau niwafunde wahusika wajue majukumu yao baadaye baada ya Afrika kuliwa na wakoloni weusi. Si baada ya kumaliza huo mkutano wa Young African Leaders tukaarikwa kwenye mwingine wa Old leaders African Leaders. Mwakwetu, hapa kulikuwa na mambo na vijimambo usisikie. Kwa vile Old African Rulers wameishazoeleka na vimbwanga vyao, waliowika kwa vimbwanga wakati huu ni bi wakubwa zao wapendwao kuitwa First Ladies hata kama wengine ni second ladies. Hayo tuyaache.
          Nawapongeza sana first ladies wetu kwa kuonyesha jinsi bara letu lilivyotajiri. Maana walipiga pamba hadi Michele akaonekana kama housegirl wao. Walikula vitu vya bei mbaya kiasi cha gazeti moja kuchanganyikiwa na kuandika, “If all those bags were authentic, there was at least $20,000 worth of internationally-recognized status on display in the form of satchels and shoppers.” Maana yake kwa kimasai ni kwamba kama mikoba yote ilikuwa si feki basi wapo walioshika mikoba yenye kufikia dola za Kimarekani 20,000. Wamarekani walishangaa sana na kuhoji kuwa inakuwaje waume zao waende kuomba wakati utajiri wanao na wanaukalia? Mmojawapo aliniuliza nikamjibu kuwa Afrika kwa ufupi haikuwa maskini bali tajiri maskini. Nilimfahamisha kuwa, kimsingi, waliochokuwa wakifanya first ladies ni kuonyesha madaraka ya waume zao ambayo ni yao pia. Walikuwa wakionyesha faida za kulala kitanda kimoja na bwana mkubwa kiasi cha kugeuka bi mkubwa yaani rais nyuma ya pazia.
           Baada ya Michelle kugundua pamba aghali walizokuwa wamepiga first ladies wa Kiafrika, aliamua kujivalia kagauni ka mtumba ili kuogopa kumufilisi mumewe ambaye ukimlinganisha na marais wa Kiafrika kiutajiri utagundua kuwa yeye ni maskini kuliko hata shamba boys wao. Anachowazidi ni kuongoza taifa tajiri kuliko yote wakati nao wakimzidi kwa utajiri wakiongoza mataifa maskini kuliko yote duniani. Unaambiwa wamama wa watu walifanya kufuru kiasi cha kuwaacha wamarekani wamechachawa na kutaka waende Afrika kugundua siri ya utajiri huu wa kutisha.
          Baada ya kugundua ushamba wa wamarekani wa kushangaa vitu vya kawaida kama ukwasi wa watawala wetu na wake zao, niliwatolea uvivu kwa wasome tabu langu la Nyuma ya Pazia. Niliwapa kiduchu kuwa wake za viongozi hawapaswi kutumia kwa woga wala kujali nani anakula au kulala njaa kwa vile wao wana walipa kodi wanaogharimia matanuzi yao.  Hivyo, kazi yao ni kutanua na si kuwaza nani analala njaa au kufa kwa magonjwa yanayoweza kutibiwa au kuzuilika.  Katika usawa wa kifisadi kufikiria mwenzio ni ushamba. Niliwapasha wamarekani wasishangae kusikia eti watawala wa Kiafrika wanaomba au kukopa. Hii ni kutokana mazoea tu ili kujichangamsha na kukutana na wenzao lau wapate namna ya kusafiri nje na kujifunza maajabu ya dunia. Wahenga husema: Kutembea kwingi ni kujua mengi. Unaweza kuongeza kuwa kusafiri sana ni kupata per diem nyingi. Nani asiyetaka kutanua huku akilipwa Per Diems kwa kufanya hivyo?
          Hakuna walioniacha hoi kama jarida la Washington Post ambalo huwa napenda kulisoma ninapokuwa Umarekanini. Nalo liliona miuya na kuandika, “From high hair to status handbags, Africa’s first ladies use fashion to talk about the past and the future.” Hii sitafsiri. Kama hujui kinyasa shauri yako. Naongopa kuharibu uhondo wa kichwa hiki cha habari kinachoongea yote. Wakati jamaa hawa wakishangaa shangaa mavazi wapo waliozimia dogo dogo ambao baadhi ya vibabu vimevuta. Jamaa yangu Paul Bia wa Kameruni aliwaacha hoi na kimwana wake Chantal. Pia mhuni Junkun Yahaya Jammeh ambaye tulipiga skuli pamoja alitisha na kimwana chake  Alima Sallah binti wa balozi wake Saudia alichoozwa kumlia vyake baada ya kushindwana na bi mkubwa Zeinab aliyetimkia Umarekanini. Waswahili kwa kutetemekea na weupe acha!  Utadhani jamaa zangu akina Mura Wirema!
          Ukiachia mbali mashindano ya kupiga pamba, First Ladies walishindana kutafuta wafadhili wa makampuni yao almaarufu NGOs ambayo waliyaunda baada ya waume zao kuukwaa. Wamarekani walishangaa wakihoji kama wahusika hawatatumia njuluku hizo kupiga pamba na matumizi mengine binafsi. Wakati wakishangaa mikoba ya dola alfu ishirini wapo walionusurika kufa kwa shinikizo la moyo nilipowapa kuwa hiyo dola 20,000 ni pesa ya kifungua kinywa kwa wamama hawa waliobarikiwa kuliko wengine. Maana niliwapasha kuwa ukihesabu thamani ya mikufu na migold yao wengine wanavaa midudu hadi ya $300,000. Hapa hujaongelea akaunti zao nono zilizotapakaa ughaibuni wala za waume zao au vitegemezi vyao.
          Kwa kufuru na nyodo walizomwaga first ladies, acha niachie hapa vingenvyo mwaweza kuzimia nikisema yote. Good news, mke wa mlevi wala hakuonekana kwa vile alipiga pamba zake za mitumba ya Manzese.
Chanzo: Nipashe Jumamosi Agosti 15, 2014.

6 comments:

Anonymous said...

watauza sura sana lakini hawana tija ila ufisadi nakuchaguwa marafiki kwenye nyadhifa nyeti lakini mtajuta 2015

Anonymous said...

watauza sura sana lakini hawana tija ila ufisadi nakuchaguwa marafiki kwenye nyadhifa nyeti lakini mtajuta 2015

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon usemacho ni kweli. Hakuna tija kwenye ushamba na matanuzi yao.Hata hivyo, naomba sana Mungu hili janga lituondokee na atokee mtu mwenye udhu aliweke lupango na genge lake la majambazi.

Anonymous said...

Mkapa alisema kweli msichaguwe Rais kwa uzuri wa sura
japokuwa enzi zake tulimuita FUSO kwa ajili ya uso wake lakini alisema

Anonymous said...

URAIS UNATAFUTWA KWA NGUVU ANANGALIENI KWA MICHUZI GLOB MKE WA RAIS MTARAJIWA ETI ANATOA MISAADA YA MATREKTA CCM HIYO NA WAFADILI WAARABU TEMBO WATAPONA

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon unaongelea bi Dorcas Membe siyo? Huu ni ushahidi kuwa jamaa zetu wameishanunuliwa na wanapumulia mifukoni mwa mafisadi, Hata hivyo sidhani kama CCM wanaweza kufanya kosa kuruhusu rais ajaye atoke Mtwara. Hivyo, Membe anapoteza muda wake. Usishangae wanaotajwa tajwa wote wakanoa akachomolewa mtu mwingine kusikoeleweka ilmrad awe tayari kuwalinda mafisadi waliopita na wanaomaliza muda wao na waramba viatu na makalio yao.