Baada ya kuona maigizo yakizidi kuibuka hapa na pale na kila siku, kijiwe kimeona kijipe jukumu ambalo wengi wanaonekana kuliogopa yaani kukumbushia wenye madaraka juu ya jinai ya kuvamia kwa kituo cha runinga cha Klouds.
Kapende anaingia na gazeti la sirikali la Mizengwe. Kwanza, kila mmoja anamshangaa kuona anapoteza njuluku kwenye gazeti linaloandika mapambio na habari za upande mmoja. Kama aliyesoma mawazo yetu anasema “najua wengi mnadhani fyuzi huku juu zimeungua hadi naanza kutupa njuluku kwenye gazeti kama hili. Kuna kitu kimenigusa baada ya kukisoma humu. Mna habari kuwa kuna kankakati ka kuzuia wachovu kufikiri?”
Kabla ya kuendelea Mgoshi Machungi anakula mic “Mgoshi hii kai kwei kwei eti tizuiiwe kufikii! Thubutu yako. Kama hivyo basi watiuue lakini hawatafanikiwa kufunga bongo zetu waa kuzizuia. Mbona sisi hatiwazuii kufikii tena hata pae ushahidi unapoonyesha wanafikii vibaya kama waivyoingia mikataba mibovu ya makinikia bia umakini?”
Kabla ya Mgoshi kuendelea Mijjinga anampoka mic “mwenzenu nalimiss gazeti la Asubuhi lilivyokuwa likipaka kinomi. Mna habari hata ile stori ya mpuuzi mmoja aliyelewa ulaji hadi akaharibu shamba la kiongozi wa wapingaji nilizinyaka mle? Tena umenikumbusha. Hivi uchunguzi na matokeo ya uvamizi wa kituo cha Klouds vimeishia wapi au ndiyo hayo ya kutaka kutufunga hata vinywa, akili na utashi? Sijui jamaa wanagwaya nini au nao wana mambo yao nyuma ya pazia?”
“Mwanangu unaongelea habari za Klouds na za mshamba mmoja kuharibu shamba la mwenzie! Unategemea nini kujikomba na kujigongagonga vinapogeuza sera? Unategemea nini wahuni wanapopewa nyadhifa za heshima au waishiwa kuitwa wahishimiwa? Kama imezimwa na kuuawa kashfa ya Bashite kiasi cha kusimamisha zoezi la kuwasaka na kuwashughuliki vihiyo na mabashite wenzake walioghushi nini Klouds? Hii Bongolalaland ndugu yangu.”
Msomi Mkatatamaa ananyakua mic “nadhani hapa tatizo ni kufanya mambo kizimamoto kama siyo kwa nguvu ya soda. Kama ukifuatilia kwa makini na si makinikia, ni jambo gani walilosimamia kuanzia mwanzo hadi mwisho? Hukumsikia dingi anasema kuwa pamoja na kutumbua vibaka na mibaka ya bandarini bado wanapiga dili hadi kushushwa vichwa kumi vya treni hivi karibuni na wasistuke? Hapa bila kunyonga mafisadi na kupambana na ufisadi bila kuangalia ubashite na upuuzi mwingine, tunatwanga maji kwenye kinu tukitegemea kupata unga.” Anapiga chafya mara tatu na kuendelea “bila kubadili mfumo, hata hawa wanaoonekana wana udhu watachafuliwa au kubadilishwa. Hivyo jibu ni kubadili mfumo au kubadilishwa na mfumo ikawa business as usual. Mara hii mmesahau Tunituni bingwa wa uvuvi wa kufikiri alivyoingia kwa gea kali akaondoka akiwa ameishabadilishwa na mfumo baada ya kushinda kuubadili?”
Mipawa aliyekuwa akivuta sigara kali anampasia Mzee Maneno kipisi na kudema “nadhani sisi tuna tatizo moja. Kwanini tusiandike barua ya kumbushio na kuipeleka wenyewe kwenye ofisi ya waziri kuhusiana na hii jinai ya Klouds ili tuone atachukua hatua gani ili tupange nasi za kuchukua zaidi.”
Kabla ya kuendelea mheshimiwa Bwege anamchomekea “atachukua hatua gani wakati ameishachukua hatua?”
Mipawa anauliza kwa mshangao “amechukua hatua gani mbona sikuelewi?”
Mheshimiwa Bwege anajibu “amechukua hatua ya kutochukua hatua kwani hiyo siyo hatua? Wewe ulitegemea nini kesi ya ng’ombe inapopelekwa kwa nyati au ya kobe kwa kasa? Wenye akili tulishajua hasa tulipoona waliogushi wa chini wakiadhibiwa vikali wakati wa juu wakikingiwa vifua hata kwa aibu ya wazi. Inashangaza; sijui wanapata faida gani kwa nafasi zao!”
Kanji anakula mic “hii Shite iko tumia dava bwana. Kama ile natoa dava kwake iko boko kweli kweli. Maana nakinga yeye fua kama wile yeye iko toto ya muungu. Hapa iko kitu kuba sana takuja sema siku moja. Hapana vezekana hii ive bure.”
Mpemba anaamua kutia guu “Kanji wallahi nami nkubaliana nawe. Hapa lazimu kiwepo kitu tena kikubwa sana. Maana, ukiona namna habari yenyewe ilivotangazwa na huku mwenye akikomaa unashangaa sana. Ingekuwa Pemba au Mombasa ungesikia mengine.”
Mgoshi anadandia “unamaanisha nini au yae ya popobawa?”
Mpemba anajibu “hayo unsema wewe. Mie nasema kama Pemba wasema hapa lazima kuna msukule. Maana huyu alovamia Klouds angekuwa ntu kweli basi ndata weshamnyaka; na angekuwa korokoroni angojea nyolewa bila maji.”
Sofia Lion aka Kanungaembe aliyekuwa akiteta jambo na Mchunguliaji anaamua kula mic “sasa mmesema mengi. Hiyo barua ya kwenda kwa waziri inaandikwa lini ili tujiandae kuipelekea? Pia ningeshauri iandikwe nyingine kwa waziri mwingine kukumbushia vita dhidi ya walioghushi maana naona kama inasahaulika. Hatuwezi kuendelea kufanya mambo kizimamoto. Kama wao wamesahau au kujisahaulisha, basi acha tuwakumbushe lau wajue kuwa tunafuatilia movie wanazoleta bila kusahau mambo muhimu yaliyopita.”
Kijiwe kikiwa kinaanza kunoga si kunguru akamnyea mzee Maneno. Acha atukana huku wengine tukiruka kuepuka ndege huyu mwanaharamu asituharibi viwalo vyetu.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.
No comments:
Post a Comment