Hivi karibuni rais John Magufuli aliwafurahisha watanzania kiasi cha kuwaaminisha kuwa ufisadi hauna nafasi katika nchi yetu. Ni baada ya kuchukua hatua za makusudi na za kupongezwa za kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa kashfa ya wizi wa mabilioni ya fedha toka kwenye fuko la Escrow. Kimsingi, hatua hii adimu na adhimu ilizidi kuongeza imani ya umma kuwa kumbe hakuna asiyeguswa japo bado wapo marais wastaafu ambao serikali zao ziliingiza kampuni la Independent Tanzania Power Limeted (IPTL) ambalo ndiyo mama wa wizi na uhujumu huu.
Tokana kuanza kuishughulikia kashfa ya Escow kisheria, wengi wanaamini mwisho wa yote mkono mrefu wa sheria utatua IPTL. Pamoja na hatua hii ya kutia moyo, wengi wangetaka rais Magufuli aende mbali na kuwakamata watuhumiwa wengine ambao walihujumu taifa na kuliingiza hasara ya mabilioni ya shilingi. Leo, bila kuficha wala kumung’unya, tunamkumbusha rais Magufuli kuwa bado kuna kashfa nyingine kama vile Lugumi ambapo kampuni iitwayo Lugumi Enterprises Limited inadaiwa kupewa tenda na jeshi hilo kwa ajili ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole – ‘Biometric Access’ katika vituo 108 nchi nzima kwa gharama ya Sh bilioni 37. Mpaka kashfa yenyewe inaibuka Lugumi iikuwa imefunga mashine katika vituo 14 pekee wakati ilikuwa tayari imeishalipwa Shingili bilioni 34 ambazo ni sawa na asilimia 99 ya fedha zote za mkataba. Kuna haja ya kuchunguza mazingira na sababu za kufanyika kwa malipo haya kwa kampuni ambayo ilikuwa haijafanya kazi yoyote ukiachia mbali kuchunguza historia ya kampuni ya Lugumi na wamilki wake.
Je, kama hakukuwa na namna, ilikuwaje kampuni hiyo ikapewa malipo ya asilimia 99 bila kuwa imetekeleza angalau asilimia sawa za kazi iliyokuwa iifanye? Maana, kiakili na kisheria ni jambo lisilowezekana bila kuwa na namna yoyote haramu ya kupinda au kuvunja sheria. Je Lugumi ni kikaragosi kilichotumiwa na wakubwa fulani kuliibia taifa?
Kuna taarifa ambazo hazijawahi kupingwa kuwa Lugumi ni mkwe wa kigogo mmoja wa polisi ambaye ameishastaafu. Je hii haiwezi kuwa clue ya kutufikisha kwa Lugumi mwenyewe? Kutelekezwa na kutotekelezwa mradi mzima ni hasara kubwa kwa taifa kifedha na kiusalama.
Je ni makosa mangapi ambayo serikali ililenga kumpambana nayo yalitendeka baada ya Lugumi kutofunga vifaa husika?
Mbali na Lugumi, kuna kashfa nyingine ambayo nayo ni tata; na ililisababishia taifa hasara ya mabilioni ya shilingi sawa na kashfa tajwa hapo juu. Kashfa hii si nyingine bali ya utwaliwaji wa iliyokuwa Kampuni ya Uchukuzi Dar Es Salaam (UDA). Kwa wanaojua historia ya kashfa hii ni kwamba UDA ilitwaliwa na kampuni ya Simon Group kinyume cha sheria na kwenye mazingira yenye utata kuhusiana na namna kampuni ilivyouzwa huku serikali ikikana kuwa hisa zake zilikuwa bado kuuza hisa zake. UDA ilikuwa ikimilikiwa na Halmashauri ya Jiji na serikali kwa uwiano wa hisa 49 (Serikali) kwa 51 (Jiji la Dar Es Salaam). Ajabu ya maajabu hata hisa za Jiji hazionyeshi namna zilivyouzwa. Hakuna ushindani uliofanyika kama sheria ya manunuzi ya umma inavyotaka. Je ni kwanini utaratibu ulikiukwa? Kama Lugumi, mmilki wa Simon Group, Simon Kisena ni mtu wa kutia shaka ambaye hana historia inayoeleweka kibiashara ukiachia mbali kutuhumiwa kuhujumu viwanda vya usindikaji pamba ambao ulimlazimisha rais Magufuli kutoa amri virejeshwe kwa umma huko mkoani Mwanza. Je, kama Lugumi, Kisena ni wakala wa wakubwa au jamaa zao ambao hawataki kujulikana? Hapa napo kunapaswa kufanyika uchunguzi kujua kilichoko nyuma ya pazia kama ilivyo kwa Lugumi.
Kwa vile rais Magufuli amepania kurejesha uwajibikaji na heshima katika utumishi wa umma ikiwamo kuhakikisha mali na raslimali za umma zinaunufaisha umma, tunaamini kuwa ni wakati muafaka kumkumbusha kuwa na kashfa tajwa zishughulikiwe ili taifa lisiendelee kuchezewa na kuhujumiwa kiasi cha kujidhalilisha kwa kuombaomba na kutegemea uhisani wenye masharti magumu udhalilishaji vya hali ya juu. Kwani, haiingii akilini taifa liendelee kutoa huduma muhimu kwa umma wakati linaachia mali na raslimali zake kuhujumiwa na kundi dogo la mafisadi na wezi. Kazi ya serikali yoyote duniani ni kuwalinda wananchi wake na mali na raslimali zao. Isitoshe, serikali inavyo vyombo na asasi za kuweza kushughulikia kadhia kama hizi ambavyo watumishi wake wanalipwa mabilioni ya shilingi ya kodi za wananchi. Kama vyombo hivi na serikali wanashindwa na genge dogo la wachache, nini maana ya kuaminiwa na kulipiwa na umma?
Tumalizie kwa kumtaka rais Magufuli na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wajielekeze kwenye kadhia hii ili kuepusha upotevu wa fedha za umma ukiachia mbali uhujumu wa taifa. Kama alivyowahi kusema rais Magufuli, wakati wa Tanzania kuwa shamba la bibi umekwisha. Hivyo, Lugumi na Simon Group wanapaswa kuunganishwa na wenzao wa Escrow ili haki itendeke kwa pande zote ukiachia mbali kuonyesha seriousness ya rais Magufuli ya kupambana na uoza. Kwa leo tunaishia hapa.
No comments:
Post a Comment