Baada ya kuwazidi kuzoeleka taarifa za kuhuzunisha ambacho wanene wetu wanadedia kwenye hospitali ya Apollo huko Ugabacholini, Kijiwe kimeamua kujitoa kimasomaso na kuhoji deal hili ambapo wanene sana wanawateua wanene kiasi wagonjwa ili kutibiwa kwa njuluku za kijiwe huku wanakijiwe wakiteketea kwa magonjwa yanayoweza kuzuilika na kutibiwa.
Leo Kapende analianzisha, “Jamani waheshimiwa mwaonaje hili dili la wanene wetu kudedia ugabacholini wakati huduma za afya hapa kayani zikizidi kuhujumiwa na kudumaa?”
Mipawa anakula mic, “Hata mie nashangaa uroho na roho mbaya hii ambapo wanene wanaijihudumia kwenye hospitali zenye kila kitu huku wakituachia hospitali zisizo na kitu chochote zaidi ya mateso na mauti. Sijui inakuwakuwaje hadi wanene wagonjwa wanabakizwa kwenye ulaji ili wafie humo na matibabu yao tubebeshwe sisi.”
Mijjinga ananyakua mic, “Unashangaa hili! Kwa taarifa yako hii ni kaya ya wagonjwa na walafi ambapo –kwa makusudi mazima –wajamaa wanaojijua kuwa wako hoi bin taabani wanawania ulaji na kupita bila kupimwa afya zao jambo ambalo linaongeza mzigo kwa wachovu wa kaya hii. Nani anajali iwapo kila mnene anaona ni zamu yake kula?”
Mpemba anakatua mic, “Yakhe mie nshashangaa sana. Kwanini tusibadilishe sharia kiasi cha kutaka kila anayegombea nafasi ya umma apimwe afya yake ili kuepuka kaya yetu kugeuzwa mfadhili wa wagonjwa tena wenye njuluku nyingi?”
Msomi Mkatatamaa anatia guu kwa zali na kusepa, “Hakuna haja ya kushangaa hasa ikizingatiwa kuwa kikundi kidogo cha walaji, mafisadi, wezi, wasanii na wababaishaji wamepoka kaya yetu kiasi cha kufadhiliana hata kwa gharama ya afya na maisha ya wachovu wetu. Ukiangalia takwimu unaweza kuzimia. Sell Kombania, Abdi Kikalio, na yule mama mwingine sijui anaitwa nani wamedidia kule wakitibiwa kwa njuluku za umma. Ukiangalia waliodedia kule Apollo tangu fasheni ya kuhujumu na kuua huduma za afya ianze unaweza kuzimia. Inashangaza mnene mkuu anayeondoka kuwa bingwa wa kuteua wagonjwa ilhali wachovu wazima na wasomi tupo.”
Mheshimiwa Bwege anakula mic, “Msomi usinichekeshe japo si kwa furaha. Nani akuteua wewe uende kuwaumbua kwenye wizi, ufisadi na ulaji wao? Thubutu! Kayani sifa za kitaaluma hazina maana tena zaidi ya kujuana na mitandao mingine ya kishenzi inayohujumu kaya yetu. Laiti kama rahis au mkewe wangekuwa ndugu zako unadhani ungekuwa hapa kijiweni ukilalamika wakati una elimu ya kutosha na ya juu kuliko hata rahis mwenyewe? Mie nadhani wanene watueleze waziwazi kuwa tumegeuka kaya ya wagonjwa. Vinginevyo tusipoamka na kushupalia wizi huu wa kulindana na kufadhiliana, tutaendelea kunyotoka roho huku wenzetu wakienda majuu kupima hata kutibiwa mafua.”
Sofia Lion aka Kanungaembe anakwanyua mic kwa usongo, “Hivi jamani nani aliwaroga wachovu wa kaya hii? Mnataka wanene nao wakasongamane na kutolewa njuluku kwenye hospitali zetu uchwara kana kwamba wao si wanene siyo? Kwanza mmempata wapi huu uongo kuwa wanatibiwa kule kwa njuluku zenu kama siyo umbea na roho mbaya? Nani amewazuia nyinyi kwenda kutibiwa Apollo kama siyo roho mbaya tu?”
Kanji anakatua mic, “Mimi iko unga kono veve dada yangu Sofi. Kama India natoa huduma bora zito yote takwenda kupata huduma bwana. Kama nasindwa jenga hospitali zuri yako tegemea nini jamani? Nasahau kuu nakwenda kwa Joji Chaka tibiwa ile gonjwa nafisha ogopa stua nyinyi penzi yake?”
Mgosi Machungi anakatua mic kwa usongo, “Da Sofia na Kanji tiheshimiane na tisitiane madole eheee! Titachenjiana hapa. Kwani inataka kusomea inteijensia kujua kuwa wanakwapua njuuku yetu? Nadhani kama wewe hujui waivyo waroho na wenye roho mbaya basi hupaswi kuja hapa na kama utakuja hapa basi ujinyamazie.”
“Mimi mwenzenu hakuna kilichoniumiza kama kifo cha huyu Phil-ku-Njombe aliyekufa kwenye ajali ya chopa hivi karibuni. Utadhani mwaka huu ni wa wanasiasa!” analalamika Mchunguliaji ambaye mara nyingi huwa hachangii sana.
“Ni kweli inahuzunisha. Nadhani kuna haja ya kuoni vyombo na miundo mbinu yetu. Maana nijuavyo, kwenye ufisadi uliotamalaki, kila kitu huwa hatari hasa vyombo kama ndege. Nadhani haya makampuni yanayoendesha hii biashara ya chopa yanapaswa kumlikwa kuona kama yanafuata taratibu zote za kiusalama. Hata hivyo sina shaka watashughulikia kutokana na kuwa nyenzo hii mara nyingi inatumiwa na wanene ambao mara nyingi huwa hawataki shida,” anajibu Msomi.
Anakohoa na kuendelea, “Kuhusiana na hili la kama wanatumia njuluku zetu au zao mfukoni, nadhani kila kitu kiko wazi ingawa da Sofi anajitahidi kuupaka rangi upepe. Mgosi umemjibu vizuri. Kwa walivyo waroho, wabinafsi na wenye roho mbaya bila shaka wanalipiwa na njuluku yetu ya kodi ambayo licha ya kulipiana matibabu wamekuwa wakiiba na kuwapa washihrika zao misamaha ya mabilioni ya njuluku.”
Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si ukapita msafara wa geneza la kamanda Deo Phil-ku-Njombe likielekea kwenye hekalu lake alilolioacha bichi kule Kijichi. Wote tuliamua kumsindikiza kamanda huyu aliyechukia ufisadi na aliyonyotoka roho akiwa bado mbichi.
Chanzo:Tanzania Daima Okt.,21, 2015.
No comments:
Post a Comment