The Chant of Savant

Saturday 30 August 2014

Mlevi aenda Bondeni kumpa tafu Maleema


Juzi mlevi alikuwa amealikwa na chata la Economic Freedom Fighters (EFF) la Julius Maleema aka Juju ili kushuhudia akimtia adabu mzee Jake Xuma, dingi wa Bondeni mbele ya umma wa wasauzi na dunia nzima. Timing yao ilikuwa poa kinoma!  Mlevi, kwa vile ni mtu wa zali, hakujivunga. Alishirikiana vilivyo na waheshimiwa wa EFF kuzomea bwana kuba bila kujali kuwa ni rahisi. 
Kwa magenge twawala yaliyozoea kujiona vijogoo yajue. There are new kids on the block. Kwa tulioshuhudia mzee Mzima Xuma akigalagazwa na mtoto aliyemtengeneza mwenye, Maleema, watakubaliana nasi kuwa murume amekutana na saizi yake.  Baada ya Xuma kumtumia Maleema kumpoka madaraka rahisi wa zamani mzee Taabu Mvuyelwaa M-beki tena kwa aibu alikosea. Alidhani yalikuwa yamekwisha asijue ukipanda mbigiri unavuna hiyo hiyo na aishiye kwa upanga lazima afe kwao. Sasa mzee Mbeki yuko anachekelea tena baada ya kuombwa msamaha rasmi na Maleema mnamo Aprili mwaka huu. 
Hakuna kitu kilichomuumiza, kumuaibisha na kumnyima usingizi Xuma kama zomea zomea ya EFF wakipiga kelele, we want our money back yaani tunataka urejeshe uchache wetu. Walikuwa wakimshinikiza kulipa Rand (haya ni madafu ya Sauzi) milioni 200 zilizotumika kuboresha makazi yake binafsi kule kijijini kwake Nkandla Kwazulu-Natal. Xuma alisononeka na kuondoka mjengoni kimya baada ya spika Mbeleka Mbwete kutishia kuleta polisi wa kuzuia ghasia asifanye hivyo baada ya tishio lake kutofua dafu. 
 Waishiwa wa ANC walijiribu bila mafanikio kuingilia hoja za EFF. Kila mbinu ya kuwahujumu EFF ilifanyika bila mafanikio. Hatimaye, baada ya maji kuzudi unga, Mbwete, yaani Makindamakida wa Sauzi, alibwaga manyanga na kuamua kuahirisha kigwena huku Xuma akiondoka kimya kimya akiinamisha kichwa kwa ghadhabu na aibu. Ni pigo si mchezo mwanangu. Hata nilipokwenda kumpa pole Xuma alikataa kupokea mkono wangu wakati sisi ni mabeste ile mbaya. 
Kitendo cha kuahirisha kikao kati kati ya kipindi cha mkuu kujibu maswali ya waishiwa, licha ya kuwa pigo kwa Xuma na chata lake la Afrikan National Congress (ANC) ni aibu na pigo kubwa tu. Kimsingi, Xuma alistahiki alichotendewa. Kwani, wakati ule Maleema akiwa dingi wa Umoja wa Vichipukizi wa ANC alimshushia matusi mazito M-beki huku Xuma na wenzake wakichekelea wakingojea kupoka madaraka wasijue historia ina tabia ya kujirudia. Sasa ni zamu yao. Wanaanza kulalamika wakati walimtengeneza Maleema wenyewe kwa uchoyo na upogo wao. Tuachane na ya Malema na Xuma. 
Si uzushi. Bongo inahitaji Maleema wake baada ya wapingaji waliopo kuwa kondoo wazuri ukiachia mara moja moja kujifaragua chini ya Umoja wa Kondoo wa Kaya (UKAWA). Ukiangalia jinsi Chama Cha Maulaji na Malazimishi (CCMM) kinavyoburuza Kaya huku kikijifanyia mambo ya hovyo kitakavyo, tunahitaji Malema wetu. Zamani tulikuwa naye Chris Mtikisa aliyetikisa hadi nyasi. Hatujui kilichompata gwiji huyu wa siasa za kukabiliana kwa maneno makali na bila woga.   
Ukiangalia jinsi, kwa mfano, njuluku yetu inavyoibiwa kwa kulipana kwa mambo ya kijinga kama Mjengo wa Mauaji ya Katiba (MMK) uliogomewa na UKAWA, unatamani Maleema angezaliwa au kutengenezwa Bongo lau arejeshe kuheshimiana na kuthaminiana miongoni mwa walaji wetu. Haiwezekani genge moja litugeuze mateka na majuha kwa kutuletea kila upuuzi na asitokee Maleema. 
Je Maleema wetu atazaliwa au kutengenezwa lini iwapo wale ambao tulitarajia wangefanya kazi hii wamo kitandani na watesi wetu? Vijana wa Bongo mko wapi? Je hamuoni huu uhuni na jinai mnazotendewa? Wezi wanalipana laki tatu kwa siku bila kufanya lolote zaidi ya kupotosha Kaya nanyi mnaangalia tu! Mbona huko nyuma hamkuwa hivyo?   
Mmeingiliwa na nini Yarabi? Hivi hizi laki tatu wanazopeana zingeweza kusomesha au kutibia vitegemezi vya walevi vingapi? Je zingewezesha kupeleka maji kwenye vijiji vingapi vya walevi? Je zingewezesha kujenga barabara kilometa ngapi ili walevi wagongwe vizuri na wenye mashangingi yao yatokanayo na kuwaibia? Hayo ndiyo maswali magumu na muhimu mnayopaswa kujiuliza wakati huu ambapo Kaya iko msalabani likisulubiwa na wezi wasio na uoni wala visheni. 
Tunataka Maleema atakayemshikisha adabu mkuu ambaye hujifanyia mambo tena ya hovyo na kuchefua atakavyo kana kwamba yeye ndiye papa pekee baharini. Tunataka Maleema atakayehoji matumizi ya Nkandla yetu yaani safari zisizoisha ughaibuni za Vasco da Gama wetu, tenda feki, manunuzi ya kutia shaka, utoro maofisini hasa unaofanywa na mawaziri kama ilivyogundulika juzi juzi wakati wa kutafuta kukamilisha akidi ya kupitishia katiba yao ya mizengwe wanayoita  Katiba mpya wakati si chochote wala lolote bali sanaa na uhujumu kwa Kaya na vitegemezi vijavyo. Tunataka Maleema  wa walevi sasa hivi.  
Uko wapi Maleema wetu? Uko wapi tukufuate na kukuunga mkono hata kama una ugomvi wako wa asili na wenzio? Hilo halituhusu. Heri kukutumia kwanza na baada ya kumalizana nao tunaweza kujipanga upya na kujua ipi mbivu na mbovu hata mbichi.
CHANZO: NIPASHE 

No comments: