The Chant of Savant

Saturday 28 May 2022

Tumeishiwa hadi kutozana madarajani?

Juzi nilikuwa nikiangalia clip niliyotumiwa na rafiki yangu toka Kenya ikionyesha namna wakenya wanavyolipia expressway iliyojengwa hivi karibuni jijini Nairobi. Mradi huu uliozamisha mabilioni ya shilingi unapigiwa upatu kama game changer kuhusiana na msongamano wa magari jijini Nairobi. Mradi huu ni sawa na ule wa Dar Rapid Transit au Daraja ka Kigamboni hata la Tanzanite jijini Dar. Hii ni miradi ya kimkakati na kimaendeleo ingawa nikiangalia namna ya baadhi inavyoendeshwa, sioni mantiki ya maendeleo au umkakati. Nina sababu zifuatazo:
        Mosi, je ni halali wananchi kulipia matumizi ya vitu kama barabara na madaraja yaliyojengwa kwa fedha ima yao ya kodi au mikopo iliyochukuliwa kwa jina lao na kulipwa kwa fedha zao? Mfano mdogo ni hapa Kanada ninapoishi. Japo kuna mataifa yana mfumo wa barabara na madaraja ya kulipia, je hili lina tija kwa nchi maskini kama zetu? Mfano, kuna mantiki gani kwa watanzania kulipia daraja la kigamboni wakati uwepo wake ni sawa na huduma ya kuuganisha maeneo ya Kigamboni sawa na tulivyojenga barabara kwenda mikoani na nchi za nje?
        Pili, kwanini badala ya kuwaumiza maskini ambao wanapata taabu kutumia, mfano, Daraja la Kigamboni, wasitozwe kodi matajiri na kuwaacha maskini waendelee na kuhangaikia maisha  yao bila tozo ambazo zinaepukika kama mamlaka zitasimamia mapato na matumizi ya serikali kwa umakini mkubwa bila kusahau kupambana na ufisadi na ufujaji? Nadhani swali kuu tunalopaswa kuuliza, kuulizwa, hata kujiuliza, (kwa wale walioko madarakani) ni kwanini watu wetu maskini walio wengi wanatozwa kodi na vitu kama hivi vinajengwa kwa fedha yao ima kwa njia ya mikopo, ukasimishaji madaraka ni hao hao ambao ima wao au watoto wao kama siyo kodi zao zitalipia madeni ya ujenzi wa miradi hii tunayowatoza. Inakuwaje watozwe mara ya pili?
        Tatu, je hii modeli ya biashara inawanufaisha watu wetu maskini walio wengi au ni kwa ajili ya wachache ambao wengi wao ima ni wale wanaoishi kwa kuwanyonya au kuwaibia walio wengi au matajiri ambao nao wengi wao wanapata utajiri kutokana na kufanya biashara zenye utata na baadhi ya watendaji wa umma wasioaminika wala kuwa waadilifu wanaoweka maslahi binafsi mbele na wakashindwa kusimamia vilivyo mapato na maslahi ya umma?
        Nne, je hii miradi ni mali ya nani? maana, inapoanza kujengwa miradi kama hii utasikia wakubwa wakisema kuwa wanalenga kupunguza msongamano kwenye majiji,  kuokoa fedha inayopotea tokana na misongamano na kuwaletea maendeleo wananchi. Je msongamano unasababishwa na wananchi au mipango mibaya ya serikali zetu? Je kweli kwa kuwatoza gharama za kutumia hata madaraja na barabara wananchi, mtapunguza misongamano au ni biashara na siasa za majaribio?
  Tano, mbona madaraja tunayovuka kwenye barabara za kawaida hatuyalipii zaidi ya nauli ya kawaida kwa chombo cha kusafiria? Je hapa tofauti yake ni ipi hasa kwa mwananchi, kwa mfano, anayeishi Kigamboni ambaye anakwenda kwenye shughuli zake za kila siku mjini saw ana wale wanaoishi maeneo mengine ya mji ambapo vyombo vya usafiri kama Bodaboda na magari havitozwi tozo kwa kutumia barabara husika? Tunasema haya kwa sababu ukivitoza tozo vyombo hivi, navyo vinahamishia mzigo kwa mlaji ambaye ni raia maskini asiye na uwezo wa kuwa na usafiri wake. 
Sita, je hii ndio njia pekee na sahihi ya kupunguza misongamano au kupiga fedha na kuwaumiza maskini ukiachia mbali kuwabagua kwa kuwazuia kutumia miradi ambayo mingi imekopewa fedha kwa jina lao? Je tumeisha ubunifu hadi kuwalangua wananchi wetu bila ulazima?
Je inahitaji shahda katika mambo ya uchumi kujua kuwa wananchi maskini sasa wana maisha magumu kuliko wakati wowote? Mafuta yamepanda bei kiasi cha kuathiri bei za karibu kila kitu. Inakuwaje mnawatwisha tena mzigo wa kulipia vitu ambavyo vilipaswa kuwa huduma za kawaida kama kweli tungekuwa na maono na utukutu wa kutumia fedha, mali na raslima za umma? Nasema tunawatwisha mzigo usiowahusu hasa ikizingatiwa kuwa: a) tulipodai uhuru, tuliwaaminisha wananchi wetu kuwa tutawaletea maendeleo. Je haya ndiyo maendeleo?, b) pili, wao wanatimiza wajibu wao kama vile kufanya kazi, kulipa kodi na kutii serikali. Je watawala tunatimiza wajibu wetu? Kama tunatimiza, inakuwaje mambo kama haya yanatokea?
Saba, je nini kifanyike kuepuka kadhia hizi ambayo ni ubaguzi wa wazi kwa baadhi ya wananchi hasa wa kipato cha chini? Nadhani yapo mengi yakufanya japo hapa nitataja machache. 
        Mosi, tuwe wabunifu na wenye kujali wananchi wetu. Mfano, tusimamie fedha, mali na raslima za umma vilivyo. Maana, ukiangalia kiasi cha fedha zinazopotea kwenye ufisadi, uzembe, wizi na matumizi mabaya ya umma, utakuta ni nyingi kuliko tunayowakamua wananchi maskini. Je tunafanya hivi kwa sababu maumivu yatokanayo na tozo za vitu ambavyo wananchi hawapaswi kulipia hayatugusi? Je kuna mahali tumekosea?
        Pili, walioaminiwa madaraka watimize wajibu wao kwa wale waliowaamini madaraka huku wakijua kuwa bila kufanya hivyo, wanatengeneza mabomu yanayoweza kuzamisha nchi. Rejea, mfano, kuanza kurejea kwa panya road. Huu ni ushahidi kuwa mambo siyo sawa. Kuna wanaoshiba na wanaolala njaa.
        Mwisho, kwa wale walio madarakani, wajue kuwa wapo ndugu zao wanaoumia. Pia, wajitahidi kuvaa viatu vya maskini wetu walio wengi na kuona kama wangekuwa wao wangetaka wafanyiwe nini.
Leo tutaachia hapa ili kutoa fursa kwa wahusika yaani waathirika, wasomaji na watawala kufanya tafakuri ya kina na kujaribu kuyaangalia madhara ya mambo yanayoendelea ambayo siyo kama vile kuwatoza watu tozo ya kutumia barabara na madaraja.
Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: