How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday, 3 October 2015

Nitakavyomkumbuka Kikwete







            Bila shaka –bbaada ya kumaliza kuaga ndani na nje –rais Jakaya Kikwete atakuwaanafunga virago kuondoka Magogoni; tayari kujiunga na wastaafu.  Hata hivyo, kwa muda aliokaa madarakani –pamoja na mapungufu yake –kuna mambo amefanikisha kwa kiwango cha juu. Nitayataja mafanikio ya Kikwete bila kupoteza muda.
            Mosi, amefanikiwa kutimiza ahadi yake ya Maisha Bora kwa Wote. Kwani, si haba. Japo si watanzania wote wamepata maisha bora zaidi ya bora maisha, walio karibu ya Kikwete wamepata maisha bora na hata zaidi.
            Pili, amefanikiwa kutengeneza ajira. Kama hapo juu, kazi hizi zilikwenda kwa watu wake wa karibu, marafiki, waramba viatu. Na nyingi ya nafasi husika ni za kisiasa. Rejea kuunda utitiri wa mikoa na wilaya na kuwateua watu wake kwenye nafasi hizo. Akina Mihigo Rweyemamu, Paulo Makonda, wabunge wa dezo wa kuteuliwa, Mwantumu Mahiza, Amos Makala, Wilson Mashilingi Abdulrahaman Simbo, Jack Zoka, Charles Makakala na wengine watamkumbuka bwana huyu bila kusahau waandishi habari nyemelezi aliowatumia kama nepi kuwachafua wapinzani wake na baadaye kuwazawadia vyeo. Rejea kutea mabalozi nje hata wenye kutia shaka bila kusahau majaji na maafisa wengine. Nadhani aliposema atatengeneza ajira na kuleta maisha bora kwa wote wengi hawakujua wote ni akina nani.
            Tatu, amefanikiwa kupata warithi wake kisiasa toka kwenye ukoo wake. Rejea mwanae kurithi nafasi yake ya ubunge wa jimbo la Chalinze huku mkewe akiibuka kuwa mjumbe wa vikao vikubwa vya chama. Pia usisahau alivyomwezesha mke wake kuanzisha NGO na kuweza kuongeza utajiri binafsi ukiachia mbali kujenga shule ya sekondari ya wasichana kwao. Sina shaka. Huyu mama niliyeambiwa ni mwalimu wa shule ya msingi tena mwenye elimu haba atakuwa ni tajri wa kutisha kama mke wa mtangulizi wa Kikwete, Anna Mkapa ambaye alianzisha utamaduni huu wa kujitajirisha kwa mgongo wa ikulu.
            Nne, Kikwete aliingia akisifika kuwa chaguo na kipenzi cha watu. Kweli amefanikiwa katika hili hasa ikizingatiwa kuwa chini ya utawala wake wengi waliokuwa waishie gerezani kama vile wezi wa EPA, Escrow, Kagoda, Richmond majambazi, wauza unga na wengine aliwapenda kiasi cha kuwaonea huruma asiwafunge.
Tano, Kikwete alifanikiwa kuitangaza nchi nje. Hadi juzi alikuwa ameishaizunguka dunia mara 410. Japo wabaya wake walimwita Vasco da Gama, kwa vile ni mtu wa watu hakujali na aliendelea na matanuzi yake.
            Sita, Kikwete amefanikiwa kujenga barabara nyingi hata kama ziko chini ya viwango na ni chanzo cha ajali ukiachia mbali kutolinga na kiwango cha fedha zilizotumika kuzijenga.
Saba, Kikwete amefanikiwa kukuza deni la taifa kiasi cha taifa letu kuwa miongoni mwa mataifa yanayokopesheka na yanayojua kutumia fedha.
Nane, Kikwete amefanikiwa kurahisisha elimu. Rejea jinsi wanafunzi wanavyosoma vitabu vichache ili wasiumize vichwa bure wakati elimu yenyewe haina soko hasa baada ya utajiri wa mkato kupitia jinai kama wizi na uuza mihadarati kugeuka deal. Rejea alivyoendelea kuwateua mawaziri waliotuhumiwa kughushi kama vile akina Mary Nagu, William Lukuvi, Deodorous Kamala, Makongoro Mahanga, Emanuel Nchimbi na wengine wengi tu bila kutaka wachunguzwe au kuadhibiwa kama manesi, polisi, walimu na mahakimu wanaofungwa na kufukuzwa kazi kwa kosa hilo  hilo.
Nane, amefanikiwa kuwaacha wanaotaka kumchimba na kujua utajiri wake wakibunia. Kwani , kwa miongo miwili amegoma kutangaza utajiri wake.
            Tisa, amefanikiwa kukiimarisha chama chake cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwezesha kuhamwa na mawaziri wakuu wastaafu wawili.
Kumi, amefanikiwa kuandika katiba mpya ya watawala na kuachana na ile ya kizamani ya wananchi iliyokuwa ikipigiwa upatu na akina Jaji Warioba.
Kumi na moja, chini ya utawala wa Kikwete wanyama wetu walipigwa jeki kwa kupandishwa ndege kwenda uarabuni ili kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia. Rejea Tanzania ilivyopata ugeni mkubwa wa machinga toka Uchina, India, Uturuki bila kusahau wafanyabiashara hodari wa pembe za faru na ndovu.
Kumi na mbili, Kikwete alifanikiwa kuweka uwazi na ukweli hasa kuwapasha watoto wa kike wa shule wanaopata mimba kuacha kiherehere chao ili wasidungwe mimba. Huu ni mfano mzuri wa kuigwa kwa kuwa na rais mwenye uchungu na mabinti zake hadi anawapa vidonge vyao japo kufanya hivyo si jibu iwapo wanaowadunga hawashughulikiwi kutokana na mfumo mbovu.
Kumi na tatu, Kikwete alifanikiwa kutoa uhuru kwa polisi kufanya watakavyo hasa kuwakomesha wapinzani na waandishi wa habari bila kusahau kuwachapa au kuwaua wananchi wanaojifanya kujuajua.
Kwa ufupi haya si mafanikio haba hata kama yanaweza kuwa na mshikeli. Mafanikio ni mafanikio yawe hasi au chanya. Cha mno atakachokumbukwa kwacho Kikwete ni kuacha nchi kujiendesha ikiwa kwenye autopilot kwa miaka nenda rudi huku yeye akiimarisha uhusiano wa kimataifa kwa kuizunguka dunia na kuitangaza duniani.
Hivyo ndiyo –binafsi –nitamkumbuka Kikwete. Je wewe msomaji utamkumbuka Kikwete kwa yapi? Tuonane jumapili ijayo.
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 4, 2015.

No comments: