The Chant of Savant

Wednesday 12 July 2017

Barua ya wazi kwa Halima Mdee

Image result for photos of halima mdee polisi
          Mheshimiwa Halima Mdee,
            Kwanza, pole kwa mazonge yanayokukuta mara mara kwa kutokubali kuwekwa sawa au kuwa ndiyo mzee. Kwa tunaojua thamani na haki ya uhuru wa mawazo, tunakuona kama shujaa ambaye hana wa kumshangilia au kwa kimombo unsung heroine. Hata hivyo, usife moyo; kuna siku ukweli utadhihiri kama ulivyodhihiri juu ya wenzio waliopinga mikataba mibovu wakatukanwa, kukamatwa hata kufukuzwa bungeni. Wewe si wa kwanza. Hivyo, kaza buti. Kimsingi, barua hii ni faraja kwako na machukizo kwa watesi wako. Pia barua hii ni ya kukera kwa wasio na hekima na woga wanaopenda kuambiwa na kusikia wanachotaka kusikia na si kile wanachopaswa kusikia. Kama kijana mahiri, usife moyo kwa kupata misukosuko. Kwani, mfalme Mhubiri 4:13 inasema ni Heri kijana maskini mwenye hekima Kuliko mfalme mzee mpumbavu. Sitaki niseme mengi. Ila wewe si sawa na wale wapumbavu waliogawa nchi yetu kwa wawekezaji waliogeuka wachukuaji. Wewe siyo mchoyo kama wanasheria waliosaini mikataba hii ya kipumbavu na kijambazi ambayo ni moja ya mambo unayopigia kelele ukiachia mbali usawa wa kijinsia.
            Pili, kwa tunaojua thamani ya uhuru wa kuwa na msimamo, tunasherekea ithibati yako ya kutoyumbishwa kwa kile unachoamini. Kawaida, watu wa namna yako ni wachache, hasa akina mama tokana na makali ya mfumo dume. Hivyo, unazidi kujiwekea historia ya mama jasiri ambaye mchango wake utakuja kukumbukwa na kuenziwa siku moja. Akina Bibi Titi walianza kama ulivyoanza. Hivyo, usikatishwe tamaa, kutishwa wala kujiona kama unachukua njia isiyokufikisha mahali. Amini mdogo wangu unachofanya kinafuatiliwa na wengi wanaoelewa kuwa kila lenye mwanzo lina mwisho. Nani mara hii amesahau waliowahi kuwika kwenye unyanyasaji wa raia wakaishia kumezwa na historia wakiwa wamelipwa ipasavyo.
            Tatu, Halima inapaswa kujiuliza swali moja dogu: Binadamu ni nini hadi ajilishe pepo wakati ni udongo tu unaongoja kurejea ulikotoka? Binadamu ni nini wakati ni mfu anayetembea akigemewa kwenda huko walikokwenda wengi wasirudi? Je ni wangapi wanaikubali na kuifanyia kazi busara hii rahisi hasa katika mambo ya umma? Kwa wanaokumbuka waziri wa zamani wa mambo ya ndani Augustine Mrema alivyochachafya waliopinga serikali, wanajua kilichotokea baada ya yeye kufunga virago na kujiunga na hao hao waliokuwa wakiikosoa serikali yake kipenzi.
            Nne, Halima, yakupasa kufahamu kuwa wapo wenye nguvu wanaoweza kufunga mwili wako lakini si mawazo yako. Wanaweza kufunga mikono yako lakini si kinywa chako. Wanaweza kukufukuza bungeni lakini si jimboni.  Wanaweza kudhani wanakunyamazisha wakati wanakufyatua. Wanaweza kudhani wanakutisha kumbe wanakuondoa woga. Hakuna kinachoweza kusimama mbele ya haki. Kwani haki ni haki daima huvunja hata milima aliwahi kuandika mshahiri mmoja wa kale. Hivyo, wanapofunga njia moja nyingine nyingi zinafunguka. Badala ya kulia na kuhuzunika kwa kuwekwa korokoroni, inabidi ushangilie. Wenye kujua thamani ya mchango wako, hatuhuzuniki bali kusherehekea kwa ushindi unaoupata ndani ya kipindi kifupi cha maisha yako na ubunge wako.
            Tano, inakupasa kujua kuwa, hakuna tofali linalofaa kujengea nyumba imara lisilopita kwenye tanuri. Hivyo, kinachopaswa kukuhangaisha siyo kwanini unafukuzwa bungeni, kukamatwa na kuwekwa ndani bali kuangalia kama unachopigania kinawaridhisha waliokutuma kwenda kuwawakilisha. Na isitoshe, anayekufunga wewe hamfungi Halima Mdee bali Mbunge mwakilishi wa wananchi wa jimbo la Kawe. Kwa lugha nyepesi, anayeshughulikiwa si wewe bali wapiga kura wako. Unapaswa kutumia muda huu wa kuwa nje ya bunge kuwaelimisha wapiga kura wako wajue wanavyotendewa ndiyo siyo na vyombo vya dola hasa mihimili mikuu yaani Bunge na Utawala.
            Halima, mwisho naomba nihitimishe kwa kukutaarifu kuwa kwa tunaoujua umuhimu wa ujasiri, ukweli na kutojikomba wala kujigongagonga na unafiki mwingine ili kupata cheo au mlo, tunakusherehekea na kukufanya moja wa mashujaa wetu hata kama hilo hulijui wala kulihitaji kutokana na kutimiza wajibu wako kama binadamu, mbunge, mwanamke na yote katika yote kama mtanzania mwenye mapenzi makuu na mema kwa taifa na watu wake. Nafahamu fika kuwa hata ukiimbiwa zaburi uwasaliti hutawasaliti watanzania. Najua fika, hata ukifungwa minyororo hutageuka bali kukengeuka na kuendeleza msimamo wako. Hata ukiahidiwa vyeo na fedha hutageuka nyuma na kuwa jiwe kama yule mama mpumbavu mke wa Luti aliyegeuka jiwe pamoja na kukanywa au yule msaliti Yuda Iskarioti pamoja na usomi wake. Naamini hutakuwa mtumwa wa tumbo bali mwenye kutumia kichwa badala ya tumbo kuendelea kuwa kwenye uringo wa kisiasa.
            Nakutakia mapambano mema. Ila ushauri wangu ni kwamba utakapo cha mvunguni shurti uiname. Na hakuma masika yasiyo na mbu wala marefu yasiyo nan cha. Hivyo, mwanzo wa masahibu yako unaashiria mwanzo wa ukombozi wa watu wetu kifikra.
            Leo nitakuacha na hekima ya gwiji Martin Luther aliyesema kuwa
Ujasiri ni uamuzi wa mwisho wa ndani wa kwenda mbele hata kama kuna vikwazo. Woga huficha udhalili na kuupa kicho. Woga huzaa kujisalimisha kikondoo kwa masahibu. Ujasiri huzaa ubunifu; woga huuliza kama ni salama wakati uhakika huuliza kama ni busara; kiburi huuliza kama ni sifa. Ila adili huuliza kama ni sahihi; kwani kuna wakati tunapaswa kufanya maamuzi bila kujali kuwa ni salama, busara, umaarufu ila kuhakikisha tunachofanya ni sawa au sahihi.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo

No comments: