How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday, 23 August 2014

Mlevi ahoji: Dini au duni ‘Askofu’Jambazi?

Mlevi huwa si mpenzi wa kushangaa. Ila hii ya hivi karibuni ya jambazi na kibaka aliyejipachika Uaskofu kufungwa miaka 32 imemuacha hoi. Je wako wangapi waliojificha nyuma na juu ya mimbari wakijivika kama wateule wa bwana wakati ni mbwa mwitu wanaowararua watu wake?
Je wako wangapi wenye majina hata magari makubwa wakijifanya wanamuhubiri Yesu wakati wakiishi na shetani? Je ni wangapi wanaojifisia kuwa na roho mtakatifu wakati ukweli ni kwamba wana roho mtakakitu? Utawajua kwa sura zao, maneno yao, ukwasi wao hata vyeo vyao vya kujipachika. Tangu lini askofu wa kweli akajiteua? Tangu lini mchungaji akajiteua? Huyu kweli ni askofu au asmbovu? Huyu ni mchungaji au mchunaji?
Acha tuwape inshu nzima. Jambazi mmoja aitwaye J4 Kilongola wa Kanisa la Christian Followship Assemblies of God kule Arusha alikula mvua 32 baada ya kupatikana kwa kosa la kuvunja na kuibia benki mwaka 2004. Mdukuzi huu jambazi na bazazi alishirikiana majambazi wengine toka nchi ya Kenya.
Hawa jamaa, kabla ya jeshi la Bongo kuamua kuja na kanuni ya shoot to kill, yalikuwa yakijisifu kuwa ukienda kwenye benki Bongo kuwaibia unawaambia wafanyakazi, “Tafadhali fumbeni macho tuwaibie” nao wanafumba macho mnahomola.Ila baada ya ndata kuamua kuwamiminia shaba mbona mchezo uliishia kama kibatari kizimikavyo?
Kwa vile mlevi alishaonya, si mara moja wala mbili, lisirikali kuchunguza majambazi waliojificha nyuma ya dini na kupuuziwa, nadhani sasa watafumbua macho. Hata hivyo, nina shaka. Wengi wamekuwa waki-survive kwa kujifanya ni wapenzi na wakereketwa wa nambari wahedi.
Kamuulize mchunaji Gettie Rwakataare bingwa wa kudanganya akina mama kuwa anaweza kuwaombea wakapata waume wakati yeye mwenyewe ni kanunga. Muulize Zach Ka-Tortoise aliyewahi kusema kuwa rais Jake Kiquette ni mpole sana. Ndiyo maana anawaacha wapinzani.
Wengi hawakujua. Kumbe jamaa alikuwa akijikomba kwa mkuu ili azuie TANESCO kupitisha nyaya karibu na duka la njembe hii liitwalo kanisa.Baada ya mkuu kumtolea nje mbona jamaa anaongea utadhani ni kiongozi wa upinzani aliokuwa akikandia na kuchongea! Hapa kuna dini au duni kama si dili?
Bwana mkubwa Yesu aliwahi kusema kuwa wengi watakuja wakilitaja jina langu. Alionya, “Msiwaamini kwani watapotosha wengi.” Je hamuwaoni wakijidai na mahekalu na migari ya bei mbaya huku hata wengine wakiiba wake za wenzao? Yuko wapi yule dada aliyesifika kuimba akaolewa na sharubaro mmoja ambaye alifuata umaarufu asijue mwisho wake ni ufu? Jose Gwaiji-iima upo hapo? Da Flo Mbaaasha upo hapo nawe mshirika?
Mwambie mkaguzi mkuu wa hesabu za kaya akawakage hawa wanaojiita maaskofu. Atagundua ukwasi wa kutisha utokanao na wizi wa sadaka na mihadarati pia ujambazi kama huyu aliyedakwa na kutoswa lupango kwa miaka 32. Wako wengi. Tunawajua kwa sura na majina yao.
Utamsikia bambataa na jambazi akiita mara mzee wa Upako kumbe ni ubako wa njuluku za walevi.Namkumbuka mmoja akiitwa Sili Gamanyua aliyejikomba kwa waziri mkuu fulani. Jamaa alipotimka madarakani na jamaa akifilisika na kuanza utapeli.
Kusema ule ukweli wa Mungu, uchungaji hasa huu wa kujipachika umegeuka uchunaji wa watu wetu. Hauna tofauti na uganga wa kienyeji.
Nakumbuka mmoja bazazi na jambazi aitwaye Gwaijie aliwahi kumtukana na kumsingizia hata baba wa taifa Mwl JKN kuwa aliiweka kaya chini ya shetani.
Nashangaa hawa waduwanzi wanaojifanya kuvaa viatu vyake walikaa wakichekelea wasifunge mtu. Ajabu waliweza kuwafunga akina Babu Yeya tena kwa kugombea mabibi lakini wanashindwa kumshikisha adabu mpuuzi mmoja anayemsingizia na kumtukana mzee Mchonga wetu!
Sitashangaa siku nyingine askofu wa kuchonga kama huyu kukamatwa na viungo vya zeruzeru kama siyo kufumaniwa na mke wa mtu.Hawa jamaa wana laana ajuaye Subhana mwenyewe.
Wamegeuza jina la Yesu biashara ya kuibia wachovu huku mamlaka zikishuhudia!  Hawa hawana tofauti na mashehena yaitwayo mashehe kama wale waliokuwa wakifanya uganga wa kienyeji na utabiri uchwara.
Je wako wangapi jijini wakitangaza dhambi zao wazi wazi na mamlaka zikiangalia? Utalisikia hili likisema eti linaongea na majini.Thubutu! Ukiona jini wewe si Hutojinyea? 

 Tuangalia upande wa pili wa sarafu.
Je ni kwanini majambazi wanafanikiwa kujivika vyeo vya kidini kirahisi? Je sababu ni ile hali ya kaya kugeuka waabudia vitu na uganga wa kienyeji na ushirikina? Je inakuwaje wapuuzi wanatangaza urongo kama vile kuongea na majini, kutibu ukimwi, kutengeneza nyota za utajiri wakati wao ni kapuku na umma haustuki? Je kaya ya namna hii si kaya ya mataahira, vichaa na wahalifu?
Ningekuwa mkuu mtu akatangaza kuwa anatibu ukimwi basi ningetoa amri akamatwe na kuambukizwa ukimwi ili ajitibu tujiridhishe. Hawa wanaotangaza kutengeneza nyota za utajiri ningewalazimisha wazitengeneze ili kaya yetu iachane na uombaomba na kopakopa na udhalilishaji tunaoshuhudia kila siku ambapo mkuu amegeuka kiguu na njia kofia mkononi akiomba hata akivaa suti ya bei mbaya namna gani.
Tumalizie kwa kuwaonya wachovu kuacha uchovu na bangi kiasi cha kugeuzwa shamba la chizi na majambazi na matapeli wanaojifanya wanahubiri dini wakati ukweli ni kwamba wanahubiri duni.
Mshikwe wapi ndipo mgutuke? Kwanini mnajirahisi kuliwa mkiona na kila tapeli kuanzia wale wa barabarani, mahospitalini hadi kwenye siasa na sasa kwenye dini? Ogopeni siku ya siku mtachomwa kama kuni kutokana na ujuha na ujinga wenu. Enyi wanakaya wapumbavu, nani aliyewaroga ambao kila kitu kiliwekwa wazi machoni penu kuwa hawa si viongozi wa dini kitu bali duni na dunia gunia? Tieni akilini kabla hasira za baba hazijawashukia.

Chanzo: Nipashe Agosti 23, 2014.

No comments: