Baada ya Anna Tamaa Makapu na Salimia Kiquette kuugeuza ufesti leidi biashara, Mlevi ameamua kutoa nasaha kwa festi leidi ajaye. Kwanza ngoja nitoe utabiri wa kweli. Festi leidi ajaye atakuwa mwanamke. Pili atakuwa na elimu ya wastani. Tatu, atakuwa anasikiliza ushauri wangu.
Kwa vile nimeishazoea kuishi na festi leidi wangu wa walevi kwa zaidi ya miaka 20 ambavyo ni vipindi viwili vya urahis, nina uzoefu mkubwa na mafesti leidi. Mimi na gwiji Mchonga Kambarage wa Burito tuliwazuia mafesti leidi wetu kujiingiza kwenye uchuuzi na umachinga wa kwa mgongo wa ikulu. Hatukutaka ikulu iwe pango la wezi. Hatukuwaruhusu waanzishe kampuni almaarufu NGOs za uongo na ukweli. Mara Fursa za Ulaji kwa Wao mara MAWA. Wizi mtupu tena wa kichovu. Nani angekubali biashara hii kichaa yenye kutia aibu mamlaka? Kama ni kuhudumia akina mama si wizara ya wanawake na watoto ipo? Kwanini kuanzisha NGO mumeo anapoingia madarakani na si kabla kama si kutafuta utajiri wa haraka tena wa kifisadi? Piga buku kama Graca Machel uone.
Basi, kwa vile ufisadi huu wa kichovu umeanza kukubalika, leo natoa waraka maalum kwa festi leidi ajaye.
Kwanza, namtahadharisha na biashara ya NGO. Inachafua heshima yake, mumewe na utawala mzima. Mama anayejiamini hawezi kujificha nyuma ya mgongo wa mumewe.
Pili, namshauri festi leidi ajaye asijiingize kwenye siasa za majitaka za kugombea vyeo uchwara kwenye chama cha mumewe simply because ni mke wa mwenyekiti. Wala asiruhusu watoto wake wala ndugu kutumia mgongo wa mzee kutafuta ulaji wa kisiasa au kibiashara kupitia NGO na upuuzi mwingine. Hata kama atakaidi akaenda kuomba kama jamaa yangu fulani ambaye mzee wake anaongoza kwa kwenda nje kubomu naye akifuatana naye kuomba misaada ya uongo na ukweli, ni aibu. Hata ukijengewa kijishule kimoja au viwili vya sekondari kama miradi binafsi bado hutaacha kuonekana mroho na mbinafsi na anayetumia madaraka vibaya.
Tatu, namshauri festi leidi ajaye aende shule ajipigie kitabu badala ya kukimbizana na vijesenti vya aibu. Mfano wa kuigwa ni festi leidi wangu wa walevi. Hana NGO wala si mwanachama wa chama changu cha Ugali Nyama na Maharagwe (UNM). Nilipochaguliwa na walevi kula vyao kirahisi yeye aliamua kupiga book. Tena mwenzenu kasoma ughaibuni na hata akiongea ung’eng’e hapaniki, kubukanya wala kumiminikwa na jasho utadhani anakimbizwa. Kisomi mchezo wa kutumia madaraka ya mzee kwa mhusika kujineemesha na jamaa zake huitwa Bedroom politics ambapo mhusika hutumia kitanda kama mtaji.
Nne, asimsumbue mzee kwa kutaka ateue ndugu au mashoga zake kwenye ulaji hata kama hawana sifa. Aache kila mtu apige msele apate cheo kwa jasho na sifa zake.
Pia festi leidi ajaye aepuke kupenda matanuzi kiasi cha kutaka kila safari anayofanya mzee ughaibuni naye awepo na mashoga zake kwenda kutoa tongo tongo. Si mmemuona rafiki yangu na mwanafunzi wangu Braaka Obamiza alivyokuja juzi Afrika. Hakuja na Michele wala Unga wala watoto wao. Siyo lazima kila anapokuwa baba na mama awepo hata kama anaruhusiwa kufanya hivyo.
Tano, festi leidi aepuke kupenda makuu kama vile kupokelewa kama mzee aendapo kwenye shughuli zake binafsi. Walevi watachagua na kumuapisha mzee tu. Hivyo, lazima rahis awe mmoja. Ufujaji tulioshuhudia usirudiwe. Maana ni aibu na ni kishawishi cha kufanya Ukiwila kama aliofanya Anna Tamaa na mzee wake ambao sasa wanaishi kwa kutegemea kulindwa na wenye ulaji kwa sasa ambao nao watategemea kulindwa na mzee ajaye.
Sita, ngoja niishie hapa niende kukamata ulabu na bangi kidogo ili kuchemsha bongo.
Muhimu, festi leidi ajaye azingatie ushauri na uzoefu wangu kama rais wa Walevi watakatifu.
Tukutane ikulu!
Chanzo: Nipashe Oct., 3, 2015.
No comments:
Post a Comment