Akiwa mkoani Geita, rais mstaafu Benjamin Mkapa alisikika akitoa somo la maendeleo na uwajibikaji. Alikaririwa akisema “kila siku utawasikia watu wanadai haki, makongamano, midahalo ya kudai haki, swali la kuwauliza wao je, wametimiza wajibu kama watanzania.” Kutimiza wajibu ni kuwajibika. Je Mkapa aliwajibika alipoaminiwa urais au kujinufaisha, familia, marafiki na waramba viatu wake? Historia ina jibu sahihi. Hisani huanzia nyumbani; wahenga walinena. Je Mkapa–kama atakuwa mkweli kwa nafsi yake na watanzania–ametimiza wajibu gani kama rais na raia wakati wa kubinafsisha viwanda na raslimali zetu au kujitwalia nyumba na mali za umma kama Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira? Je Mkapa anadhani watanzania wamesahau au kusamehe? Je Mkapa amesahau tokana na uzee au ujuaji?
Mkapa aliyasema aliyosema na matusi mengine alipokwenda kukabidhi nyumba nyumba 50 zilizojenga na taasisi yake. Si jambo baya kuchangia maendeleo ya taifa kwa mtanzania yoyote hasa kiongozi kama Mkapa kama kufanya hivyo kunatokana na utashi na historia iliyotukuka. Mfano, mwalimu Julius Nyerere hakujenga nyumba hata moja; kupitia uwajibikaji wake binafsi, alitoa mchango mkubwa kwa taifa kuliko kitu chochote anachoweza kutoa binadamu.
Tukimrejea Mkapa, wanaojua historia ya utawala wake ulivyoiingiza nchi kwenye matatizo makubwa kiuchumi kutokana na uwekezaji usio makini na uhujumu wa wazi wa taifa, ubinafsi, ufisadi, ulafi na maovu mengine, wanashangaa anapopata jeuri hii kuwazodoa wenzake wakati anayepaswa kuzodolewa ni yeye kwanza? Je ni yale ya wahenga kusema kuwa nonihino haoni nonihino lake? Je Mkapa anadhani kujenga nyumba 50 kutafanya watanzania wasahaua namna alivyoasisi utawaliwaji wa nyumba za umma jijini Dar Es Salaam tena zenye thamani kubwa kuliko hizi anazojenga mikoani? Kama kuwajibika anakosema Mkapa anamaanisha, kwanini asirejeshe hizo nyumba za umma?
Japo ni kweli kila mtanzania anapaswa kuwajibika, je Mkapa aliwajibika vilivyo tena akiwa rais? Je Mkapa anawajibika sasa kashfa zake zinapofumuliwa kiasi cha kutegemea hisani na ulinzi wa rais? Kama kuwajibika ni dili–na Mkapa anataka wote wawajibike–mbona yeye hawajibiki kwa angalau kutolea maelezo kashfa zake kuanzia ANBEN, NBC, Kiwila, Tanpopwer na nyingine ambazo ima alihusika moja kwa moja au kwa njia nyingine? Heri Mkapa angejinyamazia kuliko kujivua nguo akidhani yake yameishasahulika wakati aliyatenda juzi tu? Je Mkapa anadhani watanzania wamesahau yake au anadhani bado wanaishi zama zile akiwatukana kuwa ni wavivu wa kufikiri asijue naye ataishia kuwa bingwa katika hili?
Kwanini Mkapa ameshindwa kujua suala jepesi kuwa kudai kutendewa haki kwa watanzania si jambo la kutegemea huruma ya mtu yeyote? Mbona lipo kikatiba? Mkapa anaonekana kujichanganya pale anaposema “viongozi tubuni miradi ili kujiendeleza na kujiletea maendeleo sisi wenyewe.” Hivi hawa wanaozuiliwa kufanya hata mikutano ya kawaida ya siasa, watapata wapi namna ya kubuni miradi wakati wao si chama tawala? Sijui kama Mkapa anasoma magazeti au anajifanya kutojua kinachoendelea nchini kuhusiana na upinzani. Mbona kitendo cha juzi kilichotendeka pale kwa wakwe zake hakukilaani ambapo shamba la mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (CHADEMA) liliharibiwa na mkuu wa wilaya hiyo Gelasius Byakanwa? Je Mkapa anajifisia kuwa na taasisi yake ambayo nayo ukiichunguza mchango wake kwa taifa na kwake binafsi unaweza kukuta ni kama mali binafsi? Nadhani Tanzania–kama akina Mkapa wangeiendesha vizuri–haikupaswa kuhitaji misaada wala uhisani wa vitu vidogo kama nyumba 50 anazoonea fahari Mkapa badala ya kuonea aibu tokana na namna nchi inavyoibiwa tokana na uhovyo wa sera za akina Mkapa za kujihudumia. Hatuoni akina Obama wakijiingiza kwenye umachinga kama huu zaidi ya kuwa chemic hemi ya fikra kwenye ustaafu wao.
Wanaojua utajiri tuliojaliwa uliofujwa na kuhujumiwa, haiingii akilini kujipiga kifua kwa kujenga vijumba 50 wakati makampuni ya kigeni yakiondoka na matrilioni ya shilingi kwenye nishati na madini ambavyo akina Mkapa walihujumu ili watanzania waendelee kuwa maskini waje kuwafadhili kwa udohoudoho kama vijumba 50. Kwa wanaojua Mkapa alivyopoteza fursa kubadili taifa, wanashangaa wapi anapopata ujasiri huu wa kujidanganya na kuamini anaweza kudanganya wengine. Nani hajui kuwa baadhi ya waliokosoa ufisadi na utendaji wa kifisadi wa Mkapa wengine walifutiwa uraia? Nani amesahau Mkapa alivyozodoa vyombo vya habari kuwa havina haki ya kumsema kuhusiana ufisadi kwa vile naye alidhani vilikuwa vimepata mitaji yake kifisadi? Kuonyesha kuwa Mkapa aidha amesahau au anajifanya kusahau, amerudia uvivu ule ule aliowatuhumu watanzania kuwatukana wakosoaji wa rais Magufuli kuwa ni wapumbavu bila kutoa ushahidi wowote wa kisomi na kisomi. Kwani Magufuli ni Mungu asiyekosolewa? Kwa umri wake na nafasi aliyowahi kushika nchini, kama Mkapa asingejichafua tokana na ima uvivu wa kufikiria au uroho, asingekuwa mtu wa kutegemea kulindwa na rais Magufuli ambaye ni junior kwake. Rejea Magufuli alivyokaririwa hivi karibuni akisema tuwaache akina Mkapa wapumzike baada ya baadhi ya wabunge wa upinzani kutaka wafuitiwe kinga wakipata cha mtema kuni. Tuliona hili kwa Mwl Julius Nyerere. Hakujigonga kwa aliyemfuatia yaani Ali Hassan Mwinyi wala Mwinyi hakujigonga kwa Mkapa tokana na kujijengea maisha ya kuheshimika bila kuhitaji kukingiwa kifua. Alikaririwa akisema kuwa “mwenyekiti Msukuma ameniunga mkono kuwaita wapumbavu…” sijui hapa upumbavu ni upi kati ya wale waliokosolewa wakawatukana wakosoaji wakaingia mikataba ya kipumbavu ambayo inamhangaisha rais kiasi cha kusema wazi kuwa viongozi waliuza nchi kwa kuwekewa chao Ulaya. Sijui kama Mkapa anajua kuwa rais anapolalamikia viongozi waliouza Tanzania naye ni mmojawapo.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.
No comments:
Post a Comment