Baada ya kutokea kifo cha ghafla cha Chris Mtikila, Kijiwe kilikaa kama kamati kumkumbuka gwiji huyu wa ukombozi pamoja na utata wake. Kijiwe kilihuzunishwa na kifo cha Mtikila hata kama hakiungi mkono misimamo yake yote.
Msomi Mkatatamaa ndiye analianzisha. Anaingia akiwa na huzuni wazi wazi jambo ambalo si kawaida kwake. Anasema, “Mwenzenu nina huzuni sina mfano. Kaka Mtikila hatunaye tena. Ameaga dunia kwenye ajali itokanayo na ubovu wa sheria za barabarani na barabara pia. Kaya imepata pigo jingine baada ya lile la Mchonga.” Anainamisha kichwa kama ishara ya kuiombea roho ya marehemu.
Sofia Lion aka Kaunungaembe anakula mic, “Inasikitisha ila kifo ni jambo la kawaida kwa kila mja. Nadhani wakati wake ulifika hivyo hatuna la kufanya. Sikubaliani na kumlinganisha Marehemu na baba wa taifa. Walikuwa vitu viwili tofauti. Hata hivyo ametuachia somo kubwa kuhusiana na mahusiano yetu kama wanajamii.”
Mgosi Machungi anapoka mic, “Da Sofi acha utani. Unaongea kama vie hujaguswa na kifo cha gwiji huyu wa Saa ya Ukombozi na magabachoi. Unaonyesha wazi kuwa hukumpenda huyu gwiji sijui ni kwanini,” anamaliza sentensi huku akimtazama Kanji kwa chati.
Sofia anajibu, “Niguswe nisiguswe hili si muhimu. Nimepende nisimpende hiyo si kazi ya mtu. Kwani alikuwa ndugu yangu? Kwa taarifa yako, mimi sikupenda hotuba zake za chuki na uchochezi zilizolenga kutochonganisha na kutugawanya. Hata hivyo, nasikitika amepotea.” Anamalizia huku akitabasamu jambo ambalo linawashangaza wengi.
Mipawa anakamua mic, “Dua la kuku halimpati mwewe da Sofi. Heri yeye amefunga chake kuliko hawa wanaoshangilia kifo chake kana kwamba wao hawatakufa. Nadhani tunapaswa kumuangalia marehemu kwa yale aliyosimamia. Pia tutazame mema yake tukipuuzia mabaya. Nani ni malaika? Heri yake alisema na kuweka msimamo wake wazi kuliko wanafiki na mafisadi wanatudanganya kwa kubadili vyama kama nepi.”
Kapende anadandia mic, “Mie huyu bwana nilikuwa namkubali na ni mtu pekee aliyenitoa na kuingia mitaani na kushiriki maandamano kwa mara ya kwanza na ya mwisho miaka ile ya magabacholi aliosema wamemiliki uchumi wa kaya yetu huku sisi tukiteseka. Haya ndiyo masuala ya kuongelea au vipi?”
Msomi anarejea, “Kwanza niwapongeze kwa michango yenu ya kisomi na tekenyeshi. Ni kweli, kama alivyosema Dk Mipawa ni kwamba tusiwe na mawazo mafupi ya kujadili watu badili ya masuala. Hebu tusiwe wezi wa fadhila. Nionyeshe mwanasiasa yeyote aliyehai anayeweza kuvaa viatu vya marehemu. Tumpate wapi jasiri kama yeye? Tumpate wapi mtu aliyeweza kueleza hoja zake kwa lugha na staili vinavyoeleweka? Tuwe wakweli. Marehemu alikuwa jasiri na mwenye kuchukia upuuzi ambao umetufikisha hapa,” anakohoa na kuendelea, “Tunapomlinganisha marehemu na baba wa taifa, hatuna maana ya kumkosea yeyote heshima au kumpalilia. Tunachomaanisha ni kwamba, hata kama walitofautiana na baba wa taifa, wote walikuwa na misimamo inayoeleweka hata kama hatukukubaliana nao, walikuwa wakweli, jasiri na wajuvi wa mambo na wenye ufasaha kwa kueleza mawazo na hoja zao huku wakijua kujenga na kubomoa hoja za wapinzani wao.”
Mpemba anakamua mic, “Yakhe msemayo kweli. Hata kama twawachukia watu, wakishakufa twapaswa kuwasamehe. Mie huyu bwana aliniudhi sana pale aliposema eti nasi ni magabacholi wakati ni wanakaya. Hata hivo, namsamehe sana na kumuombea maghufira aamin. Hakuna haja ya kushangilia mauti ya mwenzio. Kullu nafsin zaikatul maut, kila mtu yatamfika mauti.”
Kanji anachangamkia mic, “Mimi iko penda sana yeye Tikila. Hapana chukua ile yote nasema. Yeye nasema moja kwa moja. Iko nyingi nachukia sisi lakini hapana sema wazi wazi. Mie iko penda adui naambia mimi kuliko ile nacheka na mimi.”
Mheshimiwa Bwege anakula mic, “Kama alivyosema Profesa Msomi, hebu tuwe wakweli. Kweli dhambi ya marehemu unaweza kuilinganisha na majambazi kama Rugemalayer au hawa wanaotuhadaa tuwachague wakati walishatutesa kwa kutuibia sana? Nadhani marehemu alikuwa msemakweli hata kama ana utata wake. Angalau yeye alisema wazi wazi kuliko wanaoficha na kututapeli. Saa ya Ukombozi ni sasa.”
Mzee Maneno anakamua mic, “Nyinyi hamjui. Marehemu alikuwa mshirika na mshauri wangu wa karibu ingawa sijawahi kuwaambia hili. Tulishauliana mambo mengi kuhusiana na ukombozi. Hivyo kifo chake kimenitia simanzi ajuaye Mungu mwenyewe. Ni muhimu tumsamehe na kusimamia yale aliyosimamia tunayoona yana maana katika maisha yetu.” Baada ya kumaliza kuongea tunaangaliana kama kuonyesha kuwa hili la marehemu kuwa mshauri wa mzee Maneno ni kama changa la macho.
Wakati tukiwa tumebung’aa na kuangaliana, Msomi anakula mic tena, “Mie nadhani huyu bwana alikuwa mtu wa watu kwa kiasi kikubwa. Kuna kipindi alikuwa na msimamo si kawaida ingawa baadaye alilainika. Hata hivyo, sijui kilichomlainisha ingawa kipindi hiki alikuwa amerejea upya kuonyesha msimamo wake dhidi ya harakati za mafisadi kutaka kututawala.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si tukaona msafara wa magari yaliyosindikiza mwili wa marehemu ukifika. Wote tulifunga kijiwe na kuelekea Diamond Jubelee kumuaga shujaa huyu wa walalahoi na kiboko ya magabacholi na mafisadi.
Chanzo: Tanzania Daima Okt., 14, 2015.
No comments:
Post a Comment