Baada ya kuupiga na kujifanya Mike Tyson si nikamvamia bi Mkubwa wangu. Wajua kosa lake nini? Kunipikia miugali badala ya wali. Kosa jingine? Kuhoji kwanini nataka apike pilau wakati sikuacha mshiko hata senti. Nami bila kujua; nilikuwa nimeutwika; si nikamkwida huku nikimrushia mingumi mizito lau kuonyesha undavandava wangu kama nyamaume nisijue naye mrume wa nguvu! Ghafla bin vu alinivuta na kuniangusha chini huku akitua juu yangu na kunikalia. Nilizoea kumuangukia na kumlalia asilalamike nikiwa nimelewa. Bi Mkubwa mwenyewe ni Tunituni fulani aliyejazia. Acha anishindilie mingumi huku jasho likinitoka. Baada ya kugundua kuwa angeweza kuninyotoa roho, ilibidi nijikaze kike ili asijekuniua kiume.
Baada ya kuzidiwa ikabidi nimuombe msamaha. Naye bila kusita, alisitisha mashambulizi akiomba nimtambue kuwa yeye ni mwanaume; nami ni mwanamke. Nami bila kusita nilimwambia “kweli wewe ni mwanaume tena wa shoka kama Akashia.” Kana kwamba haitoshi, aliniamuru niseme “mimi kweli ni mwanamke.” Nilisita kidogo; na kichapo kikazidi. Kuona huyu mrumejike; tuseme jikedume angenyotoa roho, ikabidi mwishowe niamue kurudia maneno yake na kumwambia mke wangu “mimi ni mwanamke; nawe ni mwanaume.”
Sasa turejee mantiki ya somo nililojifunza kwenye ubaguzi huu wa kilevi, kijinga na kijinsia. Hivi, tunaposema fulani ni mwanaume tukimaanisha shujaa tunatoa picha gani kwa akina mama? Je kuna aliyejiumba au kutuma maombi aumbwe alivyo? Je kama mafanikio au ubabe ndiyo ushujaa au uanamume, kuna wanawake wangapi ni wanaume bila kusahau wanaume ambao ni wanawake tokana na kushindwa na wale wanaowaona kama jinsia dhaifu kulhali kuanzia ubabe wa kifedha, kiakili hata kimituringa kama nilvyofanyiwa na Bi Nkubwa wangu ambaye namheshimu kuliko mwanzo? Je hapa tunajitukana kijinsia ili kupata nini? Hivi mama yako angekuwa mwanaume ungezaliwa na huo udume wako uchwara?
Ugomvi wangu na bi Mkubwa ulinikumbusha baadhi ya watuhumiwa wa kunufaika na fedha za Escrew ambao walimtishia mbunge wa Kigoma Mashariki David Kafulila kuwa kama angekuwa mwanaume alipaswa aende kuwashutumu nje ya Mjengo. Wengine walimwita tumbili alipowaita wezi. Sijui kwa usawa huu, hawa wanaume siyo “wanawake” kweli baada ya kuumbuka? Na wanawake ambao wamekuwa wakilipa kodi ili wao waescrow siyo wanaume wa shoka kuliko wao wanawake wa hovyo?
“Mwanaume” gani anaiba fedha ya kodi na akaendelea kuwa “mwanaume?” Je kuna anayeutaka uanaume wa maovu kama jamaa zetu waliozoea kutuibia madini yetu kwenye michanga halafu tunawaita wezi kabla ya kubadilisha kibao na kuwaita wanaume. Je kweli hapa mwanaume ni nani kati yao nasi? Je mwanaume wa kweli hapa ni yupi kati ya yule anayeiba au kunyonya na wale anaowaibia au kuwanyonya ukiachia mbalil anayemsifia ujinga? Sijui mwanaume hapa ni yupi kati ya mwizi aliyemweka sawa aliyemwibia au aliyeibiwa akaanza kumvisha uanaume mwizi wake simply because amemuahidi kushirikana naye kumrejeshea kidogo? Je kuna wanawake wanaume wangapi na wanaume wanawake kiasi gani duniani katika hali hii?
Baada ya kuwa nasikia ujinga huu mara kwa mara tena toka kwa watu ambao hukutegemea ukiangalia nafasi na elimu zao, leo nimeamua kutumia PhD yangu ya ulevi kuwashukia hawa wabaguzi wa kijinsia ambao kwa kisukuma huitwa misogynists kama siyo mishongezi wa kijisia kwa kisambaa. Kama mnaona uanaume ni mali kuliko uanauke kwanini mnawawowa na msiwowane tukawajua nyinyi ni nani?
Hivi kama uanaume ni ushujaa, hivi mimi na bi Mkubwa wangu aliyenikung’uta nani mwanaume? Au tuseme mimi ninayemkopa bi Kotilde muuza kanywaji nisimlipe nani mwanaume? Kama uanaume ni mali mbona hatuoni mkiuuza mitaani lau wote tuwe vidume? Acheni ushamba na ulimbukeni na udhalilishaji kijinsia. Wote tunategemeana kama alivyonichapa bi Nkubwa wangu. Wakati mwingine huwa nanchapa; wakati mwingine ananigeuzia kibao. Tunchapana kuonyesha usawa; na maisha ndivyo yalivyo. Dume la leo laweza kuwa jike la kesho na kadhalika kama udume ni ubabe, ufanisi, mali, ushujaa, umaarufu na mambo mengine mengi.
Leo namaliza kitakatifu nikimkariri rafiki yangu na ndugu yangu mwana wa Adam aliyeuliza “kama mwili wote ungekuwa sikio, jicho lingekuwa wapi?” Je kama wote tungekuwa wanaume, wanawake wangelikuwa wapi; na kama wote tutakuwa wanawake, wanaume watatoka wapi? Tafakarini.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.
No comments:
Post a Comment