How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 19 August 2014

Kijiwe kulipiza kisasa kama Silaha atauawa


BAADA ya kunyaka nyuzi kuwa baadhi ya makada wa Chama cha Mauaji (CcM) kupanga kumnyotoa roho katibu mkuu wa Chakudema Dk. Willy Silaha, Kijiwe kimeamua kutoa msimamo wake kuhusiana na huu mfumo wa kigaidi na kijambazi unaoanza kuzoeleka.
Mbwa Mwitu anaingia akiwa anaimba, “Wameishiwa! Wamezidiwa! Wamegeuka chinja chinja! Wamegeuka magaidi!”
Wote tunashangaa staili hii mpya ya kuingia na mbwembwe, tambo kushangilia na kuzomea. Mpemba anaamua kumuuliza Mbwamwitu nini kimemsibu na hao walioishiwa ni akina nani. Anasema, “Yakhe mbona watuchanganya? Hao waloishiwa ni nani?”
 Mbwa Mwitu anajibu, “Ami hujui! Husomi magazeti nini?” Anamrushia gazeti la Danganyika Always Today. Kichwa cha habari kinachoongoza kinasema, “Mashele apanga kuwanyotoa roho Dk. Silaha na M-nyika.”
 Wakati Mpemba akiendelea kujielimisha na gazeti, Msomi Mkatatamaa aliyekuwa ameishazinyaka anaamua kushuka kinoma. Anasema, “Tulishasema. Uteuzi wa hovyo wa wahuni na wapuuzi wasiojua mipaka ya madaraka yao utawatokea kinywani. Hivi mtu kama huyu aliwezaje kuteuliwa waziri?
Mijjinga aliyekuwa ndiyo anaingia anaamua kupoka mic, “Kwanza wakubwa niwape habari njema. Bi mkubwa ametuletea Queen Anatalia.”
Kabla ya kuendelea Mipawa anakwanyua mic, “Nkwingwa, kwanza hongera. Je ni kwanini umempa jina la Anatalii? Je ni kwa vile amezaliwa chini ya utawala wa mtalii Njaa Kaya ambaye yuko kwa Kichaka akitanua wakati wenzake waliisharejea siku nyingi?”
 Mgosi Machungi anaamua kuchomekea, “Ulitaka amwite Salma au Aisha?”
Mijjinga anakwanyua mic tena, “Hilo la mtoto si muhimu sana. Nataka nijibu maswali mazito na magumu ya Msomi anayeshangaa Mashele aliwezaje kuteuliwa kuwa waziri. Kwanza, uwaziri siku hizi hauna tofauti na utarishi hasa ikizingatiwa kuwa kuna vilaza na vihiyo wengi tena walioghushi walioteuliwa kwenye nafasi hii.”
 Mipawa anakubaliana naye, “Huyu jamaa namfahamu sana akiwa anasoma shule ya Msingi Ngokolo. Hana lolote na hafai. Akifaa basi anafaa kuwa baunsa lakini si vinginevyo. Hata hivyo, sishangai. Najua uhusiano wake na mtoto wa kigogo mwenye maulaji ambaye naye amegeuka kuwa mkuu kwa vile baba yake ni mkuu. Huyu ndiye aliyemsukia akaula.”
Msomi anatikisa kichwa na kusema, “Sasa naelewa. Maana hata kwenye madai ya kurubuni hawa madiwani huyu kitegemezi anatajwa sana pamoja na wahuni kama vile Mwiguu Michembe, Nipe Mapepe Ninaye na Eddie Ewassa. Jamani wanaipeleka wapi kaya yetu hawa wanahizaya?”
 Sofia Lion aka Kanungaembe aliyekuwa akifikicha kucha zake anaamua kukamata mic, “Hakuna haja ya kutukana watu kuwa ni wahuni. Kama mwenye mamlaka ameona wanamfaa nyinyi ni nani kuhoji kama siyo utovu wa adabu?”
Kanji hafichi ushabiki wake. Anakatua mic, “Sofia ambiya yeye kweli. Hii nasumbuliwa na viwu tu. Kama yeye fahamiana na toto ya kuba kosa ya nani?”
Kapende aliyekuwa amekaa kimya muda mrefu anaamua kumchomekea Kanji, “Wewe na Sofi tunawajua sana. Mna mapenzi ya kibubusa. Kwa vile nanyi ni wasaka tonge lazima muunge mkono kila upuuzi wa chama chenu.”
Sofia hakubali. Anakwanyua mic tena, “Wewe unayajua mapenzi ya kibubusa au unasema tu?”
Kabla ya kuendelea Kapende anamchomekea akisema, “Sofi angalia lugha yako vinginevyo nitamwita We-rema aje akushughulikie ukome.”
 Mheshimiwa Bwege aliyekuwa akicheka anaamua kuokoa jahazi kwa kuingilia kati akisema, “Tuachane na upuuzi wa We-rema na Mashele. Nadhani cha mno na muhimu kujadili hapa ni hatua gani tutawachukulia hawa magaidi wanaopanga kunyotoa roho wenzao. Napendekeza tutoe karipio tukilaani ugaidi huu kwa kutaka vyombo husika viwachukulie hatua hawa magaidi kabla hatujaenda kuwachoma moto kama vibaka.”
Huku akitikisa kichwa kumkubali mheshimiwa Bwege, Msomi anakatua mic, “Mheshimiwa Bwege umesema mambo makubwa na ya maana. Kwa vile Dk Silaha na M-nyika ni viongozi wa watu wote, lazima tuwalinde na kuwapa moyo wasiogope.
Nani huyu anayetaka kutoa uhai wa wenzake kana kwamba yeye hatakufa? Mashele aambiwe wazi kuwa kama amezoea kuua vikongwe huko kwao, ajue. Hawa si vikongwe wala vihongwe bali watu makini wanaoweza kumgeuzia kibao kisheria tena kwenye asasi za kimataifa akapotezwa. Wako wapi akina Chaz Taylor wa Liberia na wahuni wengine waliojiona miungu kwa vile walikuwa madarakani?”
Mgosi anaamua kuongezea, “Tiwafahamishe waeewe kuwa hata kama wengine ni vitegemezi wa wakubwa au wametumwa na baba zao, hakuna mkubwa kuliko kaya. Titawafunga. Tena hawa ni ahisi kuwafunga ikizingatiwa kuwa mwakani watakuwa nje ya madaaka. Wasitichezee. Ohooo! Mwenye akii na atie akiini.”
 Mpemba baada ya kumaliza kusoma gazeti anaamua kula mic, “Hivi hawa jamaa wameingiliwa na nini mbona huko nyuma hawakuwa hivo? Wadhani waweza kudhulumu roho za watu wakashinda? Wallahi hili halivumiliki hata kidogo. Lazima, kama alivosema mhishimiwa Bwege tuwashughulikie hawa manyang’au kabla hawajatekeleza ugaidi wao.”
Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si lilitolewa wazo kuwa tumwendee Mashele huko aliko tumtie adabu. Hivyo, wote kwa pamoja isipokuwa Kanji na Sofi tuliamua kuingia mitaani kumsaka Mashele ili tumtie adabu kwa kumfanyia kitu mbaya.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 20, 2014.

3 comments:

Anonymous said...

hana mpango huyu mtoto
kwanza si mtu wa SHY mjini ole wako mwakani

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon unamaanisha huyu jamaa si mtu wa Shy Mjini, ni mshamba wa kawaida asiyejua afanyalo? Basi mpigeni chini kwenye uchaguzi ujao ili mjikomboe na kuondokana na aibu mnayopata toka kwa kilaza huyu gaidi.

Anonymous said...

si mwanashinyanga huyu katoka MASWA kwa kina SHIDUDA WANYATUNZU MAFISADI HAKUNA USUKUMANI