The Chant of Savant

Wednesday 6 August 2014

Je kwanini Kikwete anawakwepa UKAWA?


       Baada ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kususia vikao vya Bunge Maalum la Katiba (BMK) wakitaka kuonana rais Jakaya Kikwete ambaye ameonyesha kuwakwepa, kumejengeka hisia kuwa anawagwaya. Je Kikwete kweli anawagwaya au ana sababu nuzuhu? Hebu tudurusu mkwamo huu kujaribu kuona ni kwanini Kikwete hataki kukutana na UKAWA.
Wapo wanaoamini kuwa sababu mojawapo Kikwete kutotaka kukutana uso kwa uso na UKAWA ni ile hali ya kutoweza kujenga hoja ana kwa ana. Hivyo, kuhofu kuzidiwa na UKAWA.  Hapa lazima Kikwete apige chenga ili bora liende hata kama taifa likakosa katiba kuliko kuramba matapishi yake.
Wapo wanaoona kama Kikwete amezoea kuvizia vizia baada ya kupata hoja za upande wa pili. Rejea alivyomvizia mwenyekiti wa Tume ya Kukusanya Maoni Jaji Joseph Warioba. Je akijipinga tena ataweka uso wake mbele ya wahafidhina wa CCM waliombana hadi akakengeuka na kupingana na dhamira safi ya kuandika katiba mpya isiyo na mizengwe?
 Pia zipo hisia kuwa Kikwete anaogopa kutoa maoni mengine yanayoweza kukinzana na msimamo wa chama na wake wa awali baada ya kupewa hoja zenye mashiko na ushawashi na UKAWA jambo ambalo hatari yake ni kutoa msimamo tofauti na ule alioutoa wakati akivuruga rasmi alipomvizia Warioba na kuhutubia bunge maalum baada yake kinyume cha sheria.  Maana, alipaswa kuhutubia kabla na si baada ya Warioba. Hapa lazima Kikwete aogope kujifunua na kuandamwa zaidi.  Kwa alivyovuruga mambo, kwa vile yeye si gwiji ataizidi kuonyesha uhovyo wake.
Licha ya kuwachukiza wahafidhina kwenye chamani na wakongwe waliomhadaa na kumbana akabadili msimamo, Kikwete akitoa msimamo tofauti na ule wa kuvuruga mchakato wa katiba atakuwa kwenye hatari ya kuonekana kigeugeu sifa ambayo, hata hivyo, hawezi kuikwepa baada ya kuvuruga mchakato mzima wa katiba mpya.
Sababu nyingine ni kutegemea makada wa chama wenye mazabe na madhambi yao wamalize kazi japo wameonyesha wazi kushindwa. Ukiachia mbali na hili, magwiji waliokuwa wakimshauri, mfano, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru hakuunga mkono uvurugaji. Dhambi ya Kingunge ni kusema, “Kuna tofauti kubwa za kiuchumi kati yetu na wale waliotutawala. Tatizo letu sisi tunaandika Katiba ambazo hazina msingi wa kiuchumi ndani yake, badala yake zinakuwa na mwelekeo wa kugawana vyeo kama njugu.” Hili halikuwapendeza wakubwa wenye tabia hii ya kuiba na kugawana madaraka kama njugu.
Pia hatujui kama wale waliomdanganya wakamtisha na kumtibulia msimamo wanaendelea kuvuta kamba nyuma ya pazia hasa ikizingatiwa kuwa maovu yaliyowasukuma kujenga na kumtia hofu Kikwete bado yako pale pale. Maneno makali kama haya ya kada mwenzao mwenye msimamo tofauti bila shaka yanazidi kuwachochea wavute kamba zaidi. Kingunge ndiye kada pekee mwandamizi aliyekemea CCM pale ilipoanza kumshambulia na kumtusi Jaji Warioba. Na hakika baada ya kufanya hivyo matusi yalikoma.
Sababu nyingine Kikwete kujizungushia washauri na wasaidizi wabovu wanaoangalia maslahi binafsi badala ya yale ya taifa. Hivi unategemea nini toka kwa wasaidizi kama waziri mkuu Mizengo Pinda aliyeonyesha kupwaya na kufanya mambo kienyeji kama kuamuru askari wawapige wapinzani jambo ambalo walilitekeleza kwa kuua watu? Unategemea nini toka kwa makamu wa rais Dk Gharib Bilal ambaye tangu ateuliwa kazi yake ni kufungua mikutano na matamasha?  Hii ilithibitika wakati wa mgomo wa madaktari ambapo walimshauri naye akakubali kukwepa mgogoro kwa kwenda ughaibuni wakati ambapo alipaswa kuwa nchini ili aotoe maelekezo. Unategemea nini kutoka kwa watu kama Samuel Sitta ambaye analitumia sakata la UKAWA kutafuta kuteuliwa agombee urais? Hata jinsi alivyoutatua kwa kuamrisha kutekwa kwa rais wa Chama Cha Madaktari (MAT) Dk Steven Ulimboka unaweza kutoa mwanga juu ya UKAWA wanashughulika na mtu wa aina gani.
Kikwete na wenzake wako radhi nchi ikose katiba hata kuingia kwenye machafuko kuliko kupata katiba mpya ambayo inatishia mstakabali wao hasa baada ya kuvurunda na kufanya ufisadi wa kutisha madarakani. Kwao ni heri kukosa katiba wakasalimika kuliko kupatikana majaliwa yao baada ya kuachia madaraka yakawa shakani. Kama alivyosema mzee Kingunge, kuna tofauti kubwa kiuchumi kati yetu na waliotutawala. Nani anajua Kikwete ana utajiri kiasi gani iwapo aligoma kuutangaza huku akizungushazungusha?
Pamoja na Kikwete kuona kama kupiga chenga na kugwaya kukutana na UKAWA ni suluhu ni ya muda mfupi. Iwe chini ya uongozi wake au ujao lazima katiba mpya itaandikwa na yale yanayosababisha kugwaya kuandika katiba mpya bado yatafumuliwa kama wahusika watakuwa hai. Je UKAWA watalegeza msimamo wao au kuendelea kuukazia? Uwezekano wa UKAWA kutobadilika ni mkubwa hasa ikizingatiwa na mizengwe na makosa yanayofanya na serikali kama kuruhusu bunge liendelee bila UKAWA wakati ni kinyume cha sheria. Busara isipotumika kuna uwezekano wa pesa ya umma kufujwa bila kupatikana katiba mpya ukiachia mbali hata kuzua machafuko. Ukwepaji majadiliano ni suluhu ya hovyo na ya muda.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 6, 2014.

2 comments:

Anonymous said...

Viongozi walevi wa uongozi wanapoendelea fikra za kilevi na porojo katika mambo muhimu, na kushangaa nani adui wa maendeleo na kuendelea omba omba kwa nchi za magharibi...Mnyoo kama alivyokuwa akiita Marehemu Ilunga, Mnyonyo ukiisha unapigwa chini na rundo la madeni

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon nimependa analogue yako ya mnyoo. Sijui kama wanajitambua hata wakijitambua kama wanakubali na ukweli huu mchungu. Mngoje Njaa Kaya mwakani atakavyokuwa akihaha kuomba vibarua lau apate kuzurura kama alivyozoea.