The Chant of Savant

Sunday 23 July 2017

Magufuli atafanikiwa kutumikia mabwana wawili?

Image result for photos of magufuli kikwete and mkapa
            Akiwa ziarani mkoani Geita rais John Magufuli alisikika akilalamika na kuwataarifu wananchi namna baadhi viongozi wa ngazi za juu waliomtangulia walivyokuwa wameiuza Tanzania kwa kuwekewa chao kwenye mabenki huko Ulaya kama alivyosema. Kwa wanaojua namna Tanzania ilivyozamishwa kwenye ufisadi na uhujumu vya kutisha baada ya baba wa taifa Mwl Julius Nyerere kuachia ngazi wanajua aliowalenga Magufuli.  Alisema “mimi ni Yohana ninayeandaa njia… ndiyo maana nimejitoa… kwani mimi si ningeweza kuwekewa changu Ulaya? Hapa bila shaka wote waliohusika wanajulikana na kujijua ingawa wengine wanajitahidi kumkubali na kumsifia kwa kuanza kusafisha nchi waliyoichafua.  Hata hivyo, wapo wanaoanza kuhoji ithibati ya Magufuli hasa baada ya kutamka hadharani kuwa baadhi ya watangulizi wake wanaotuhumiwa kujihusisha na hujuma na ufisadi huu waachwe wastaafu kwa amini badala ya kufikishwa mahakamani; kama ambavyo baadhi ya watanzania walimtaka afanye. Je hii inaleta picha gani kuhusiana na ithibati ya Magufuli katika kutenda haki bila upendeleo?
            Magufuli aliongeza kuwa kwa kuogopa kufanyiwa hila, hataki kusafiri. Anakaa nchini ikuwatumikia wananchi.  Alikaririwa akisema “ndiyo maana sitembei, nikienda huko watafanya ya ajabu, ngoja nidili na nao kwanza, lazima nihakikishe nasafisha kwanza.” Hii inaonyesha kuwa Magufuli anaongoza nchi peke yake. Maana, kama ingekuwa si hivyo, basi asingehofia kusafiri. Pia, hii inaonyesha Magufuli hawaamini wasaidizi wake; na wala hawapi fursa ya kumsaidia. Maana kama angekuwa anawaamini asingehofia kutokuwapo kwake tena kwa siku chache kungesababisha hujuma. Hii maana yake ni kwamba wasaidizi wa rais wapo pale bila imani ya bosi wao. Pia, hii inaonyesha kuwa wasaidizi wa Magufuli hawana wanachomsaidia zaidi ya kuziba nafasi tu na kupokea mishahara na marupurupu bila sifa ya kuweza kumsaidia kuutimikia umma.
            Wakati akiyasema haya, Magufuri kabla ya hapo alikuwa amekaririw akiwataka watanzania kuwaacha marais wastaafu wapumzike; kwani walifanya kazi kubwa mojawapo ikiwa ni kumwezesha kufikia alipofikia. Je hili ni jambo la kujisifia na kuwasifia wahusika au Magufuli anawapiga vijembe kuwa uzembe wao ndiyo umemfikisha hapo alipo kama rais tena mwenye kusifika dunia nzima kwa kusafisha uoza hata kama ni kwa upendeleo? Maana, haiwezekani Magufuli akasema wapo viongozi wa umma wa juu waliouza nchi halafu hapo hapo akawasifia akaeleweka. Anasema marais wastaafu walifanya kazi kubwa. Kazi ipi; kama mambo yenyewe ni haya? Je Magufuli anaanza kujipiga mtama kiasi cha kujichanganya? Je kati ya uzalendo na ufisadi, Magufuli atachukua njia ipi? Je uoza alioukuta unavumilika au kuweza kukingiwa kifua; au kutafsiriwa kama kazi kubwa waliyofanya watangulizi wake? Je Magufuli anaanza kugundua makosa aliyofanya kwa kutoa matamko ya kuwalinda watu waliofanya uovu huku akijua hili linapingana na dhamira yake ya kweli ya kulikwamua na kulikomboa taifa hili lililokuwa limegeuzwa shamba la bibi kama ambavyo amekuwa akisema mara nyingi? Je Magufuli atatenda miujiza gani kufuta kauli kama hizi na kufanya kinyume chake kwa kuhakikisha kila aliyeshiriki uchafu anafikishwa mbele ya vyombo vya dola? Je, kisheria, rais anao uwezo wa kumsamehe mtu makosa ya jinai kabla ya kupatikana na na hatia akafungwa ndipo akamuachia kwa msamaha wa rais?
             Je Magufuli ataweza kuendelea kuwalinda wastaafu wanaotuhumiwa huku akiwaumbua hadharani kama alivyofanya akiwa Chato tena wengine wakiwapo baadhi yao? Je itawekezekana Magufuli kuwatumikia wanyonge kama asemavyo mara kwa mara sambamba na kuwahifadhi waliowaibia wazi wazi? Kwanini Magufuli asiwaache akina Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete n ahata Ali Hassan Mwinyi wakabeba mizigo yake wakati yeye akibeba jukumu la kuuondoa umma kwenye uoza na kero walizotengeneza wawili hawa bila sababu za msingi zaidi ya ufisadi na uroho wa kawaida tu? Nani hajui kuwa watanzania bado wanafahamu namna Mwinyi alivyohalalisha ufisadi kupitia sera yake ya ruksa. Nani hajui Mkapa alivyofanya biashara akiwa ikulu kinyume cha sheria? Rejea makampuni yake kama vile ANBEM lenye kuundwa na ufupisho wa Mkapa na mkewa Anna, Tanpower na Fosnik kampuni ya mwanae inayoundwa kwa majina yake yaani Nicholas na Foster. Rejea kujitwalia machimbo ya Makaa ya Mawe ya Kiwira kinyume cha sheria na kashfa nyingine kama vile kuhujumu shirikala la umeme la Taifa (TANESCO) na iliyokuwa Benki ya Biashara (NBC).
            Tukija kwa Kikwete, watanzania wanajua namna alivyoshirikiana na Mkapa kwenye kashfa ya EPA ambayo wanaojua ukweli wanasema wazi ilivyompa mtaji wa kupatia urais. Kikwete haishii hapa. Nani amesahau kashfa yake ya Richmond ambayo ilimlazimisha kumtoa kafala rafiki na waziri wake mkuu Edward Lowassa mbali na mauza uza mengine kama vile utwaliwaji wa lilokuwa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) kati ya nyingi? Je Magufuli atatumia miujiza gani kuwasahaulisha watanzania uchafu huu ili waendelee kumwamini na kumuunga mkono kwenye harakati zake zinazoanza kuharibiwa na hii hali ya kuwakingia kifua watawala wa zamani waliotuhumiwa kujihusisha na ufisadi? Je hapa Magufuli anapigana vita na ufisadi gani kama hawezi kuwaacha kila mtu abebe mzigo wake? Je vita ya ufisadi nchini itafanikiwa kwa kuwasulubu dagaa na kuwakumbatia mapapa na bado iendelee kuleta maana kiasi cha kuendelea kuwashawishi watanzania kuwa ni kwa ajili yao hasa wanyonge?
            Tumalizie kwa swali. Je rais Magufuli atafanikiwa kutumikia mabwana wawili?
Chanzo: Tanzania Daima J'pili leo.

No comments: