The Chant of Savant

Sunday 9 July 2017

Kumpinga rais au serikali si jinai

            Hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari viliingia utatani hadi vingine kufungiwa huku wanasiasa na wakosoaji wakipewa onyo kali kuacha ima kuipinga serikali au rais. Tukio la hivi karibuni ni pale rais John Pombe Magufuli alipoamuru polisi kuwakamata wote wanaohoji baadhi ya mambo anayofanya kama vile kushindwa kudhibitiwa kwa mauaji ya Kibiti, upelekaji bungeni mikataba ya haraka bungeni, hata baadhi ya hatua anazochukua kuhusiana na mambo mbali mbali kama vile uhuru wa vyama vya siasa kufanya siasa.
            Tokana na utata huu–ambao wengine huuona kama uimla–kuna haja, kama taifa, kukaa pamoja na kukubaliana namna ya kuendesha nchi yetu hasa vita dhidi ya uhujumu wa taifa na tishio dhidi ya usalama wa raia. Hivyo basi, leo nitadurusu mambo muhimu ambayo pande zote zinapaswa kuzingatia kama ifuatavyo:
Mosi, Tanzania si mali ya rais, serikali wala chama tawala. Ni mali ya watanzania wote kwa usawa. Hivyo, kila mtanzania ana uwezo wa kuamini aonavyo ilmradi asivunje sheria. Kwani, kwa mfano, wanaohoji mambo hayo hapo juu, hawatendi kosa lolote hasa ikizingatiwa kuwa kila binadamu amejaliwa uhuru na uwezo tofauti wa kuyadurusu na kuyaelewa mambo.  Hivyo, kutishiana kukamatwa na polisi si jibu wala njia sahahi kwa mustakabali wa taifa letu. Tupingane kwa hoja na si vitisho wala kutumia misuli ya dola.  Baba wa taifa Mwl Julius Nyerere alituachia tunu tatu kuu. Moja uvumilivu, pili, kujibu hoja kwa hoja kwa njia ya majadiliano, na tatu uadilifu. Kimsingi, uadilifu ni sehemu mojawapo ya kuwathamini wengine na michango yao na si juu ya mali wala fedha tu.
            Pili, matumizi ya vyombo vya dola kunyamazisha wakosoaji ni uvunjaji demokrasia jambo ambalo ni jinai bila kujali anayelitenda ni nani au ana cheo gani. Kwani, kama nilivyoeleza hapo juu, kila binadamu amepewa ubongo afikiri atakavyo na kuhoji na kujibu anachojua au kutilia shaka. Hapa lazima tuelewe; kama mtu anasema uzushi, tunampa ukweli lakini si kumnayamazisha. Tunaweza kuwafunga wakosoaji hata magezeti lakini hatuwezi kufunga akili na vinywa vyao.
            Tatu, kwani rais na serikali yake hawakosei? Rais ni binadamu na serikali yake inaendeshwa na binadamu. Sijui, kwa mfano, serikali inapata wapi jeuri ya kutaka kuwanyamazisha wapinzani wanaohoji miswaada ya sheria chini ya hati ya dharura bungeni wakati ni miswaada na staili hiyo hiyo iliyosababisha kutungwa sheria mbaya za kifisadi hadi Tanzania ikawa inaibiwa mchana kweupe? Je ni serikali ya chama gani iliyoingia upuuzi huu kama siyo hii hii iliyoko madarakani? Hivi kuhoji huyu roho mtakatifu alipotekea nalo ni kosa au tunapenda kurudia makosa tu bila sababu? Nani amesahau wabunge kama David Kafulila, John Mnyina na Zitto Kabwe hata walivyofurushwa bungeni kwa kupinga sheria mbovu zinazobadilishwa kwa sasa? Hawa nao wanyamaze wakijua wazi kitakachotokea baada ya kufanya mambo kwa kukurupuka? Kama tumeibiwa miaka 20 tukavumilia–japo si jambo jema–inakuwaje tukurupuke kama tulivyokurupushwa na waliobariki huu ufisadi? Nadhani shughuli za taifa si za kuaminiana tu bali kutiliana shaka na kuchunguzana. Na isitoshe, hizi siyo zama za chama kimoja na zidumu fikra za mwenyekiti.
            Nne, kama wabunge wanaowawakilisha waliowachagua kufanya hivyo wametumwa kusema wanayosema, inakuwaje mnawatisha na kuwafukuza kama mtu mmoja wakati wanawakilisha wale waliowatuma? Sasa nini faida ya kuwa na wabunge kama wabunge wote wanapaswa kuwa ndiyo mzee? Naungana na baadhi ya wabunge waliosema kuwa badala ya kuwatisha na kuwaona kama maadui wa taifa, basi tubadili katiba na kuendesha nchi kwa chama kimoja bila kujali kuwa kile kilichotufanya tutoke huko bado kiko pale pale au tunataka tuendelee kulazimishwa na wazungu namna ya kuendesha nchi yetu kutokana na kutokubaliana na baadhi ya mambo? Mfano, nani amempa rais mamlaka ya kujadiliana na kampuni ya Barrick huku vyombo vya dola vikiigwaya kampuni inayotuhumiwa ya Acacia? Je hili pekee halionyeshi kuwa tunaanza vibaya kumdai mtu ambaye huna mkataba naye eti kwa vile ni mbia wa aliyekuibia? Ni sheria na busara gani hii jamani?
            Kwa waliosoma Migogoro na utatuzi wa migogoro (Conflict Resolution Studies) wanajua fika kuwa katika mgogoro wowote lazima kuwapo na watu au makundi zaidi ya moja yanayogombea hiki moja au parties to conflict. Hawa wanaweza kujiwakilisha kwenye majadiliano na wataalamu wa eneo husika lakini hawawezi kujivua uhusika. Mfano, ukiwa na ugomvi nami, siwezi kuwakilishwa na mke wangu kama party to conflict vinginevyo aje kama mtaalamu au mteuliwa tu asiye na uwajibikaji kisheria bali kukusemea tu.
            Tumalizie kwa kuitaka serikali itambue kuwa hata wanaoipinga, licha ya kuwa na haki kufanya hivyo, wana akili sawa na hawa wanaowapinga. Pia wafahamu na kukubali kuwa wanapingwa tokana na historia yao yaani kuingia mikitaba mibovu. Na mwisho, wao si Mungu asiyekosea; ni wanadamu tu wa kawaida. Wangekuwa hawakosei wala wasingekosea kwa madudu yanayotuhangaisha kama taifa.
Chanzo: Tanzania Daima J'pili leo.

No comments: