Si kawaida kwa mgombea wa chama kulaumu chama chake au serikali yake hasa pale kinapokuwa chama tawala. Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi, Dk John Magufuli na katibu mkuu wa CCM Abdulrahaman Kinana wamesikika mara nyingi wakikosea serikali ya rais anayeondoka Jakaya Kikwete. Lawama zinapotolewa na watu hawa zinakuwa na ukweli na zinapaswa kuwa na athari kuliko zikitolewa na wapinzani ambao mara nyingi hulaumiwa kwa kulaumu hata kama wanachosema ni kweli.
Hakuna ubishi kuwa serikali ya awamu ya nne ni moja ya serikali mbovu Tanzania ilizowahi kuwa nazo. Tutatoa sababu.
Kwanza, hakuna ubishi kuwa serikali ya Kikwete haikutimiza ahadi zake jambo ambalo wakosoaji wake huliita usanii au utapeli.
Pili, imesababisha uchumi na sarafu yetu kudorora. Nakumbuka wakati Benjamin Mkapa akiondoka madarakani shilingi yetu ilikuwa ikibadilishwa kwa takribani 1,200 kwa dola. Sasa imeporomoka zaidi ya nusu.
Tatu, ilisababisha deni la taifa kuumka bila maelezo tokana na matumizi mabaya kama vile kusafiri kwa rais nje mara kwa mara akiandamana na walaji wengi ukiachia mbali kutokusanya kodi vilivyo na kupanua serikali bila sababu. Rejea kuongeza idadi ya mikoa na wilaya kwa sababu za kisiasa zaidi ya za kiuchumi.
Nne, serikali ya awamu ya nne ilifuga na wakati mwingine kushiriki ufisadi. Rejea kuingia kwake kuhusishwa na kashfa ya EPA na sasa Escrow ambayo walioisuka wako nje wakiendelea kuheshimiwa hata kupewa tuzo za uongo na ukweli.
Tano, ilipoteza fedha nyingi za umma kwenye mambo ya hovyo kama vile kutumia mabilioni kugharimia ukusanyaji wa maoni ya katiba mpya iliyoishia kuuawa huku maoni aghali kama haya yakidharauliwa. Wengi wanajiuliza: Kama Kikwete hakutaka kuwa na katiba mpya ni kwanini aliharibu muda na fedha vya umma?
Sita, iliua elimu kiasi cha wasomi wetu wanaozalishwa kwa sasa kushindwa kuajirika hata kujiajiri.
Saba, iliahidi kurekebisha mikataba ya uwekezaji ikaishia kuingia mikataba mingine michafu na ya hovyo kuliko hata ile iliyopaswa kuirekebisha. Rejea uuzaji wa Richmond kinyemela kwa Dowans ambayo nayo iliingia kinyemela kiasi cha kuendelea kupoteza fedha za umma. Rejea utata wa ubinafsishaji wa lililokuwa Shirika la Usafiri Dar Es Salaam kwa kampuni yenye kutia shaka ukiachia mbali kuhusishwa na vigogo ya Simon Group.
Nane, kutumia fedha nyingi kujenga barabara zisizofikia viwango wala kulingana na gharama ya fedha zilizotumika. Rejea madai yaliyotolewa na vyombo vya habari kuwa barabara nyingi–licha ya kujengwa chini ya viwango–zimepunjwa ukubwa wake kiasi cha kugeuka makaburi ya abiria wasio na hatia. Hata tuhuma zilizotolewa, serikali haikujihangaisha kukanusha wala kutoa maelezo.
Kimsingi, makosa ya serikali ya awamu ya nne hayawezi kujadiliwa kwenye makala moja au hata kumi. Hivyo, kwa kuangalia hayo machache juu, tunashauri rais ajaye afanye yafuatayo.
Kwanza, asijiingize kwenye jinai ya kuzurura ughaibuni bila sababu. Akifanya hivyo, atakuwa hajifunzi kutokana na makosa.
Pili , afufue uchumi kwa kukusanya kodi , kuziba mianya ya kukwepa kodi na kuzuia misamaha ya kodi ambayo mara nyingi ni dili kati ya wafanyabiashara na wakuu wa idara za mapato.
Tatu, afumue mikataba ya uwekezaji ya kijambazi ili lau taifa liweze kunufaika na raslimali zake.
Nne, awashughulikie watuhumiwa wote wa ufisadi wanaojulikana ambao serikali inayoondoka –iliwaogopa au kuwaacha kwa sababu ijuazo –kiasi cha kusababisha tuhuma kuwa nayo ilikuwa ikila nao.
Tano, ahakikishe elimu yetu inafufuliwa kwa kurejesha mfumo wa zamani uliwapa changamoto wanafunzi kusoma vitabu mbali mbali badala ya vichache wanavyosoma kwa sasa na kumaliza shule bila kupikwa na kuiva vya kutosha.
Sita yote katika yote, ahakikishe katiba ya wananchi iliyouawa kwa hofu za kifisadi inapatikana. Hili –licha ya kuwa muhimu–ni rahisi kulitimiza tokana na kuwepo maoni yaliyokusanywa na Tume ya Jaji Warioba.
Saba, asiendelee na tabia ya kuunda mikoa na wilaya kwa sababu za kuzawadiana na kufadhiliana kisiasa kama ambavyo imekuwa.
Nane, atimize ahadi alizotoa kwenye kampeni kiasi cha kuwashawishi wananchi kumchagua. Nadhani aibu anayoipata Kikwete inatosha kutorudiwa vinginevyo ajaye awe ni photocopy ya utawala unaoondoka kiasi cha kuwafanya wapiga kura wajutiea kuwa wanawaamini wanasiasa bila kuwa na mfumo wa kuwawajibisha ambao kimsingi ulikuwa kwenye katiba mpya iliyouawa.
Mwisho, rais ajaye asiruhusu mkewe kujiingiza kwenye biashara ya kuanzisha NGO kwa ajili ya kufanya biashara ikulu. Pia atangaze mali zake na za mkewe ili ujue ameingia na kiasi gani na akiondoka ataje ujue ataondoka na kiasi gani. Tusisitize kuwa rais ajaye asiwe kama Mkapa aliyeingia akiwa maskini akaondoka akiwa tajiri kiasi cha kushindwa kutaja utajiri wake.
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 11,2015.
No comments:
Post a Comment